Iwapo lengo lako ni kudumisha na kuendeleza uhusiano mzuri na watu wengine katika maisha yako, basi mojawapo ya vifaa au zana bora kabisa zinazohitajika ni sifa. Kifaa kingine ambacho, ni kinyume na hicho ni kukosoa. Vifaa hivi viwili, vinaweza kuleta tofauti kubwa ya matokeo yanayotokana na watu wanavyohisi. Tofauti hii ya kuhisi miongoni mwa watu, inaweza kusababisha tofauti kubwa nyingine ya namna watu wanavyofanya kazi. Unawezaje kutumia sifa na kukosoa kuwasaidia watu na kujiletea manufaa na ufanisi?

1. Jifunze  kuwasifia wengine hadharani na kukosoa faraghani. 
Huu ndio ukweli sifa zinapotolewa hadharani, huwafanya watu wahisi kuwa ni bora na wanaofaa kutegemewa. Lakini ukosoaji unapotolewa hadharani huwafanya watu wajihisi kuwa hawafai kitu. Mara nyingi watu wanaoathirika  na lawama au ukosoaji huu wa hadharani, hupanga kulipiza kisasi kwa wale wote waliowapinga ama kuwakosoa, na mara nyingi katika wakati ambao, watu hawa hawakutegemea au hawana habari. Hivyo, ni muhimu kujifunza kusifia hadharani na kukosoa faraghani.

SOMA; Hizi Ndizo Rekodi Ambazo Hazijawekwa Duniani.

2. Unapaswa kurekebisha uwiano wako wa kukosoa na kusifu. 

Mara nyingi tumekuwa na mtazamo wa kukosoa zaidi kuliko kusifia. Sababu mojawapo kwa hali hii ni mwelekeo wetu wakutaka wengine wafanye kwa kiwango kile tunachotaka, tena bila maoni wala ushauri kutoka kwetu. Wanaposhindwa kufanya hivyo, ndipo huwakosoa na kuwatupia lawama nyingi. Na pia tunaamini tunaowajibu wa kuwakosoa na kuwalaumu watu wengine. Matokeo yake tumejikuta tukiwa watu wenye tabia ya kukosoa na kulaumu zaidi kuliko kusifia.

SOMA; Usimlaumu Yeyote, Anza Kujilaumu Wewe.

3. Unapowasifia wengine unapaswa kumaanisha jambo hilo na si vinginevyo. 
Sifa pekee inaweza ikafanya maajabu au miujiza. Hata hivyo inaweza ikawa sawa na kugonga ardhi ngumu au mwamba , iwapo wanaopewa sifa hizo watakuwa hawaamini kuwa, wanasifiwa kikweli na kwa dhati, au kama watahisi kwamba, sifa hizo zimetolewa kwa unafiki. Njia mojawapo ya kuwatolea sifa wenzetu  ni kwa kuwahakikishia  kwamba, sifa hizo tunazowapa zinatokana na mambo mazuri waliyoyafanya au wanayoyafanya ambayo tunahisi kutoka mioyoni kabisa kwamba, yametugusa na yanastahili sifa.

Ukweli ni kwamba, sifa ina nguvu. Na kuendelea kuwasifu na kuwasifu watu wengine, kutawachochea watu hao, waendelee kutenda katika hali na kiwango kinachokubalika kwetu na kwao pia, nap engine hata kuvuka kiwango cha kawaida. Wakati mwingine sisi huchochewa kutenda zaidi na zaidi kutokana na ile haja yetu ya kutaka kutambuliwa na hata kusifiwa na watu wengine, hasa wale wanaotuhusu. Iwapo lengo letu ni kutambuliwa na wengine basi sifa inaweza ikawa sumu kwenye harakati zetu za maisha.

Kumbuka, ni jambo rahisi sana kwa watu kufanya kazi nzuri huku wakitazamia kupata sifa kutoka kutoka kwa watu wengine, na iwapo hawatasifiwa itakuwa ni rahisi kwao kukata tamaa. Hii ndiyo sababu inayofanya mchanganyiko wa sifa na kukosoa ufanye kazi vizuri zaidi kuliko kukosoa peke yake au kusifu peke yake. Hivyo tunashauriwa tulifanye jambo hili kuwa ni tabia yetu, yaani kutoa sifa, bila kusahau kutia moyo. Na kutia moyo huku sharti kuambatane na kusifia.

4. Unapotoa sifa ya kweli na udhati unakuwa unainua heshima kwa wengine. 

Hii ni kwa sababu, kutoa sifa ni suala ambalo, ni adimu sana miongoni mwetu na ndiyo maana, ni rahisi kuwabaini watu wanaofanya hivyo. Na ikumbukwe kwamba, kutoa sifa siyo jambo gumu kama wengine wanavyozani, kwani ni njia rahisi na yenye nguvu inayohusisha uzoefu wa ndani  ya mtu.

Jambo kubwa la kufanya hata hivyo, ni kujitahidi kutazama na kuwa makini nay ale ambayo watu wengine wanafanya. Tunapaswa kutenga wakati wa kuzungumza nao na kujaribu kuwaambia angalau jambo dogo la kuwafurahisha na kuwatia moyo litakalowafanya waifurahie siku.

Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio makubwa na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku kujifunza zaidi, mpaka maisha yako yaimarike.

IMANI NGWANGWALU,

0767 048035/dirayamafanikio.blogspot.com

0713 048 035/ingwangwalu@gmail.com