Huu ndio ukweli ambao huwezi  kuupinga hata ungefanya nini kuwa binadamu anavyofikiri ndivyo anavyokuwa. Mawazo au fikra zako ndizo zinazokujenga. Haiba na mawazo yako kwa ujumla ni matokeo ya mawazo yako ya kila siku. Ukiwaza na kuishi katika hofu, mashaka na wasiwasi, basi maisha yako yatakuwa katika muonekano huo. Amani ya nafsi kwako itaendelea kuwa kitu kigumu kukipata.

Mawazo yako yakitawaliwa na upendo, amani, ujasiri, kujiamini, maelewano na furaha, basi maisha yako yatachukua sura hizohizo. Ndio maana huwa ni muhimu sana kwa mtu  kubadilisha fikra zake na kujivika fikra chanya. Nataka niseme kwamba amani halisi ya maisha ya mtu ipo kwanza katika mawazo ya mtu. Ukiwa na mawazo yenye utulivu au amani, basi ni rahisi pia kuiona dunia kuwa ni sehemu ya amani.

Utulivu wa nafsi ndiyo mwanzo wa maisha ya furaha. Ridhiko halisi na la kweli lipo kwanza katika mawazo ya mtu. Liko kwanza pia katika nafsi ya mtu. Vitu, watu au mazingira kwa ujumla hayawezi kumletea mtu ridhiko au utulivu wa nafsi. Mawazo chanya yenye utulivu ndani yake, yakijengeka vizuri katika maisha ya mtu, haya huwa ndio msingi mkuu wa maisha ya amani, furaha na mafanikio makubwa.

SOMA; Kwa Nini Ni Muhimu Sana Wewe Kuwa Na Furaha.

 Matatizo mengi humu duniani ukichunguza kidogo utagundua yamesababishwa na pilika pilika za watu kutafuta raha na furaha. Michakato mingi ya kutafuta amani katika maisha ya watu imeleta maafa makubwa hadi sasa. Maafa mengine yamesababishwa na juhudi nyingi za kutafuta nguvu, iwe ya madaraka(kisiasa) au ya kiuchumi. Ingawa jambo la ajabu ni kwamba binadamu hapati utulivu huo anaoutafuta.

 
 
Lakini, unapokuwa na sifa za upendo na amani katika mawazo ya mtu ndiyo siri kuu ya maisha ya amani, furaha na mafanikio makubwa. Ubora huu wa upendo na amani katika mawazo ya mtu ukijengeka vizuri, ndiyo mwanzo wa sifa nyingine kama vile kujiamini na ujasiri. Mawazo mengine chanya huweza kujengeka katika misingi ileile ya amani. Yaani, hizi ni nguvu tosha za kumjenga mtu na kumpatia furaha na amani ya kweli. Hata dini zote duniani bila shaka zinasititiza haya.

Ukiyakaribisha mawazo chanya katika maisha yako, utaanza kujihisi mwepesi. Maumivu ya maisha yataanza kutoweka . Mawazo ya wivu, husuda mbaya, kutokujiamini, woga, aibu za ziada, mashaka, wasiwasi, hofu, ukatili na hata tamaa mbaya vitaanza kukimbia katika maisha yako. Utaanza kuhisi amani tu unaweza ukawa hujui kesho utakula nini lakini mawazo ya amani na utulivu yatakufariji na kukupa nguvu na utakula tu.

SOMA; Hii Ni Haki YakoYakuzaliwa, Usitegemee Kupewa Na Wengine.

Pasipo na mawazo ya amani na utulivu hakuna njia. Usione ajabu mtu kuwa mlevi hadi kuwa sugu. Akilewa anapata utulivu wa mawazo. Anahisi raha, anahisi amani. Japo wote tunafahamu kuwa sifa ile ni ya muda tu, akiamka asubuhi atakuwa anajisikia hovyo zaidi ya jana. Lakini inaonyesha kwamba, utulivu wa mawazo ya kila mtu anaweza kuupata akiamua. Hata Yule aliyeathirika kwa malezi mabaya.

Ukijua namna ya kujipa utulivu mwenyewe kwa njia ya mawazo chanya, hata ndani ya ndoa yako au kazini kwako mambo yatakuwa mazuri. Wanandoa wengine hutegemea sana kupata amani na furaha kutoka kwa wenzi wao. Wakiikosa misuguano huanza. Naomba niseme kwamba, wajibu wa kwanza kabisa uko kwa mtu mwenyewe kujipa furaha, amani, utulivu na kijiletea mafanikio katika maisha yake.

Ukilijua hili na kulishika, inakuwa rahisi kumuathiri mwenzio vizuri avutike kwako. Ataziona hizi sifa zako na kutamani awe kama wewe. Hapo sasa maelewano makubwa yatafuata na utaanza kuona mabadiliko kwa maisha ya wengine na hata ya kwako pia. Lakini pia unapokuwa na utulivu ndani yako, itakusaidia sana hata wewe kufanya mambo yako mengi kwa utulivu hali itakayo pelekea uvute mafanikio makubwa katika maisha yako.

Namalizia makala hii kwa kukuachia zoezi hili litakalokusaidia kukupa msingi mkuu wa amani, furaha na mafanikio katika maisha yako. jifungie ndani ya chumba chako cha kulala, ukimya tu utawale. Kaa kitini vizuri bila madaha. Fumba macho. Yaache mawazo yako yatulie bila kuyumbayumba. Usiwaze hili na lile, ila wazo likija usilifukuze kwa nguvu, liache tu lirande. Akili yako iwe makini na jinsi unavyovuta pumzi ndani na kuitoa. Tumia si chini ya dakika kumi. Ukipenda endelea kidogo, fanya hivi kila siku, hii itakusidia sana kukujengea utulivu mkubwa ndani mwako.

Nakutakia kila la kheri, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kujifunza na kubadili maisha yako kila siku.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika, mpaka maisha yako yaimarike.

  IMANI NGWANGWALU,