Mpendwa rafiki yangu,

Mwandishi mmoja aliwahi kusema, watu wako bize kuibadilisha dunia kuliko kujibadilisha wao wenyewe kwanza. Kwa asili ya binadamu huwa sisi tunajiona hatuna makosa ila wengine ndiyo wenye makosa. Huwa tunapenda kuwaangalia wengine makosa yao lakini sisi wenyewe huwa hatujiangalii.

Ni rahisi sana kujadili mambo ya watu lakini ni ngumu kwa watu wengi kukaa chini na kujadili mambo yao muhimu. Kama ingekuwa watu wanajitoa kama vile wanavyojitoa kufuatilia maisha ya watu, basi wengi wangeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye kile wanachofanya kwenye maisha yao.

Sisi binadamu tunapenda sana kuonekana tukiwa na mafanikio ya nje kuliko ya ndani. Tunapata shida ya ndani ili kuwafurahisha watu wasiyojali kwenye  kile tunachofanya. Maisha yamekuwa ni utumwa wa watu wengi kuishi vile wanavyotaka wengine na siyo vile wanavyotaka wao kwenye maisha yao.

Mahusiano muhimu unayopaswa kuyaboresha kabla ya mengine ni mahusiano yako ya ndani. Wengi wetu mahusiano yetu ya ndani ni mabaya, tunajitahidi kuboresha mahusiano ya nje ili kuficha udhaifu wetu wa ndani.

Siku zote kama mahusiano ya ndani yakiwa mazuri utayaona hata nje. Tunatakiwa kubadilisha kwanza mahusiano yetu ya ndani. Kwanza unaweza kukuta watu wengi wanaishi na vinyongo vya wao kwa wao. Wanapigana na vita na nafsi zao za kushindwa hata kujisamehe wao wenyewe.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Sisi wenyewe tumekosa ushirika mzuri na nafsi zetu, tumeshindwa kujirekebisha ndani tunataka kurekebisha ya nje. Hatutaweza kufanikiwa kwenye mahusiano ya nje kama ya ndani hayajakaa vizuri.

Angalia mahusiano yako na familia ni mazuri? Vipi kuhusu mke au mume wako? Muda mwingine unakuwa ni unafiki kutaka kuonekana nje ni watu safi wenye mahusiano yenye afya lakini ndani yetu mahusiano yetu hayana afya.

Mahusiano ya ndani yakiwa vizuri,hata utendaji wetu wa kazi utakuwa mzuri. Ufanisi utaonekana nje, watu wengi kwenye mahusiano hawafurahii mahusiano yao bali wanavumilia mahusiano ambayo wanayo.

Hujaumbwa kuja kuvumilia mahusiano yanayokuumiza bali unaingia kwenye mahusiano ili kufurahia maisha kupitia yule uliyemchagua kuwa naye. Jenga utamaduni wa kuboresha mahusiano yako ya ndani kuwa vizuri, hakikisha mahusiano yako ya ndani yanakuwa vizuri sana.

SOMA;Jinsi Ya Kubadili Hisia Mbaya Za Wivu Na Chuki Kwenda Hisia Nzuri Za Heshima Na Upendo.

Punguza muda wa kufuatilia mahusiano ya watu na tumia muda mwingi kujenga mahusiano yako ya ndani ili yawe bora. Mahusiano yetu ya ndani yakiwa vizuri tunapata afya karibu kila eneo la maisha yetu. Kama mahusiano yetu ya ndani yako vibaya hata nje tunakuwa tumechakaa, hivyo ni vema kukarabati mahusiano yetu ya ndani.

Hatua ya kuchukua leo, weka juhudi kubadilisha mahusiano yako ya ndani, acha kuhangaika kuboresha mahusiano ya wengine kabla hujaboresha ya kwako.

Kwahiyo, maisha ni mahusiano. Tunaweza kukwepa yote lakini siyo kukwepa mahusiano yetu ya ndani. Hivyo jitahidi kuangalia mahusiani yako yanakuwa yanakuwa na afya kwani hatuwezi kuwa na mahusiano bora ya nje kama hatuna mahusiano bora ya ndani.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana