Kuna swali ambalo huwa linaulizwa tena na tena na tena yaani kila siku swali hili linaulizwa. Hata nitakapomaliza kuandika hapa, mtu akipiga simu au kuandika email atauliza swali hilo.
Swali lenyewe ni NIFANYE BIASHARA GANI AMBAYO INA FAIDA SANA, au NI BIASHARA GANI AMBAYO INALIPA SANA KWA SASA. Na jibu langu limekuwa moja mara zote, KILA BIASHARA UNAYOONA WENGINE WANAFANYA, INALIPA.
Sasa leo hatutajadili kuhusu biashara gani inalipa na ipi hailipi au kwa nini kila biashara inalipa. Nitakupa link hapo chini uweze kupitia hilo.
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kujua Biashara Inayolipa Eneo Ulipo.
Leo nataka tujadili ukweli mmoja ambao wengi hawapendi kuusikia. Ukweli wenyewe ni wkamba huwezi kuwa sahihi kwa mara ya kwanza. Hata ukiingia kwenye biashara inayolipa kiasi gani, hata ukawa na mtaji wa kukutosha, hata ukawa na washauri wazuri kiasi gani, bado mara ya kwanza utakutana na changamoto. Utakuwa umeweka mpango mzuri lakini ukifika sokoni mambo yanakuwa tofauti.
Unaweza kufikiri bidhaa au huduma fulani ndio itakayokuletea faida, unakuja kukuta hiyo ndio mzingo na nyingine ambayo hukudhania ndio inafanya vizuri. Hakuna anayeweza kuitabiri kesho na ndio maana hakuna anayeweza kuwa sahihi kwa mara ya kwanza.
Sasa hii inakusaidiaje wewe mfanyabiashara? Inakusaidia jambo moja muhimu sana, usisubiri mpaka uwe kamili ndio uanze kitu au kuendeleza kitu. Kama kuna kitu ambacho unataka kufanya, anza kukifanya. Mwanzoni utakutana na changamoto na kukosea lakini ndio utajifunza kipi kinamantiki na kipi hakina mantiki. Utajua ni mipango gani inafanya kazi na ipi haifanyi kazi. Na hivyo utakuwa na nafasi nzuri ya kubadilika na kuwa bora zaidi.
SOMA; Ukiwa Na Kitu Hiki Ni Mwanzo Mzuri Wa Kufanikiwa Katika Uwekezaji.
Hakuna kanuni moja ya mafanikio kwenye biashara kwamba ukifuata hiyo una uhakika wa kufanikiwa. Ingekuwepo kila mtu angekuw amfanyabiashara mwenye mafanikio. Unahitaji kufanya majaribio mengi ili uweze kuja na kanuni yako ambayo itakufikisha wewe, yaani wewe tu kwenye mafanikio. Wengine wakiiga, kama ambavyo wengi wanafanya, wanashangaa wanashindwa wakati wewe unachanja mbuga, baadae wanasema wewe una dawa, wewe ni freemason au umewafanyia mchezo mbaya. Kumbe wameshindwa kufanya zoezi dogo sana la kufanya majaribio na kujua ni kitu gani kinawezekana kwao na kukomaa nacho.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.