Wote tunajua kwamba biashara ni wateja, ili biashara iweze kuendelea ni lazima iwe na wateja. Kama una bidhaa au huduma nzuri sana ambayo inaweza kuwasaidia watu wengi lakini hakuna watu ambao wapo tayari kuinunua, huna biashara. Lengo la biashara yoyote ni kutengeneza wateja halafu wateja ndio wanaleta faida na faida inawezesha biashara kukua.

Lakini siku hizi watu wengi wamekuwa wakibadili na kutengeneza malengo yao wenyewe ya biashara. Kuna ambao wanasema biashara ni faida, kwa maana kwamba faida kwao ni kipaumbele, biashara hizi zinaishia kuwana wakati mgumu sana. Kuna ambao wanasema biashara ni matangazo, kwamba jinsi unavyoweza kufanya matangazo mengi ya biashara yako ndivyo inavyoweza kukua. Hizi zote sio maana halisi za biashara na zimewafanya wengi kushindwa kwenye biashara.

Leo tutajifunza mbinu bora na rahisi unayoweza kuitumia kutangaza biashara yako ili uweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Kama tulivyoona, lengo la biashara yoyote ni kutengeneza wateja, lakini hao wateja watajuaje biashara yako? Lazima kuwe na kitu ambacho kitawafanya wateja wajue biashara yako ipo na inaweza kutatua matatizo yao, ndio waweze kuja.

Kuna njia nyingi sana unazoweza kutumia kutangaza biashara yako. Njia ya kwanza na ambayo watu wengi huifikiria kwa haraka ni kutumia vyombo vya habari kama redio, televisheni na hata magazeti. Hii ni njia ambayo imekuwepo kwa muda mrefu na imewezesha makampuni mengi makubwa kutawala soko. Lakini pia imekuwa ni njia ambayo inahitaji fedha nyingi. Kupata nafasi ya tangazo lako kuonekana kwenye televisheni unahitaji kulipa gharama kubwa.

Biashara na kampuni nyingi zimekuwa zinatumia njia hii ili kujitangaza na kufikia wateja wao. Ni njia ambayo imekuwa inawagharimu sana na hivyo kupunguza gharama kwenye maeneo mengine ya biashara ili kuwekeza kwenye matangazo.

Njia hii ilikuwa bora sana kwa siku za nyuma, ila sasa hivi inapoteza nguvu na wanaowekeza kwenye njia hii hawapati uzalishaji unaoendana na uwekezaji waliofanya. Hii ni kwa sababu dunia imebadilika kwa kasi kubwa sana. Sasa hivi watu wanaweza kuwasiliana kwa urahisi zaidi na mawasiliano yao yanafanya njia nyingine ya matangazo kuwa bora zaidi.

Njia ya pili ya kutangaza biashara yako ni kutumia neno la mdomo au ushuhuda. Hii ni njia ya kutangaza biashara ambapo unatoa bidhaa au huduma kwa mtu, inamsaidia sana na yeye anawaambia wenzake kwamba tumieni biashaa au huduma fulani. Hii ni njia bora sana na rahisi kutumia kwenye kukuza biashara yako. Kwa sababu gharama unayoingia ni moja tu, kutoa huduma bora kabisa kwa mteja wako mmoja na mteja huyu atakwenda kutangaza kwa watu wengine wote atakaokutana nao.

Chukua mfano huu; unataka kununua kitu na huna uhakika ununue wapi. Katika pita pita zako unakutana na matangazo ya kampuni A ambayo inajinadi kutoa bidhaa bora sana. Wakati unabadilishana mawazo na marafiki zako wa karibu mmoja anasema jinsi kampuni B ilivyomsaidia yeye katika tatizo kama lako alilokuwa nalo. Je utachagua kufanya biashara na kampuni A au kampuni B? Ni dhahiri kwamba utafanya biashara na kampuni B kwa sababu umepewa sifa na rafiki yako ambaye unamuamini hawezi kukudanganya.

Hii ndio njia bora sana yaw ewe kuweza kutangaza biashara yako, kutoa huduma bora kwa wateja halafu wateja kusambaza habari zako. Na dunia ya sasa ni rahisi sana habari zako kusambaa kwa sababu wateja wachache wakiweka habari zako kwenye mitandao ya kijamii, marafiki zao wote watahitaji kufuatilia kwa undani zaidi.

Makampuni mengi makubwa ya Tanzania, yamewekeza fedha nyingi sana kwenye matangazo halafu yanatoka huduma mbovu sana kwa wateja. Wateja wanalalamika kila siku kwa jinsi wanavyosumbuliwa na kampuni hizi, hii inayafanya makampuni haya kupoteza wateja kila siku licha ya kufanya matangazo makubwa.

Anza sasa kutengeneza wateja ambao wanaamini kwenye biashara yako, wape wateja huduma ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine na watakuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.