Habari ndugu mpendwa msomaji wa makala za kilimo katika jukwaa la AMKA MTANZANIA. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na mchakato wakuelekea kwenye mafanikio. Wiki iliyopita tulianza kujifunza kilimo cha nyanya. Leo tutaendelea pale tulikoishia, na tutajikita katika utunzaji wa nyanya zikiwa shambani, wadudu waharibifu pia tutaangalia uvunaji wa nyanya masoko pamoja na bei za nyanya.

Kama hukusoma makala ya wiki iliyopita, isome hapa; Kilimo Bora cha Nyanya; Maandalizi Ya Mbegu, Shamba Na Upandaji Wa Miche.

Utunzaji wa shamba la nyanya:
1.      Uwekaji wa matandazo (Mulching)
Matandazo yanasaidia kufunika ardhi ili kutunza unyevunyevu, kuzuia magugu, pia matandazo yanasaidia kuzuia matunda ya nyanya yasigusane na udongo ambapo yanaweza kuoza. Matandazo yanaweza kua ya aina mbalimbali, kama vile majani makavu, nyasi au hata maranda yanayatokana na miti wakati wa upasuaji mbao (sawdust). Matandazo ya aina hii ni mzuri zaidi ya yale ya plastiki ambayo sio rahisi kuoza. Matandazo ya nyasi, maranda au majani yakioza yanakua mbolea nzuri na kurutubisha ardhi. Uwekaji wa matandazo una ufanisi kwenye kilimo cha eneo dogo, ila kwa maeneo makubwa, upatikanaji wa matandazo unakawa ni changamoto.
2.     Kusimika miti ya kufungia mmea
Uwekaji wa miti/mambo kwa ajili ya kusaidia mmea wa nyanya, kunasaidia nyanya zisianguke au kutambaa kwenye udongo kitu ambacho kinaweza kusababisha madhara kama magonjwa.  Miti inapaswa kuwekwa wiki 2 hadi 3 baada ya upandikizaji wa miche. Uwekaji wa miti unasaidia ukuaji wa nyanya na hivyo kupelekea kuzaa zaidi. Kwa aina ndefu za nyanya uwekaji miti hauepukiki ni lazima uweke miti ya kueleweka ambayo itaruhusu ukuaji mzuri, pia miti lazima iwe imara ili kuweza kustahimili mzigo wa nyanya pindi nyanya itakapokua imezaa vizuri.
3.     Umwagiliaji
Nyanya hazivumilii ukame. Mavuno yanapungua kwa kiwango kikubwa endapo nyanya zitakosa maji. Ni muhimu kumwagilia mara kwa mara, hasa kama nyanya unalima kipindi cha kiangazi ambapo hakuna mvua.  Kiwango cha maji ya umwagiliaji kinategemea aina ya udongo pamoja na hali ya hewa. Mfano kama  hakuna mvua na udongo ni wa kichanga unahitajika kunyeshea mara 3 kwa wiki, hii ni kwa sababu udongo wa kichanga unapoteza maji kwa haraka. Ila kama hali ya hewa ni nzuri na udongo ni tifutifu basi umwagiliaji mara moja kwa wiki unatosha. Aina ya Umwagiliaji itategemea na miundombinu ya umwagiliaji, aidha mifereji, umwagiliaji wa matone (drip irrigation) n.k
4.     Udhibiti wa magugu (Palizi)
Palizi inapaswa  kufanyika  wiki 2 au 3 baada ya upandikizaji, ila pia inategemea na uotaji wa magugu katika eneo husika. Hakikisha shamba lako linakua safi bila magugu, maana magugu huvutia na kuficha wadudu na magonjwa. Magugu pia yana uwezo  mkubwa wa kutumia virutubisho vilivyomo ardhini kuliko mazao, ndio maana magugu  yanakua haraka kuliko mazao shambani. Hivyo hakikisha unafanya palizi mara 3 au 4 kulingana na kasi ya uotaji magugu.
5.     Uwekaji wa mbolea
Mbolea ya kupandia huwekwa wakati wa kupandikiza, unaweka 5g kwenye shimo moja( gramu 5 ni sawa na kifuniko cha soda kimoja). Mbolea ya kupandia unaweza kutumia DAP, au Minjingu.  Mbolea ya kukuzia unaweka wiki 2 au 3 baada ya kupandikiza. Ni vizuri mbolea inapowekwa shamba liwe safi, liwe halina magugu, kama kuna magugu fanya palizi kwanza. Mbolea ya kupandia unaweza kutumia Urea.
6.     Wadudu
Nyanya ni moja ya mazao yanayopendwa sana na wadudu, kutokana na majani yake ni laini. Wadudu wengi hasa wale wanaofyonza (sucking insects) wanapendelea mazao ya jamii ya nyanya. Kwa upande wa wadudu nitawataja tu baadhi, japo wengine majina ya Kiswahili ni changamoto nitaweka majina yao kama yalivyo.
·        Aphids – Kuna sehemu wanawaita wadudu mafuta, hupendelea kukaa chini ya majani, ukiona jani limejikunjakunja, ukilifunua kwa chini utakutana na hao wadudu, wapo wanaofanana na majani
·        Whitefly (inzi weupe).. Hawa ni rahisi kuwatambua maana ni weupe ila wadogo, hupendelea majani machanga yale ya juu. Pia wadudu hawa husambaza virusi vinavyosababisha ugonjwa unaoitwa TYLC (Tomato yellow leaf Curl)
·        Cutworms – hujulikana kama SOTA – huishi kweny udongo. Mdudu huyu ni hatari karibu kwa mazao yote. Hukata shina la mmea na kusababisha mmea kutoota tena
·        American bollworm – Mdudu huyu hushambulia matunda ya nyanya, hutoboa matunda ya nyanya kuanzia matunda yakiwa na wiki 3 hadi karibu na kukomaa
·        Minyoo fundo [(Root Knot Nematode) – Husahmbulia mizizi ya nyanya
7.     Baadhi ya dawa za kudhibiti wadudu:
Kwa sasa zipo dawa nyingi kama utitiri za kudhibiti wadudu. Maana majina ya kibiashara ni mengi  ila kiambato kinafanana. Mfano dawa Confidor SL 200  na Attakkan C350 zote zina kiambato (active ingredient) kinachofanana cha –Imidacloprid. Kwa kifupi, kiambato ndio sumu yenyewe. Unaponunua dawa angalia Kiambato (active ingredient) cha dawa, maana unaweza badilisha dawa kumbe umenunua ileile sema majina ya kibiashara tu ndio tofauti.
Dawa
Kiambato
Wadudu wanodhibitiwa
Actara 25 WG
Thiamethoxam
Aphids, whiteflies
Confidor SL 200
Imidacloprid
Termites, Leafminer, Whiteflies,Thrips, Aphid
Brigade
Bifenthrin
Aina nyingi ya wadudu
Actellic 50EC
Pirimiphos-Methyl
Thrips, Aphids, Whiteflies,Caterpillars,Mites
Bulldock Star
Beta-cyfluthrin & Chlorpyrifos
Caterpillars, Bollworms Aphids, Thrips
Orodha ya dawa ni ndefu kidogo, nimetoa hizo chache tu hapo.
8.     Uvunaji na Utunzaji wa nyanya baada ya kuvuna
Nyanya ina maisha mafupi baada ya kuvunwa, ni rahisi kuharibika maana sehemu kubwa ya nyanya ni maji. Upotevu wa mavuno baada ya kuvuna  inakadiriwa kua asilimia 5 hadi 50. Upotevu wa mazao baada ya kuvunwa husababishwa hasa na utunzaji duni wa mazao hayo, njia duni za usafirishaji, pamoja na kuchelewa kuvuna. Kupunguza upotevu unashauriwa kuvuna kwa wakati nyanya zako. Maana nyanya zilizoiva sana, ni rahisi kuharibika wakati wa uvunaji na hata wakati wa kusafirisha maana ganda lake la nje linakua ni laini.  Kama soko lako liko mbali vuna nyanya zikiwa ndio zimeanza kuonyesha dalili ya kuiva maana wakati huo nyanya inakua na ganda gumu hivyo kuweza kuvumilia mikikimikiki ya usafirishaji. Lakini pia nyanya itaweza kukaa muda mrefu zaidi bila kuharibika ikilinganishwa na ile iliyovunwa ikiwa imeiva sana. Ila pia zipo aina za nyanya zinazokaa muda mrefu wa hadi wiki 3 bila kuharibika kama zikitunzwa vizuri mfano Tanya na Cal J
Wakati wa usafirishaji hakikisha unaweka nyanya kwenye  vifungashio imara kama kreti ama boksi. Ukiweka kwenye mifuko ni rahisi nyanya kupondeka kutokana na mtikisiko pindi zisafirishwapo hasa kama barabara zenyewe ni za vijijini.
9.     Masoko ya nyanya:
Kuna aina kadhaa za masoko ambapo nyanya zinaweza kuuzwa.
1.     Kuna masoko ya kawaida kama Kilombero, Arusha, Kariakoo Dar, soko kuu Morogoro, Buhongwa, Mwanza, na masoko mengine kama hayo yaliyotapakaa nchi nzima. Changamoto ya masoko haya unapitia msururu wa madalali, kila mmoja anataka naye apate.
2.     Masoko ya kitaasisi kama supa markets,  mahotelini, hospitali, mashule n.k
3.     Masoko ya kiviwanda kama vile Darsh Industries maarufu kama REDGOLD ambao wako arusha , wao wanazalisha bidhaa nyingi zinazotokana na nyanya kama Tomato Sauce. Pia kipo kiwanda kinaitwa IVORI Iringa kinachotumia nyanya kama malighafi
4.     Masoko ya nje.
Aina hizo tatu za mwisho zinahitaji ubora wa hali ya juu, ndio maana wachache ndio wanaofaulu kuuza kwenye masoko hayo. Mfano masoko ya nje bidhaa yako lazima ikidhi vigezo vya kimataifa au vya nchi husika.
10.                       Bei za nyanya:
Bei za nyanya zinategemeana na misimu na aina ya soko. Kwenye masoko haya kawaida Bei ya nyanya mara nyingi inakua kubwa kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Machi au hata Aprili.  Kipindi cha kuanzia mwezi October uzalishaji unakua ni mdogo maana watu wachache ndio wanazalisha, maana kipindi hicho changamoto ni nyingi, kwanza maji ya ni tatizo maana wazalishaji wengi wanategemea mvua. Hivyo wale wachache walioko kwenye vyanzo vya maji ndio wanaozalisha. Lakini pia kipindi hicho kuna changamoto kubwa ya wadudu na magonjwa, hii hupelekea mavuno kua madogo na gharama za utunzaji nazo ni kubwa.  Kipindi hichi bei ya nyanya shambani ni Shs. 6,000 hadi 12,000 kwa ndoo ya lita 20. Bei ya sokoni hua ni Shilingi  9,000 hadi 25,000 kwa ujazo wa ndoo ya lita 20.
Msimu wa mwezi wa Aprili hadi Septemba bei ya nyanya inakua chini, maana uzalishaji ni mkubwa, maeneo mengi hali ya hewa ni nzuri kwa uzalishaji. Kipindi hichi bei ya nyanya ni 2,000 hadi 5,0000 kwa ndoo ya lita 20.
Hiyo ndio hali ya kwenye masoko ya kawaida. Kwa upande wa masoko rasmi (viwanda, mahoteli, masoko ya nje), hakuna mabadiliko makubwa ya bei kama ilivyo kwenye masoko hayo mengine, japo mabadiliko yapo. Mfano kama Tomato sauce inauzwa 5,000 kwa kopo moja, huwezi kusema kwa vile huu ni msimu wa nyanya nyingi basi uuziwe 3,000/=, hivyo tunategemea hata wale wanaouzia  viwanda nyanya kama malighafi bei inakua ina msimamo kiasi fulani.
Hata hivyo pamoja na hayo yote, ili uweze kupenya kwenye soko na kulifaidi soko lazima uwe mbunifu. Kumbuka mjasiriamali haishii tu kufuata soko, bali analitengeneza soko. Lazima uwe mdadisi, ufanye kwa utofauti.  Lengo la kujifunza hapa ni kukupa msingi mzuri wa kua mbunifu. Nakuachia kanuni hizi za kuliteka soko: Ya kwanza kua mbunifu, ya pili kua mbunifu na kanuni ya tatu nasema kua mbunifu.
Asante sana. Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Kwa ushauri au maswali, Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.comau dd.mwakalinga@gmail.com