Leo naomba tujadili kidogo kuhusu mtu kumchukia mwingine.

Labda tuseme wewe kuna mtu anakuchukia, na amekuwa akikuonesha
wazi wazi kwamba anakuchukia. Na hapa wewe huna tatizo lolote na mtu huyu.
Unajaribu kuishi maisha yako bila hata ya kuingilia maslahi yao wala kuwavurugia
chochote ambacho ni chao, lakini mtu anachagua tu kukuchukia.

Unajisikiaje katika hali kama hii? Unaumia kwa sababu
ulitegemewa mtu ambaye ni wa karibu kwako awe pamoja na wewe badala yake
anakuchukia? Unajaribu kumbadili mtu labda akupende?

Leo nataka nikupe sababu kwa nini mtu anaweza kukuchukia na njia
bora ya kuondokana na chuki hiyo.

Kwanza kabisa mtu anapokuchukia sio kwamba anakuchukia wewe, ila
anajichukia yeye binafsi. Ni hivyo tu. Mtu kuna kitu ambacho kinamsumbua kwenye
maisha yake na hataki kukikubali, hivyo anayachukia maisha yake, kwa sababu
hataki kukubali hilo pia anatafuta mtu wa kumchukia ili angalau aone tatizo sio
lake. Si unajua tabia za wakwepa majukumu?

Hivyo atajipa kila sababu kwa nini anakuchukia wewe, lakini wewe
huna tatizo lolote na yeye kukuchukia, hakuna chochote ambacho umemharibia.
Labda umeamua tu kubadili maisha yako na kwa kuwa huyo anayekuchukia hawezi
kubadilika basi anakuchukia. Kwa mfano ulikuwa na marafiki wa karibu kila siku
mnakunywa pamoja, wewe ukakaa chini na kuona kunywa kwenu hakuna faida yoyote,
hivyo ukaamua kuacha utaratibu huu wa kukutana baa kila siku na ukaanza
kujifunza na kujishughulisha na vitu vya pembeni(fanya hivi kama bado una
utaratibu wa kuhudhuria vikao vya baa kila siku). Unafikiri ni nini kitatokea
kwa marafiki zako hao? Watakuchukia. Sasa hebu jiulize wanakuchukia kwa sababu
wewe umeamua kuacha kukaa vikao hivyo kila siku? Hapana, wanakuchukia kwa sababu
wewe unaanza kuwa bora kuliko wao. Kwa mfano ingetokea huna tena kazi na hivyo
huna fedha ya kwenda baa kila siku unafikiri wangekuchukia? Hawawezi kukuchukia,
watakuonea huruma tu na wataendelea na utaratibu wao.

Hivyo kama kuna mtu yeyote ambaye anakuchukia, wala usijiumize
kichwa ufanye nini ili aache kukuchukia, endelea kufanya unachofanya na mwache
ajiue mwenyewe na chuki zake. Maisha ni mafupi sana mpaka uanze kupata muda wa
kumfurahisha kila mtu.

Usikubali uhusiano wowote wa kindugu au kirafiki uwe kikwazo
kwako kuishi maisha unayotaka kuishi wewe, kama huvunji sheria. Hata kama kuna
atakayekuchukia hawezi kukuchukia zaidi ya miaka 100 ijayo, kwa sababu wote
mtakuwa mmekufa na hakuna atakayekuja kukukumbusha kwamba nilikuchukia sana
duniani, kama mtakutana peponi.

SOMA; Hiki Ndio Kitakachotokea Miaka 100 Ijayo..

Maisha ni yako chaguo ni lako, kama kuna mtu anakuchukia muonee
huruma na achana naye, wala hata usimfikirie, wewe endelea kuweka juhudi kwenye
kile unachofanya na unachotaka kuwa bora.

TAMKO LA LEO;

Najua kwamba mtu yeyote anayenichukia sio kwa sababu ananichukia
kweli, ila ni kwa sababu anajichukia yeye mwenyewe. Mimi sina muda wa kuanza
kufikiria kuhusu anayenichukia, ni bora nikatumia muda huo vizuri kujiendeleza
kuwa bora zaidi kwenye hiki ninachofanya.

Tukutane kwenye ukurasa wa 184 kesho, Like page yangu ya
Coach
Makirita Amani
uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha
kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.

Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.

TUPO PAMOJA.