Rafiki yangu mpendwa,

Changamoto na matatizo mengi ambayo tunakutana nayo kwenye maisha yetu, chanzo chake kikuu ni hisia ambazo tunazokuwa nazo.

Ndiyo maana wanafalsafa wamekuwa wakifundisha sana kuhusu udhibiti wa hisia zetu, kwa sababu tukishaweza kuzidhibiti hisia zetu, hakuna kitakachotushinda kwenye maisha yetu.

Watu wengi wamefanya maamuzi makubwa kwenye maisha yao kwa kusukumwa na hisia, kitu ambacho kimewaletea matokeo mabaya sana. Wengi wameharibu mahusiano yao kwa sababu ya kufanya maamuzi kwa hisia, wengine wameharibu kazi na hata biashara kwa kushindwa kudhibiti hisia zao.

Katika mahusiano yetu na wengine, zipo hisia mbili mbaya ambazo zimekuwa kikwazo. Hisia hizo ni wivu na chuki.

Kwetu sisi binadamu ni rahisi sana kupata hisia za wivu pale mtu mwingine anapopiga hatua ambazo sisi hatujaweza kupiga. Wakati mwingine hisia za aina hii zinakujia kabla hata hujafikiria kuwa nazo. Unapomwona tu mtu au kusikia mtu amefanya kitu fulani kikubwa, basi hisia hizi zinaibuka ndani yako.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Na hisia za wivu huwa haziji zenyewe, badala yake huambatana na hisia za chuki. Ukishakuwa na wivu na mtu, ndani yako inajengeka chuki fulani, unajikuta unamchukia tu mtu siyo kwa sababu amekufanyia lolote, bali kwa kuwa tu amekuzidi.

Na usiwe na unafiki ukijiambia hilo kwako halipo, jamii nzima ipo hivi, na ukitaka kudhibitisha angalia pale ambapo mtu aliyekuwa amepiga hatua fulani anapoanguka, wengi sana hufurahia, na kusema afadhali alijiona yupo juu sana. Kufurahia pale mtu mwingine anapopata matatizo au kuanguka, ni kudhihirisha chuki ambayo imejengeka ndani yetu dhidi ya wale ambao wametuzidi kwa namna moja au nyingine.

Kwa kuwa kila mtu huingiwa na hisia hizi mbili za wivu na chuki, na kwa kuwa siyo hisia nzuri kwa maisha ya mafanikio, leo nimekuandalia makala inayokufundisha jinsi ya kuondokana na hisia hizi na kwenda kwenye hisia mbili nzuri ambazo zitakusukuma na wewe kufanikiwa zaidi.

Hisia nzuri mbili zitakazokupa wewe msukumo wa kufanikiwa zaidi pale unapowaona wengine wamefanikiwa ni heshima na upendo. Hizi ni hisia ambazo zinakupa msukumo wa kujifunza kwa wale waliokuzidi na kuweza kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.

SOMA; Huu Ndio Msingi Mkuu Wa Maisha Ya Furaha, Amani Na Mafanikio Makubwa.

Swali ni unawezaje kutoka kwenye hisia za wivu na chuki na kwenda kwenye hisia za heshima na upendo kwa wale ambao wamepiga hatua kuliko wewe?

Na jibu ni moja, kujiamini na kuacha kujilinganisha na wengine. Hili ndiyo jawabu ambalo litakuondoa kabisa kwenye hisia hizo mbaya.

Rafiki, unawaonea wengine wivu pale ambapo wewe mwenyewe hujiamini na hujithamini. Pale unapoona wewe huwezi unaona huna namna ya kuwafikia wale waliopiga hatua kuliko wewe. Hivyo unaishia kuwaonea wivu na hata kuwachukia. Lakini kama utajiamini na kujithamini, kama utajua hata wewe unaweza kufanya makubwa, utakuwa tayari kujifunza kwa watu hao.

Pia unapojilinganisha na wengine, lazima utajisikia vibaya, pale unapoanza kuangalia wengine wamefanya nini na wewe umefanya nini, majibu utakayoyapata lazima yatakuumiza. Unachopaswa kujua ni kwamba hakuna unayeweza kujilinganisha naye hapa duniani ila wewe mwenyewe. Kwa kuwa hakuna mtu aliyefanana na wewe kwa asilimia mia moja. Kuna mambo wewe unaweza kuyafanya vizuri kuliko wengine na yapo mambo wengine wanaweza kuyafanya vizuri kuliko wewe.

Hivyo unapoona mtu mwingine ambaye amepiga hatua ambayo wewe hujapiga kwanza heshimu kwa hatua hiyo aliyopiga na kisha jiulize kipi unachojifunza wewe kupitia yeye. Epuka kabisa kujilinganisha na kujiambia mbona wewe hujafikia alipofikia yeye. Jua hutaweza kufikia alipofikia mwingine, bali unaweza kufikia unakoweza kufikia wewe. Jiamini kwamba hata wewe kuna eneo ambalo unaweza kufanya makubwa.

Ukishaheshimu hatua ambayo mwingine amejifunza, wivu unageuka na kuwa pongezi na chuki inageuka na kuwa upendo. Unapompenda yule aliyepiga hatua kuliko wewe, unakuwa tayari kujifunza na wewe kuweza kupiga hatua pia.

Ondoka kwenye kundi kubwa la watu, ambalo linaendesha maisha kwa hisia za wivu na chuki, hasa kwa wale waliofanikiwa, na anza kuwa na hisia za heshima na upendo kwa wale waliofanikiwa. Kadiri unavyowapenda waliofanikiwa ndivyo na wewe unavyopata msukumo wa kufanikiwa zaidi. Lakini ukiwa na chuki na waliofanikiwa, unakuwa kikwazo kwa mafanikio yako mwenyewe.

Upendo ndiyo hisia kuu ya maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. Hakikisha hisia hii inakuwa ndiyo unayotumia pale unapokutana na wengine ambao wamefanikiwa kuliko wewe, kwa kuwa itakusukuma na wewe ufanikiwe zaidi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge