Habari ndugu msomaji wa Amka Mtanzania. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku. Karibu tena kwenye jukwaa hili la makala za kilimo. Wiki hii tutaangazia kilimo cha nyanya aina ya ANNA F1. Kwenye baadhi ya makala zilizopita tuliona kilimo cha nyanya kwa ujumla, lakini wiki hii tutakwenda kauangazia nyanya hii ya ANNA F1 kwa upekee. Nimekua nikipata maswali mengi kuhusiana na aina hii ya nyanya, nikaona basi ni vyema kuandaa makala maalumu kwa ajili ya aina hii ya nyanya. 

 
Kwanza tuanze kwa uchambuzi mfupi wa aina hii ya nyanya:
ANNA F1 ni aina ya nyanya ndefu huvunwa kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita. Aina hii ya nyanya inazalishwa na kampuni iitwayo Monsanto, nyanya hii ni kwa ajili ya uzalishaji wa kwenye greenhouse, japokuwa pia inafanya vizuri katika ulimaji wa eneo la wazi.
Sifa za nyanya ANNA F1
· Ni nyanya yenye umbo la kuvutia, yenye soko zuri, inafanya vizuri sana ikilimwa kwenye greenhouse, lakini pia inafanya vizuri ikilimwa kwenye eneo la wazi.
· Nyanya hii ina ukinzani kwa magonjwa kama Alternaria Stem Canker, Vertilicium, Fusarium wilt pamoja na Nematodes
· Inakomaa kwa siku 75 toka kuamishiwa shambani. Yaani ukishaitoa kwenye kitalu na kuipanda kwenye greenhouse, baada ya siku 75 unaanza uvunaji na uvunaji huo unaendelea kwa miezi 6 hadi 8
· Mavuno yanakadiriwa kufikia zaidi tani 50 kwa ekari, ikiwa na wastani wa kilo 35 kwa mche mmoja.
MAELEKEZO YA UPANDAJI
Kwa upatikanaji wa mazao mazuri ya nyanya ya ANNA F1, mlimaji anahitajika kua mwangalifu sana kwa kuzingatia maelekezo kwa kila hatua.
1. Uchaguzi wa eneo la kupanda.
Unapachagua eneo la kupanda nyanya hii hakikisha eneo hilo angalau liwe halijalimwa nyanya, pilipili hoho, viazi, ngogwe, biringanya au zao lolote linalotoka kwenye familia ya mimie ya Solanaceae kwa kipindi cha misimu mitatu.
Angalia upatikanaji na ubora wa maji ya umwagiliaji. Chukua sampuli ya maji hayo na ukayapime kwa ajili ya kujua ubora wake, na kufahamu maji hayo yana chumvi kiwango gani. Maji yakiwa na Sodium au Fluoride nyingi yataathiri ukuaji wa aina hii ya nyanya.
2. Udongo
Nyanya zinaweza kustawi katika aina kadhaa za udongo, ila udongo mzuri zaidi ni tifutifu, au mfinyanzi ambao hautuamishi maji. Udongo unapaswa uwe ambao haushikamani. Uchachu wa udongo (pH) unapaswa kua 6 -7.5. Pia ili uweze kua na mpango mzuri wa mbolea, mlimaji anapaswa kupima udongo kwenye maabara. Hii itakusaidia kujua ni virutubisho gani havipo na ni kiwango gani cha mbolea kinapaswa kuwekwa.
3. Mahitaji ya mbegu
Mbegu za ANNA F1 zinauzwa kwa idadi ya mbegu. Hivyo unanunua kulingana na ukubwa wa eneo lako pamoja na nafasi (spacing) utakayotumia kati ya mmea na mmea na mstari na mstari. Ila kiwango cha mimea kinachoshauriwa ni mimea mitatu kwa eneo la mita 1 ya mraba (1 m2 ). Mlimaji anapaswa kuongeza ziada ya mbegu kiasi cha asilimia 15 kwa ajili ya kufidia mbegu ambazo zinaweza kuharibika kwenye kitalu na zile ambazo zitakufa wakati wa upandikizaji.
SOMA; Mambo Muhimu Unayopaswa Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Greenhouse.
4. Kitalu cha mbegu
Kuna njia mbili ambazo unaweza kutumia kukuza miche yako kwenye kitalu.
a) Unaweza kutengeneza kitalu cha kawaida kinachotumia udongo. Kitalu kinapaswa kua cha matuta ya juu, tuta liwe limeinuka 15cm
b) Unaweza kutumia trays za kupandia miche ambapo unatumia udongo maalumu (coco peat)
· Kwa mbegu chotara kama Anna F1 zinapaswa kutunzwa umakini wa hali ya juu hasa kuanzia kitaluni.
· Mbegu zipandwe katika kina cha sentimita 1, na zipandwe katika mistari ambayo ina umbali wa sentimita 15 kutoka mstari na mstari.
· Hakikisha wakati wa kusia, mbegu zinapata nafasi maana mbegu hazitakiwi zirundikane kwa sababu zitasumbua wakati wa ukuaji, na huenda pia nyingine zikafa ikiwa zitakua zimesongamana sana.
· Ukisha sia mbegu unapaswa kufunika matuta kwa kutumia nyasi. Hii itasaidia kutunza unyevunyevu wa kwenye udongo na pia kuzuia mbegu zisitawanywe na maji kipindi cha umwagiliaji. Nyasi zinapaswa zitolewe mara mbegu zinapoanza kuchomoza kutoka ardhini.
· Umwagiliaji wa matuta ya mbegu unapaswa ufanywe kwa kutumia chombo maalumu cha umwagiliaji (water can). Umwagiliaji ufanyike wakati wa asubuhi.
· Mbegu zitaota ndani ya kipindi cha siku 8 na ukuaji wa miche utachukua mwezi mmoja kabla ya kupandikizwa
· Kwa utumiaji wa trays ni mzuri zaidi maana mbegu asilimia kubwa zinakua na uhakika wa kupona na kuwa na afya nzuri kuliko utumiaji wa matuta
5. Upandikizaji
Kama tulivyojifunza hapo juu, upandikizaji unafaa kwa miche yenye muda wa mwezi mmoja kwenye kitalu. Kwa maeneo yenye baridi, miche kwenye kitalu huchukua hadi mwezi na nusu (wiki 6) ili kufaa kupandikizwa.
Utoaji wa mimea kwenye kitalu unapaswa kufanywa kwa umakini sana ili kukinga mizizi ya mimea isijeruhiwe. Unaweza kung’oa miche kwa kutumia vifaa kama panga, chepeo/beleshi n.k Kifaa hicho unatumia kuchimba kwa chini kwa pembeni ili kubeba miche na udongo wake.
Wakati wa upandaji unapaswa uwe tayari umekwisha andaa mashimo ya kupandia hiyo miche. Mashimo hayo utaweka mbolea ya kupandia aina ya DAP, TSP au Minjingu.
Nafasi ya mimea inapaswa kua 60 kwa 45. Mstari kwa mstari umbali ni sentimita 60, na nafasi kati ya mche na mche inakua ni sentimita 45. Pia unaweza kutumia nafasi ya 60 kwa 60
6. Uwekaji wa Mbolea
Kwa mazao mazuri panatakiwa pawepo program maalumu ya lishe/virutubisho (nutriotional program) maana mahitaji ya mbolea yanatofautiana kulingana na hatua ya ukuaji wa mimea.
Mbolea ya kupandia inapaswa iwe yenye kirutubisho aina ya Phosphate (P) kwa sababu kinasaidia utengenezaji na ukuaji wa mizizi. Unaweza kutumia DAP au TSP au Minjingu kwa ajili ya kupandia. Hii inawekwa wakati wa upandikizaji wa miche. Mbolea ya kupandia inawekwa kwa kiwango cha kilo 60 kwa eka (60kg/acre)
Mbolea za kukuzia unapaswa kutumia mbolea yenye kirutubisho cha Nitrogen (N). Mbolea ya kukuzia unaweza kutumia UREA au CAN. Endapo utatumia Urea unapswa kuiweka wiki 2 hadi 3 baada ya kupandikiza. Ukitumia CAN unaiweka wiki ya 5 baada ya kupandikiza. Mbolea za kukuzuia zinawekwa kwa kiwango cha kilo 80 kwa eka (80kg/acre).
Maua yanapoanza unapaswa kutumia mbolea yenye kirutubisho cha Potassium (K) ambacho kinasaidia katika utoaji wa maua. Mbolea ambayo inatumika katika hatua hii ni NPK, na inawekwa kwa kiwango cha kilo 80 kwa ekari (80 kg/acre). Mbolea hii inapaswa kuwekwa tena baada ya mvuno wa kwanza.
7. Umwagiliaji
Kiwango na marudio (irrigation frequency) ya umwagiliaji kinategemea na hali ya hewa ya mahali husika. Wakati wa jua mahitaji ya maji ni makubwa kulinganisha na wakati hakuna jua. Pia kiwango cha maji kinategemea hatua ya ukuaji wa mimea. Mimea inapokua midogo mahitaji ya maji vilevile ni madogo, mimea ikishaanza kutoa maua na kutengeneza matunda mahitaji ya maji yanakua makubwa. Epuka kumwagilia wakati wa jioni ili kuepuka uwezekano wa kushambuliwa na magonjwa.
SOMA; Teknolojia Katika Kilimo: Kilimo Cha Greenhouse Na Aina Zake.
8. SUPPORT STRUCTURE
Hizi ni nguzo zinawekwa kwa ajili ya kusaidia mimea ya nyanya isitambae chini badala yake iweze kukua kuelekea juu. Kama tulivyoona kwamba aina hii ya nyaya (ANNA F1) ni ndefu hivyo kuwekewa support ni jambo la lazima. Zipo aina kadhaa za Support ambazo zimekua zikitumika katika kilimo cha nyanya hii ya ANNA F1, Ila kwa hapa tutaangalia aina moja ya support structure ambayo inatumia nguzo, nyaya (wires) pamoja na kamba.
Nguzo zinapaswa kua imara maana ndizo zinazobeba mzigo, maana wakati nyanya ikiwa na matunda mzigo unakua ni mkubwa, hivyo nguzo zinapaswa ziwe zinazoweza kuhimili mzigo huo. Nyaya (Wires) zinafungwa kwenye nguzo hadi nguzo kwa juu, kisha mimea inapewa support ya kamba ambayo inafungwa kwenye waya.
Kuitengenezea mimea support kunawezesha kuwepo na mzunguko wa hewa, hii hupunguza unyevunyevu na hivyo kupunguza uwezekanao wa kushambuliwa na magonjwa ya fangasi.
9. Kupogoa/ Upunguzaji wa Matawi (Pruning)
Pruning inafanyika kwa matawi, majani na maua.
Matawi ya pembeni yanaondolewa na kuacha tawi moja au mawili ikitegmea na unatumia mfumo gani, aidha wa kuacha tawi moja au matawi mawili. Fanya ukaguzi kila wiki kwa ajili ya kuondoa matawi ya pembeni yanayochipua.
Majani ya zamani ambayo yamezeeka yanapaswa kuondolea. Pia majani yaliyoshambuliwa na magonjwa yanapaswa kutolewa kwa uangalifu ili ugonjwa usiendelee kusambaa.
Maua yanapaswa kupunguzwa kwenye kila cluster ya maua ili kufikia idadi ya 5 hadi 6 ambayo yatapelekea kua na matunda ya wastani.
10. Uvunaji
Anna F1 inakua tayari kwa kuvuna baada ya siku 70 hadi 75 ikitegemeana na hali ya hewa. Kwa maeneo ya baridi nyanya hua zinachelewa kukomaa.
Vuna nyanya zako kila baada ya muda fulani kadri zinavyoiva kutegemea na mahitaji ya soko lako. Kwa kawaida mvuno wa kwanza ni mdogo kulinganisha na mivuno itakayofuata.
Vuna nyanya kwa kutumia mikono na kisha weka kwenye kreti kwa uangalifu ili kuepuka kujeruhika kwa nyanya.
Uvunaji unaendelea kwa miezi 6 hadi 8
Umwagiliaji unapaswa ufanyike mara tu baada ya uvunaji. Kila unapovuna hakikisha mimea inapata maji ya kutosha.
11. Upandaji wa ANNA F1 kwenye Grenhouse
Kama tulivyoona awali kwamba nyanya hii inafanya vizuri sana inapopandwa kwenye Greenhouse, katika greenhouse kuna aina mbili za upandaji.
a). Single stem system : Katika mfumo huu nyanya inabaki na shina moja tu, matawi mengine yote yanatolewa . Mfumo huu unatumia nafasi ya 60 X 45 cm. Unaweza kutazama picha hapa chini
b). Double stem system: Katika mfumo huu matawi mawili yale yenye nguvu ndiyo yanayoachwa mengine yote yanaondolewa. Mfumo huu unatumia nafasi ya 60 X 60 cm. Unaweza kutazama picha hapa chini
Greenhouse na bei zake
Hizi ni aina za Greenhouse na bei zake. Bei zinatofautiana kutokana na ukubwa wa greenhouse. Pia unapatiwa na vifaa vya umwagiliaji (mipira na tenki la maji). Unapata dawa za kuanzia kwa ajili kudhibiti wadudu na magonjwa, mbolea za kuhudumia mimea, unapata msaada wa kitaalamu na pia unafungiwa Greenhouse yako.

Greenhouse package PRICE Tsh(VAT+)
6m x 12m: Enterprise Kit ,Open Roof; Chemicals package; Fertilizer package; Agronomic support & Installation 4,200,000
6m x 12m: Enterprise Kit, open Roof; Irigation , Installation. 3,300,000
8m x 15m: Open roof model; drip irrigation; Chemicals package; Fertilizer package; Agronomic Support & Installation 8,300,000
8m x 24m: Open roof Model; Inbuilt Metal door; drip irrigation; chemicals package; Fertilizer package; Agronomic Support & Installation 11,400,000
9m x 15m: Tropical Model Kit , Open Roof; drip irrigation; chemicals; package; Fertilizer package; Agronomic Support & Installation 10,980,000

Asante sana. Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Kwa ushauri au maswali, Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com