Katika dunia ya sasa ni kawaida sana kukutana na mtu akimthamini na kumjali mtu kwa kuwa ipo faida anaipata au ananufaika kwa njia moja au nyingine. Mfano huenda ni katika eneo lako la kazi, pengine bosi wako kwa kuwa tu wewe ni mfanyakazi mzuri basi ataonekana kukubali na kukuheshimu sana tu kumbe anafanya hayo kwa kuwa tu ipo faida anaipata kwa uwepo wake mahali pale pa kazi, pengine usipokuwepo naye nafasi yake itakuwa hatarini maana ni mapengo mengi unayaziba na kumfanya aonekane kuwa bora sana mahali pake pa kazi, unampa thamani mahali pale, hivyo naye anaonekana kukuthamini tu kwa kuwa ana anachopata kwako. Ile thamani uliyo nayo inamlazimisha kukujali na hata kukutumia zaidi.
Au kwa wanafunzi unapokuwa shuleni unakuta kuna mwenzio ana uwezo zaidi kwenye somo fulani hivyo unakuta mtu yule anategemewa na wengi na anaweza kuonekana kupendwa na wengi kwa kuwa anawasaidia wengi kuweza kufanya vizuri kwenye masomo anayowasaidia kuwafundisha ili waweze kuelewa zaidi, ukiangalia kwa kawaida unaweza ona kama yule mtu anapendwa na wengi, lakini ukiangalia zaidi utagundua pale hapendwi mtu bali kipo kitu cha thamani ambacho kinapendwa kwa mtu yule, kipo kitu watu wanakifuata kwa mtu yule ambacho pengine kwa wakati ule hakuna mahali pengine tena wataweza kupata kitu hicho, hivyo naweza sema wanakuwa hawana namna mbadala ya kupata huduma ile, wanalizimika kumkubali mtu yule hata kama hawampendi, wanalazimika kumsikiliza na wanakubali kufundishwa naye maana hakuna mwingine anaweza kufanya lile.
SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako Yote.
Pengine unaweza kukutana na mtu ukamshangaa na usimwelewe kwa kuwa anaambatana na mtu fulani, pengine wewe ukiangalia kwa macho yako ya kawaida unakuwa huioni thamani ya huyo mtu, huoni cha maana alichonacho cha kumfanya mtu mwingine asitake kuwa mbali naye, unajitahidi sana kukiona hicho lakini huoni, lakini wewe ukiwa katika hali hiyo kuna mwingine ameona thamani kwa huyo mtu, na anajua namna ya kuipata, hivyo anahakikisha anamtumia huyo mtu kuweza kupata kile mtu anacho, anamtumia yule mtu kuweza kufika pale anaelekea, usiishie kushangaa ni kwa nini mtu fulani anamkubali sana yule, usiwe mwepesi kumpuuza au kuona amepotoka wakati huelewi hasa ni kwa nini anafanya vile. Kama ukiwa mwelewa na mjanja mwenye nia ya kujifunza na kueleweshwa utatumia hekima na busara ili kuweza kuona kile mwenzio anaona kwa huyo mtu, utauliza na ukielekezwa uwe tayari kuheshimu hata mawazo ya wengine, uweze kuona thamani hata kwa wengine, hata kama wewe unadhani unajua kila kitu lakini tambua wapo wengine pia wanaoweza kuwa na uelewa kuliko wewe.
Wakati mwingine unaweza kukutana na mtu na ukamshangaa kwa nini anaambatana na mtu fulani maana wewe kwa viwango vyako na vipimo vyako unaona yule mtu si sahihi au hana sifa za kuweza kuwa na mtu yule na pengine unaweza kujaribu hata kumshawishi asiwe na mtu yule, pengine hata kwa kumweleza ni jinsi gani unaona hafai kwa kuelezea yale mabaya yake au madhaifu yake lakini cha ajabu unashangaa pamoja na hayo bado mtu yule anaendelea na msimamo wake wa kuambatana na mtu yule. Tambua yule ni mtu mwenye uelewa wa kutosha naamini ni yeye anaelewa ni kwa nini anaambatana na mtu yule, anajua ni kwa nini anashirikiana na mtu yule kwenye shughuli zake, yeye ndiye anajua ameona nini kwa mtu yule, pengine wewe huoni thamani kwa mtu yule, lakini yeye ameiona hiyo na hiyo ina nguvu kuliko sauti yako ya kumwaminisha kinyume, sauti yako anaona kama kelele tu, unatakiwa ujiulize unavyomwambia hayo wewe unaonekanaje kwa mtu huyo? Kwanini aamini unayosema? Una nini cha kukufanya aamini unachosema? Je una sababu za msingi za kuona yule mwingine hafai? Huyo ambaye hafai unamwelewaje? Unamfahamu sawasawa?
SOMA; Ushauri Kwa Waajiriwa Wapya Wote Wa Mwaka Wa Fedha 2014/2015
Tambua kuwa mtu yule yule unayemuona hafai , ipo sehemu anafaa sana kwa kuwa wale watu wameona kinachofaa au wameona thamani kwa mtu yule, huenda wamechagua kuiona thamani au mazingira yamewalazimisha kuona hivyo , maana hata kama hawamkubali au kumpenda lakini ndiye anayeweza jambo fulani ambalo wanalihitaji ili kuweza kufikia malengo yao katika maisha yao, hivyo wanalazimika kuwa na mtu yule, kumtumia mtu yule kama ngazi ya kufika kule. Kila mtu anaweza kumuona mtu yule yule kwa tofauti, inategemea kama una mtazamo gani juu ya wengine, kuwa na mtazamo chanya, tarajia kuona thamani hata kwa wengine, na ukiiona kama inakufaa itumie, usione aibu kusaidiwa hata na mtu unayeona hafai au hana hadhi ya kukusaidia au kukuelekeza jambo fulani, kumbuka Muumba wetu anaweza kumpa hata yule unayeona hafai thamani na ukalazimika kwenda kuhitaji huduma yake hata kama umemdharau sana, hata kama ulishaona hawezi kukuhudumia.
Katika maisha unavyoishi hebu jiulize una nini? Kwanini watu wakae chini wakusikilize? Unacho cha kuwasikilizisha? Kwanini niache wote nije kwako? Nitapata nini cha maana au cha tofauti?
Imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772