Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutengeneza Kipato Kupitia Mitandao Ya Kijamii.

Mwaka jana tuliandaa semina kwa njia ya mtandao ambapo tulitoa elimu ya jinsi ya kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kutumia blog. Baadae tulitoa kitabu ambacho kiliendelea kutoa elimu hii ya kumwezesha mtu yeyote kutengeneza biashara yake kupitia mtandao kwa kuw ana blog ambayo inatoa elimu fulani watu wanayohitaji.
Watu wengi wamejipatia kitabu hiki na wengi wamefungua blog zao ambazo sasa zimeshaanza kupata wasomaji ambao wanazifuatilia kwa makini. Unaweza kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki kwa kusoma JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG.
Ili uweze kutengeneza fedha kwenye mtandao kwa kutumia blog kwanza itakuhitaji muda wa kuanza kujenga wasomaji wanaokuamini, itakuhitaji wewe ujifunze sana na ujiweke kama mtaalamu kwenye lile eneo ambalo umechagua kuandikia na kutoa elimu kwa watu wengine. Pia utahitaji kuwa na kompyuta ili uiendeshe blog yako kitaalamu zaidi. Sasa mahitaji haya yanaweza kuwa kikwazo kwa watu wengi ambao wanataka kutengeneza kipato kupitia mtandao.
Leo nakushirikisha njia nyingine ya kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kutumia mitandao ya kijamii. Wote tunajua kwamba dunia ya sasa karibu kila mtu yupo kwenye mtandao wa kijamii. Kuna mitandao ya kijamii ambayo ni maarufu na watu wengi wanaitumia, hata wewe pia unaitumia. Sasa leo nataka nikupe ujanja wa jinsi unaweza kuitumia mitandao hiyo kutengeneza kipato ili uweze kubadili hali yako ya kipato.

 

Ni mitandao ipi ina watumiaji wengi kwa hapa Tanzania?

Kwa Tanzania kuna baadhi ya mitandao ya kijamii ambayo ina watumiaji wengi sana. Kwanza kabisa ni mtandao wa kijamii unaoitwa facebook, huu ndio unaongoza duniani na hata hapa tanzania umejizolea watumiaji wengi sana. Karibu kila mtu anayetumia mitandao ya kijamii yupo facebook.
Mtandao mwingine wenye watumiaji wengi ni instagram. Huu ni mtandao ambao umechipukia kwa kasi sana hapa tanzania na umepata umaarufu mkubwa na watu wengi kuufuatilia. Ni mtandao ambao ni rahisi sana kutumia na kule watu wanaweka picha tu na maelezo.
Twitter nao pia ni mtandao wa kijamii ambao watanzania wengi wanatumia, ila waliomiliki sana mtandao huu ni watu maarufu kwenye jamii kama viongozi au wasanii. Twitter sio mtandao ambao unavutia wengi kuwepo kwa sababu unahitaji kuweza kutoa ujumbe kwa maneno machache sana na hivyo hii ni changamoto kwa wengi.
Linkedin pia ni mtandao wa kijamii ambao umekaa kitaaluma na kitaalamu zaidi. Kupitia linkedin mtu anaweza kuweka wasifu wake na nafasi anazoweza kufanyia kazi na ikawa rahisi wenye uhitaji kumfikia. Ni mtandao ambao haujakaa kiumbea umbea kama mingine na hivyo hauna watumiaji wengi kutoka Tanzania.
Kwa madhumuni ya makala hii nitajadili mitandao miwili ambayo watanzania wengi wanaitumia ambayo ni facebook na instagram.

Je inawezekana kutengeneza fedha kwa kupitia mitandao ya kijamii?

Watu ambao wana marafiki au wafuasi wengi kwenye mitandao hii ya kijamii wamekuwa wanatengeneza fedha kupitia mitandao hii. Watu hawa hufanya kazi na makampuni yanayohitaji kujitangaza na makampuni hayo kuweka matangazo kwenye kurasa zao kwenye mitandao hii na hivyo wao kutengeneza kipato. Na ili kuhakikisha wanaendelea kutengeneza kipato wanatafuta njia bora za kukutumia wewe.
Wanachotaka ni wewe uwe na hamasa ya kuwafuatilia na ukifika pale unakutana na matangazo mbalimbali. Watu hawa wenye wafuasi wengi wamekuwa wakitengeneza ugomvi usio na maana ili tu kuwafanya watu wengi wawafuatilie na hivyo wao kukuza biashara zao za kuuza matangazo.
Makampuni mengi yamekuwa yakitafuta njia nzuri ya kutangaza biashara zao kupitia mitandao hii ya kijamii na njia kubwa wanayoiona ni nzuri ni kutumia watu wenye wafuasi wengi.

Wewe unawezaje kutengeneza kipato kupitia mitandao hii?

Swali zuri sana, na hapa ndio ninataka nikupe maarifa ambayo yatabadili maisha yako kama utayatumia. Tumeshaona mitandao ya kijamii inayotumika sana kwa tanzania na pia tumeshaona kwamba inawezekana kutengeneza fedha kwenye mitandao hii ya kijamii kama ambavyo tayari kuna watu wanaotengeneza fedha kupitia mitandao hii.
Sasa je wewe unawezaje kutengeneza fedha pia? Kumbuka labda wewe sio mtu maarufu hivyo una wafuasi au marafiki wachache. Na makampuni mengi yanayotaka kutangaza kupitia mitandao hii wanataka watu wenye wafuasi wengi.
Hapa ndio wakati wa kutumia akili yako vizuri na ukiweza kufanya hivi utatengeneza kipato kikubwa mpaka mwenyewe utashangaa ulikuwa wapi hukujua hilo mapema. Hivyo twende pamoja na fanyia kazi yale ambayo unajifunza hapa.
Tuseme wewe ni kijana ambayo huna kazi ila una simu yenye uwezo wa kuingia kwenye mitandao hii. Kama umeshatumia mitandao hii kwa muda umeshajijengea marafiki na wafuasi kadhaa kupitia mitandao hii. Lakini siku zote umekuwa unaingia kwenye mitandao hii na kutoka bila ya kutengeneza kipato chochote.
Sasa leo nataka uwe na mpango tofauti. Kama tulivyoona hapo juu ni kwamba makampuni mengi yanakimbilia kutangaza kupitia watu wenye wafuasi wengi. Makampuni haya yanata fedha nyingi kwa muda mfupi na tangazo lao linakaa muda mfupi pia. Wewe njoo na mpango wa kuyasaidia makampuni haya kujenga wafuasi wengi kupitia mitandao hii ya kijamii.
Badala ya makampuni haya kulipa ada kubwa ya matangazo mara moja, kwa nini yasitengeneze wafuasi wake wenyewe ambao wataendelea kuwatangazia bure kila siku? Hiki ni kitu ambacho makampuni mengi hayaelewi na unahitaji kuwaelewesha na kuwapa mpango wako wewe.
Mpango wako unakuwa ni kuyasaidia makampuni kuendesha kurasa zao kwenye mitandao hii ya kijamii. Unayasaidia makampuni haya kupata wafuasi wengi, unatoa taarifa muhimu za makampuni hayo, unaendesha mashindano madogo madogo, vyote hivi vinaisaidia kampuni kupata wafuasi na kuwatangazia, huku wewe ukitengeneza kipato.

Kwa kifupi unahitaji kuwa na mpango huu;

1. Kuwa na mpango w akuweza kuisaidia kampuni kuongeza wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii. Unaweza kuanza na mitandao miwili yenye watumiaji wengi Tanzania, ambayo ni facebook na instagram.
2. Weka ada ndogo kwa kila siku ambayo kampuni unayofanya nayo kazi itakulipa. Hakikisha ni ada ndogo kiasi kwamba kampuni unayofanya nayo kazi haioni kama inapoteza fedha.
3. Toa mpango huu kwa makampuni mengi, kila kampuni unayoijua na ambayo huwa inatangaza kwenye mitandao hii wape mpango wako huo. Na hata kama kuna kampuni haijajua kutangaza kupitia mitandao hii ni wakati mzuri wa kuwajulisha hilo. Unapotoa mpango wako kwa makampuni mengi, kuna machache ambayo yatakubali.
4. Fanya kazi vizuri sana na makampuni haya na hii ndio itakuwa wasifu wako wakati unaendelea kuomba kufanya kazi hii na makampuni mengine. Kama utaweza kuonesha kwamba umeyasaidia makampuni mengine kukuza wafuasi na kutangaza kwa wengi kupitia mitandao hiyo, itakuwa rahisi kwa makampuni mengi kutaka kufanya kazi na wewe.
Unahitaji kutengeneza mpango bora ambao utatoa thamani kubwa kwa kampuni yoyote ambayo itakuamini wewe. Mambo hayo manne hapo juu ni muhimu kuyazingatia.
SOMA; USHAURI; Wakati Sahihi Na Wakati Mbaya Wa Kuchukua Mkopo Wa Biashara Benki.
Mambo yatakayokuzuia kufanyia kazi hiki ulichojifunza leo;
Kuna baadhi ya mambo ambayo yatakuzuia kufanyia kazi hiki nilichokushirikisha hapa leo. naomba niyaweke wazi hapa ili unaposhindwa ujue umeamua mwenyewe.
1. Hupo tayari kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kufikiri zaidi, kuwa mbunifu na kuongeza thamani kwenye biashara za wengine.
2. Unaogopa kutoa mapendekezo kwa kampuni usiyomjua mtu kwa sababu watakataa. Au utaongea na makampuni machache na yatakataa. Sasa kama unaogopa kwa sababu yatakataa, mpaka sasa ambapo hujatoa mapendekezo wamekataa, kwa nini usitumie mbinu nzuri kuwashawishi? Halafu ukiongea na makampuni kumi yakakataa ni kitu cha kawaida. Nitafute utakapokuwa umeongea na makampuni 100 na yote yakakataa, nitakupa mbinu za tofauti.
3. Uko tayari kushabikia timu nani na timu nani ila hupo tayari kutumia mitandao hii kwa faida yako na ya wengine. Sijui wewe kuwa kwenye timu ya mtu ambayo hata haiendi uwanjani unalipwa kiasi gani, unahitaji kuachana na huu ujinga na ufikirie kutengeneza kipato.
4. Uko tayari kuendelea kuona wivu kwenye maisha ya kuigiza kuliko kufikiria ni kipi ufanye ili kutengeneza fedha kwenye mitandao hii ya kijamii. Umekuwa unaona watu wanavaa vizuri kuliko wewe, wanaonekana kuwa kwenye ofisi nzuri kuliko wewe, wamepiga picha wakiwa wanacheka na kufurahi, wakiwa wanakula vyakula vizuri, wakiwa wapo kwenye sehemu nzuri za mapumziko. Na huenda kwa kuona wengine kwenye picha hizi unaona wewe ndio hujielewi. Sasa achana na mambo hayo ya kuonea wivu kwa sababu sehemu kubwa ya mambo unayoona kwenye mitandao ya kijamii ni maigizo. Au angalau watu hawakuoneshi wakiwa wanapitia matatizo yao binafsi, wakiwa wanakazana kupata fedha, wakiwa wanapambana na ugumu wa maisha. Wewe fikiria jinsi ya kuweza kuongeza thamani kwa wengine kupitia mitandao hii.
Fanyia kazi haya ambayo tumejifunza hapa, na kama utakwama popote wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Nakutakia kila la kheri kwenye safari yako ya kufikia mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: