Biashara mpya zina kasi kubwa sana ya kushindwa. Hapa kwetu Tanzania hatuna tafiti za kutosha ila kwa nchi zilizoendelea na zilizofanya tafiti, biashara 8 kati ya 10 zinazoanzishwa hufa mwaka mmoja baada ya kuanzishwa. Hii ni hatari sana na kwa uzoefu tu hapa kwetu hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Kuna sababu nyingi zinazopelekea biashara hizi mpya kufa, ila leo nataka tujadili eneo moja muhimu sana unalotakiwa kuzingatia. Pamoja na kupata elimu ya biashara na kuweka mipango unayoitekeleza, kuna eneo moja muhimu ambalo usipokuwa makini litakupoteza.
Eneo hili ni mtaji unaoanza nao biashara. Kama unaona biashara yako inahitaji mtaji wa milioni kumi ndio ianze, basi usitafute milioni kumi na kuweka fedha zote kwenye biashara. Bali anza na kiasi kidogo zaidi ya hapo au kama milioni 10 ndio kiasi kidogo, basi hakikisha una kiasi cha zaidi ya hapo. Kama ukiweka fedha yote ya mtaji mwanzoni mwa biashara, unajiandaa kushindwa kwa kasi ya ajabu sana.
Biashara yoyote mpya ina changamoto nyingi ambazo huwezi kuzitabiri wala kuziweka kwenye mpango wako wa biashara. Unahitaji kuwa na kiasi cha fedha cha ziada ambacho utaweza kukitumia kuokoa jahazi pale ambapo mipango yako ya mwanzo haitakwenda kama ulivyotarajia.
Kama utachukua mtaji wote na kuuweka kwenye biashara mwanzo, utapata changamoto na utashindwa kuitatua kwa kuwa huna fedha nyingine. Na utaiona biashara yako inakufa kwa kukosa kiasi fulani cha fedha ambacho ni kidogo ukilinganisha na mtaji uliowekeza.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.