Mwaka huu nitaongeza kipato changu…

Mwaka huu nitafungua biashara yangu…

Nwaka huu nitaacha ulevi….

Mwaka huu nitaanza kufanya mazoezi…

Ndio tumekusikia na malengo yako ni mazuri sana, lakini je unakumbuka malengo haya haya uliyaweka mwaka jana? Na mwaka mwingine uliopita? Kwa nini hujayafikia mpaka sasa.

Kushindwa kujiuliza maswali haya kunakufanya uendelee kushindwa kufikia malengo yako.

Sababu kubwa ya watu kushindwa kufikia malengo yao inatokana na wao kutojua njia sahihi ya kuweka na kufikia malengo hayo. Leo hapa utajiongeza na sababu kumi kwa nini malengo yako hayatatimia mwaka huu 2015 ili uweze kuziepuka.

1. Unaweka malengo ambayo hayaeleweki.

Kwa mfano lengo “mwaka huu nitaongeza kipato” sasa kama kipato chako kwa mwezi kilikuwa milioni moja mwaka huu unaongeza na kufikia milioni moja na elfu kumi umetimiza malengo yako. Lakini kiuhalisia umeshindwa, unapoweka lengo hakikisha unajua ni kiasi gani unataka kufikia.

2. Huna njia ya kujipima.

Kama umeweka malengo halafu nuna njia ya kujipima kama kweli uko kwenye njia sahihi umejiandaa kushindwa. Kitu chochote ambacho hakiwezi kupimwa hakiwezi kufanyika. Jua ni kiwango gani unataka kufika na kila baada ya muda uweze kujitathmini umefika wapi.

3. Unaweka malengo ambayo hayapo ndani ya uwezo wako.

Japokuwa hakuna kisichowezekana, lakini ni vigumu sana kwako wewe kuweka malengo ya kutengeneza bilioni moja kwa mwaka huu wakati kwa sasa kipato chako ni laki mbili kwa mwezi. Kuweka lengo kama hili kunakukatisha tamaa badala ya kukusukuma kulifikia.

4. Huandiki malengo yako.

Kama unajisemea malengo yako na kuyaacha kichwani, subiri baada ya siku chache utakuwa umesahau kila kitu. Malengo na mipango yako yote ni lazima uiandike vizuri kwenye kitabu au karatasi.

5. Unaishi kwenye mazingira ambayo hayachochei malengo yako.

Kama watu wanaokuzunguka hawaoni umuhimu wa kuweka malengo na kuboresha maisha yao, upo kwenye hatari kubwa ya kushindwa kwenye malengo yao.

6. Unakata tamaa pale unapokutana na changamoto kidogo.

Changamoto ni sehemu ya safari hii ya kufikia mafanikio. Kama kila ukikutana na changamoto kidogo unakata tamaa itakuwa vigumu sana kwako kufikia mafanikio makubwa.

7. Unapoteza muda.

Muda ni muhimu sana kwako wewe kuweza kufikia malengo yako. Kama bado unaendelea kupoteza muda huwezi kufikia malengo yako.

8. Huna mfumo wa kukuwajibisha.

Kwa asili binadamu ni wavivu, kama ukijiwekea malengo yako mwenyewe kwa siri, hata usipoyafikia au kuyavunja unajua hakuna atakayejua au kukuuliza. Tafuta mtu ambaye anaweza kuwa anakufuatilia ili kujua kama unaendelea na malengo yako au la. Wakati mwingine tangaza hadharani, kwa mfano kama unataka kuacha pombe, mwambie kila mtu kwamba naacha kunywa pombe, kwa njia hii utaona aibu kunywa kwa sababu kila mtu anajua umesema unaacha.

9. Unaangalia na kusikiliza wengine wanafanya na kusema nini.

Popote ulipo umezungukwa na watu ambao hawajui maisha yao yanaelekea wapi. Hawana malengo yoyote na hawaoni umuhimu wake. Kama utajilinganisha na watu hawa huwezi klusonga mbele kamwe.

10. Umegoma kubadilika.

Kama unataka kuishi maisha yale yale ambayo umekuwa unaishi kila siku halafu unataka ufikie malengo yako nakushauri uache kujidanganya, hakuna kitu kama hiko. Unahitaji kubadilika wewe kwanza ndio mabadiliko mengine yatokee kwenye maisha yako.

Yafanyie mambo hayo kazi ili uweze kufurahia kufikia malengo yako.