Kama tulivyoona kwenye makala iliyopita, uaminifu ni tabia muhimu sana kw amtu yeyote anayetaka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yake.
Kuna watu ambao wanafikiri ukiwa masikini au ukiwa huna mafanikio basi huwezi kuwa mwaminifu. Na watu hawa hufikiri kwamba wakishakuwa na mafanikio basi wataanza kuwa waaminifu. Kosa kubwa sana, haufanikiwi ndio ukawa na uaminifu, ila uaminifu ndio unaanza halafu yanafuata mafanikio.
Kama unataka kutokuwa mwaminifu ili ufikie mafanikio ndio uanze kuwa mwaminifu, hutafikia mafanikio hayo. Kama hutaweza kuwa mwaminifu sasa, hutaweza kufikia mafanikio.
Leo tutaangalia jinsi ambavyo unaweza kujijengea tabia ya uaminifu ili uweze kufikia mafanikio makubwa.
1. Tambua maeneo ambayo yanakushawishi usiwe mwaminifu.
Kila mmoja wetu ana mapungufu/madhaifu yake. Kuna baadhi ya maeneo kwenye maisha yako ambayo umekuwa ukijikuta unakosa uaminifu. Inaweza kuwa ahadi unazotoa kwa watu, inaweza kuwa majibu unayowapatia watu wanapotaka kujua kitu fulani, inaweza kuwa jinsi unavyohadithia watu kitu kilichotokea na pia inaweza kuwa kwenye mahusiano yako na watu wengine.
Kwa kujua maeneo ambayo umekuwa sio mwaminifu itakusaidia kuanza kubadili kile kinachokufanya ukose uaminifu.
2. Jifunze kusema HAPANA, bila kuumiza.
Neno HAPANA, kama utaweza kulitumia vizuri, ni neno lenye uaminifu mkubwa sana. Unaweza kuwa unafanya biashara, akaja mteja na kutaka umpatie bidhaa au huduma ambayo wewe huna au huna utaalamu nayo. Kwa tamaa ya kupata faida unaweza kumwambia ninayo, halafu ukaanza kumtafutia lakini hii inaweza kukuingiza kwenye matatizo makubwa hasa pale kunapotokea tatizo. Njia nzuri hapo ni kusema HAPANA na mteja akaenda kupata bidhaa/huduma hiyo kwa mtu mwingine ambaye ni mtaalamu.
Unaweza kuwa umeajiriwa na aliyeko juu yako kikazi akawa anakupatia majukumu kila muda, kwa kuogopa kuonekana ni mkorofi unakubali kila jukumu unalopewa na hatimaye kushindw akuyamaliza yote kwa wakati na hivyo kukosa uaminifu. Njia nzuri ya kuwa muaminifu ni kumueleza anayekupatia majukumu hayo kwamba hutaweza kuyamaliza kwa wakati kwa sababu bado una majukumu mengine.
Kuw amakini unaposema hapa usionekane ni mkorofi au una kiburi au hujali. Mpatie maelezo muhimu yule ambaye unamwambia hapana. Kama ni mtu anataka bidhaa au huduma ambayo hutoi mwambie huduma hizo huwa sitoi, au sina utaalamu nazo, halafu unaweza kumtajia huduma au bidhaa ulizonazo ambazo pia zinaweza kumsaidia.
3. Wakati mwingine kaa kimya.
Sio kila hali au kila wakati ni muhimu wewe kuongea. Unaweza kujikuta kwenye hali ambayo inakulazimisha wewe udanganye, unapofika katika hali kama hiyo jitahidi sana kukaa kimya. Au kama itakulazimu kuongea basi badili mada na zingumzia mambo mengine ambayo yanaweza kuwa muhimu zaidi.
Kadiri utakavyoweza kukwepa kuzungumzia kila kitu, utajijengea uaminifu mkubwa.
4. Epuka UMBEA na MAJUNGU.
Katika kitu kimoja ambacho kinaua kabisa tabia ua uaminifu ni umbea au majungu. Pale ambapo unashiriki kwenye kumsema mtu kwa ubaya au nyuma ya mgongo wake unajiondolea uaminifu wako wote.
Na umbea/majungu sio lazima useme wewe, kitendo tu cha kukaa na kusikiliza tayari kinakuingiza kwenye kundi la watu wasiokuwa waaminifu. Wakati wowote ambapo watu wanaanza kuongea majungu ni vyema ukaondoka. Au kama mtu anakufuata na kuanza kukuambia maneno ya kimbea/majungu mwambie hapana na ondoka. Ni afadhali kumkatalia mtu huyu mmbea kuliko kusikiliza halafu baadae ikakuvunjia heshima yako yote na kuonekana sio mtu mwaminifu.
5. Tekeleza unachoahidi.
Hiki ndio kipimo kikubwa sana cha uaminifu. Kuongea ni rahisi, tena rahisi sana. Ila vitendo ni hatua ngumu sana ambayo inawashinda wengi. Unapoahidi kwamba utafanya kitu fulani halafu hukufanya, unafikiri ni nani anayeathirika? Wewe uliyetoa ahadi, kwa sababu ukija kutoa ahadi nyingine ni vigumu sana kukubalika maana watu wanajua ulishaahidi halafu ukashindwa kutekeleza.
Kuna nyakati ambazo unasukumwa sana kuahidi vitu ili upate kitu fulani ambacho unakitazamia. Kuwa makini sana usitoe ahadi ambazo hutaweza kuzitekeleza. Kama huna uhakika, ni heri utoe ahadi ndogo halafu ufanye utekelezaji mkubwa kuliko kutoa ahadi kubwa halafu kushindwa kuzitekeleza.
6. Usitafute sababu.
Pale mambo yanapokwenda vibaya, pale tunapokosea na kuharibu mambo, huwa tunafanya nini? Tunatafuta sababu. Na kwa kutafuta sababu huwezi kukosa. Unapofanya makosa na kuanza kutafuta sababu za kusingizia ni kujijengea tabia isiyo ya uaminifu. Unaweza kupata sababu na kuamini ndio imesababisha wewe ukosee, ila utakuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kurudia makosa uliyofanya mwanzo.
Ukitaka kuw amuaminifu, usitafute sababu pale unapokosea. Jua sababu kubwa ni wewe, labda ulikuwa mzembe, labda hukuwa na maarifa ya kutosha. Katika hali hii utachukua hatua ambayo itakufanya usirudie tena makosa uliyofanya.
Wakati mwingine unaweza kukubali tu kubeba lawama, hata kama hujahusika moja kwa moja.
7. Sema kile unachotaka kusema.
Njia muhimu ya kuwa mwaminifu ni kuzungumza mawazo yako. Kama kuna kitu muhimu ambacho unahitaji kusema kiseme, kinaweza kuwasaidia wengi sana. Kama mawazo yako ni sahihi, hayavunji sheria na sio ya umbea/majungu suiogope kuyazungumza hata kama watu watayapinga. Kuwa muwazi na onesha ni jinsi gani ni muhimu kw akile unachosema. Watu watakuelewa na watachukua hatua.
8. Jali hisia za wengine.
Moja ya njia za wewe kuwa muaminifu ni kujali hisia za wengine. Kabla hujamdanganya mtu jiulize atakapojua kwamba umemdanganya atajisikiaje? Kama unaona hatojisikie vizuri basi usifanye hiko unachotaka kufanya. Na hii inakwenda moaka kwenye mahusiano ya kimapenzi na hata ndoa. Kwa kujali hisia za mwenzako itakufanya wewe uache kufanya mambo ambayo hayatampendeza mwenzi wako.
Njia nzuri ya kujali hisia za wengine ni kufikiria kama wao ndio wangenifanyia hiki nachotaka kuwafanyia, je ningejisikiaje baada ya kugundua? Kama usingejisikia vizuri basi na wewe usimfanyie mtu hivyo.
Tumia njia hizi nane kujijengea uaminifu. Fanya mambo hayo kila siku kwenye maisha yako ya kawaida, kazi na hata biashara. Jinsi unavyokuwa mwaminifu, ndivyo watu wengi wanavyokuamini na ndivyo itakavyokuwa rahisi kwako kufikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri,
TUPO PAMOJA.