Safari ya kufikia mafanikio sio rahisi kama ambavyo wengi wanafikiri. Ni safari ambayo inaweza kuwa ngumu sana hasa pale unapozungukwa na jamii ambayo haioni kile unachokiona wewe. Ili kufikia mafanikio ni muhimu sana wewe kuweka malengo na mipango yako na kisha kuifanyia kazi bila ya kukata tamaa hata kama mambo yanakuwa magumu kiasi gani.
Pamoja na malengo na mipango yako hiyo kuna mambo mengine ambayo unapaswa kuyasisitiza na kuyang’ang’ania ili safari yako ufike salama. Hapa tutajadili mambo 15 muhimu ya kunga’ng’ania ili kuwez akufikia mafanikio;
1. Ng’ang’ania kutimiza malengo yako.
Kwa watu wengine malengo yako yanaweza kuonekana kama mchezo au ndoto za mchana au kitu kisichowezekana kabisa. Usiwasikilize, mara nyingi hawajui walisemalo mpaka waone limetokea. Ng’ang’ania kutimiza ndoto zako ili kuboresha maisha yako.
2. Ng’ang’ania kuwa mkubwa zaidi.
Kwa kile unachofanya hakikisha unakifanya kwa kuleta picha kwamba wewe unajua unachofanya. Fanya kwa ubora zaidi na ongea kwa kujiamini. Kwa kunga’ng’ania kuwa mkubwa zaidi utajiongeze akujiamini na hii itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
3. Ng’ang’ania kusamehe.
Kama kuna mtu yeyote ambaye alikukosea msamehe na endelea na maisha yako. Usipoteze maisha yako kwa kuweka kinyongo na mtu hata kama amekufanyia nini. Ng’ang’ania kusamehe kila mtu ili wewe ubaki na moyo mweupe wa kuweka juhudi zaidi kwenye shughuli zako na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
4. Ng’ang’ania kuiona glass imejaa maji nusu.
Kama ukiwekewa glass ambayo ina maji na kuulizwa unaona nini hapo kuna majibu mawili, unaweza kuona glass ambayo iko tupu nusu au unawez akuona glass ambayo ina maji nusu. Wewe ng’ang’ania kuona glass imejaa nusu. Kwa maana rahisi mara zote una upande chanya wa jambo lolote. Kila jambo ng’ang’ania kuona upande ambao ni chanya ambapo utajifunza zaidi kuliko ukiangalia upande ambao ni hasi.
5. Ng’ang’ania kuwa mkweli kwako mwenyewe.
Mawazo yako ndio yanayojenga tabia zako. Hivyo unapokuwa na mawazo mazuri moja kwa moja utajenga tabia nzuri ambazo zitakuletea mafanikio. Watu wanaweza kukuona vyovyote wanavyotaka, ila wewe kuwa mkweli kwako wewe binafsi. Amua kuwaza mawazo ambayo yatakufanya uweze kufikia mafanikio, usijidanganye hata kidogo.
6. Ng’ang’ania kuzungukwa na watu ambao wanakufanya ukue zaidi.
Wewe ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Ukizungukwa na wazembe watano, wewe utakuwa mzembe wa sita. Ukizungukwa na watu wenye mafanikio watano, wewe utakuwa mwenye mafanikio wa sita. Wanaokuzunguka wana nguvu kubwa sana kwako hivyo hakikisha wanakwenda kule unakotaka kwenda wewe ili muweze kufika pamoja.
7. Ng’ang’ania kujifunza kutokana na makosa.
Ambaye hajawahi kufanya kosa lolote hajawahi kujifunza kitu chochote. Hii ni kauli maarufu sana ila ina ukweli mkubwa, kila mtu anafanya makosa, ila unapong’ang’ania kujifunza kutokana na makosa yako, unafaidika zaidi kuliko kuishia tu kulalamika.
8. Ng’ang’ania kuendela na kile unachoamini.
Kila mmoja wetu kwenye maisha kuna wakati ambao atajaribiwa kuenda kinyume na kile unachoamini. Usijali watu wanasema nini au wanakushawishi nini, simamia kile unachoamini na mwishowe utashinda. Kama ukilegeza kamba na kukubali kuvunja imani yako mwenyewe, huwezi kufanikiwa kwenye jambo lolote.
9. Ng’ang’ania kuondoa kelele zote kwenye maisha yako.
Wakati unakua ulikuwa unapenda sana kufuatilia maisha ya watu na kutaka kujua kila kinachoendelea duniani. Kwa sehemu kubwa hizi ni kelele kwenye maisha yako. Unapotaka kujua maisha ya wengine yameendaje unafikri ni nani anahangaika kufikiria maisha yako? Ondoa kelele hizi na sisitiza yale ambayo ni ya muhimu kwako.
10. Ng’ang’ania kuachana na yaliyopita.
Kuna wakati ambao ni vigumu sana kuachana na yaliyopita, ila kuendelea kuyang’ang’ania kunakuzuia kupata mafanikio makubwa mbeleni. Amua kuachana nayote yaliyopita hata kama wengine wanasema nini. Pata uhuru wa kujua kwamba leo ni siku ambayo unaweza kufanya mabadiliko kwenye maisha yako.
11. Ng’ang’ania mabadiliko na ubunifu.
Huwezi kutatua tatizo kwa ngazi ile ile ambayo imetengeneza tatizo hilo. Kwa kifupi kama maisha yako sasa hivi ni magumu au kuna tatizo, basi unahitaji kubadilika kwanza ndio uweze kutatua tatizo hilo. Ubunifu pia ni muhimu ili kuweza kuleta thamani na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
12. Ng’ang’ania kuwa muaminifu.
Kuwa muaminifusio kitu ambacho ni rahisi kufanya ila ni kitu ambacho ni sahihi kufanya kila mara. Bila ya kujali watu wengine wanasema nini au wanafanya nini, ng’ang’ania kuwa mwaminifu. Kwa kuwa mwaminifu itakujengea imani kwa wengine na itakuepusha na matatizo mengi sana.
13. Ng’ang’ania kuthamini kile ulichonacho.
Kuna wakati ambao unaweza kuona maisha yako ni magumu sana. Lakini ukifikiria kwa kina vitu ulivyonavyo sasa unatakiwa kushukuru sana. Unaweza kulia kwamba wewe huna viatu, kumbuka kuna mwenzako hana hata hiyo miguu ya kuvaa viatu. Ng’ang’ania kuthamini kile ulichonacho na kufanya kazi zaidi ili kuboresha maisha yako.
14. Ng’ang’ania kuusikiliza moyo wako.
Kuna wakati ambapo unatakiwa kusikiliza moyo wako na kufanya kile ambacho utashi wako unakutuma kufanya. Haijalishi watu wanasema nini au kufanya nini, jua maamuzi yoyote utakayoyafanya leo ,wewe ndio utaishi nayo kwa asilimia 100. Hivyo popote ambapo una wasi wasi ng’ang’ania kuusikiliza moyo wako.
15. Ng’ang’ania kujifunza zaidi kila siku.
Kujifunza kila siku ni muhimu sana ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kwa asilimia kubwa utakuwa umezungukwa na watu ambao hawaoni thamani ya kujifunza, wakikuona unasoma kitabu wanakushangaa na kukuona kama unapotea. Usiwajali watu hawa, wewe nga’nga’ania kujifunz akila siku ili kuweza kuboresha maisha yako.
Ng’ang’ania mambo hayo 15 na usiangalie wengine wanafanya nini wala kusikiliza wanasema nini. Ukiwasikiliza sana watakurudisha nyuma na utashindwa kufikia malengo yako.
Nakutakia kila la kheri kwa mwaka huu 2015.
TUPO PAMOJA.
Hakika kocha; haya mambo ni muhimu kunga’anga’nia.
LikeLike