Jana nilikushirikisha sababu kubwa ya matatizo kwenye mahusiano
yetu sisi na watu wengine. Na kama ukiweza kuondokana na chanzo kile basi
utapunguza sehemu kubwa sana ya matatizo kwenye mahusiano yako iwe ya kikazi,
kibiashara, kindugu au kimapenzi. Kama hukupata nafasi ya kusoma kile
tulichojadili jana basi kisome hapa; Matatizo Yote Ya Mahusiano Huanzia Hapa.
Leo nataka tugusie kitu kingine kikubwa sana kinacholeta
matatizo kwenye mahusiano yetu. Najua eneo la mahusiano ndio eneo gumu sana
kuelewana na watu kwa sababu moja kubwa, inapokuja swala la mahusiano watu
hawatumii akili kufikiri, bali wanatumia hisia kufikiri. Na pale hisia
zinapojiongoza zenyewe bila akili basi hapo ni majanga. Ndio maana ni vigumu
sana kuweza kumweleza mtu kuhusu mahusiano hasa ya mapenzi akakuelewa.
Sasa sababu nyingine kubwa ambayo inasababisha matatizo kwenye
mahusiano ni watu kuvaa visanamu mwanzoni mwa mahusiano. Watu wanapokutana ili
kujenga uhusiano, wengi wanadanganya, wanasema vitu ambavyo vitawafanya
wakubalike au kupendwa na wale wanaotaka kuwa na mahusiano nao. Hii ni kwenye
mahusiano yote, iwe ya kazi, biashara au hata mahusiano mengine ya
karibu.
SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako
Yote.
Mtu anadanganya kwenye usaili wa kazi ili aonekane ni bora na
kupewa kazi. Labda hudanganyi vitu vikubwa, ni vitu vidogo vidogo tu kama
kuahidi vitu ambavyo unajua kabisa huwezi kufanya kwa muda mrefu.
Au kwenye biashara unamdanganya mteja kwamba unaweza kufanya
kitu fulani ili akubali kufanya biashara na wewe.
Kwenye mapenzi sasa, ndio mtu atadanganya vitu vingi sana,
atabadili mpaka mfumo wa maisha, kuacha baadhi ya vitu na kadhalika.
Mambo yangekuwa rahisi sana kama kila mtu angeweza kuishi na
hiki alichoahidi anaweza kufanya. Lakini kama tulivyoona jana, watu
hawabadiliki, tena kwa haraka hivyo.
Kwa hiyo mtu atafanya kile alichosema kwa muda mfupi baada ya
hapo anachoka na hivyo kurudia maisha yake ya zamani. Hapa ndio utasikia siku
hizi fulani kabadilika. Hapana hajabadilika, amechoka kuvaa kile kisanamu na
sasa ameanza kuonesha ukweli wake.
Kuwa makini usivae kisanamu wakati unataka kujenga mahusiano
ambayo yatadumu. Kuwa mkweli, kama mtu hawezi kukukubali kwa ukweli wako hata
ukimdanganya huo uhusiano hautadumu. Nasisitiza tena hii sio kwa mapenzi tu,
bali kwenye mahusiano ya kazi, biashara na hata maisha ya kawaida. Kuwa mkweli
na utawavutia wale wa kweli. Vaa kisanamu na utavutia visanamu vingine.
TAMKO LA LEO;
Najua kwamba kudanganya mwanzoni mwa mahusiano ni kujenga kifo
cha mahusiano hayo. Hakuna uongo unaoweza kudumu kwa muda mrefu. Nitakuwa mkweli
siku zote ili niweze kujenga mahusiano bora na yatakayoniletea mafanikio. Hata
kama kuwa kwangu mkweli kutanikosesha baadhi ya mahusiano, najua kutanijengea
mahusiano ambayo ni bora.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita
Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi
yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Kuhakikisha hukosi mfululizo huu wa makala za KURASA 365
bonyeza hapa na uweke email.
Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo
maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya
facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya
email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na
KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata
utaratibu.
TUPO PAMOJA.