Katika matatizo mengi ambayo wafanyabiashara na wajasiriamali wanakutana nayo kila siku kwenye maisha yao ya kibiashara, mengi yanaanzia kwenye mtazamo wao juu ya biashara wanayofanya. Hiki kinakuwa kikwazo kikubwa sana kwao kuendesha biashara yenye mafanikio. Kwa kuwa mtazamo ni kitu kinachoanzia ndani ya mtu kabisa, hata pale mtu anapopata elimu ya biashara au ujasiriamali mtazamo wake unabaki vile vile. Na hivyo anaweza kuwa na mbinu nzuri sana za kibiashara ila bado biashara yake isifanye vizuri kwa sababu mtazamo wake haupo sahihi.

Leo kupitia KONA HII YA MJASIRIAMALI tutajadili kuhusiana na mtazamo wako wewe mjasiriamali kuhusu biashara unayofanya. Kwanza nikukumbushe kwamba ufanyaji wa biashara kwenye kipindi hiki tunachoishi umebadilika sana tofauti na ilivyokuwa nyuma. Hivyo kama BADO unaendesha biashara zako kwa mifumo ile ya kizamani unajipoteza wewe mwenyewe.
Biashara sio pata potea.
Zamani ilikuwa inachukuliwa kwamba ili ufanikiwe kwenye biashara ni lazima uwalangue watu au uwadhulumu wengine. Hivyo watu walikuwa wanauza bidhaa au huduma zao kwa bei ya juu sana ukilinganisha na gharama walizoingia. Na wakati mwingine watu waliuza vitu ambavyo havina ubora ili mradi tu wao wapate faida. Na hata kwenye upande wa wafanyakazi, watu waliajiri wafanyakazi ambao watawalipa kiasi kidogo sana cha mshahara na wawafanyie kazi. Hii ilileta picha mbaya sana kwa wafanyabiashara na wakawa wanaonekana ni walanguzi au watu wanaowaumiza wengine.
Zamani ilikuwa ukiuziwa kitu ndio umekuwa mzigo wako, na hata risiti iliandikwa kabisa kwamba MALI IKISHAUZWA HAIRUDISHWI. Hii ilionesha wazi kwamba kama utanunua kitu na kikashindwa kufanya kazi uliyotegemea kifanye basi wewe ndio umekosea na sio mwenye biashara.
Mambo yamebadilika.
Sasa hivi mambo yamebadilika sana. Ile hali kwamba wafanyabiashara wanaweza kuuza bidhaa kwa bei wanayotaka wao ili tu wapate faida kubwa haipo tena. Ile hali ya kuajiri wafanyakazi wasio na uwezo ili kuwalipa kidogo nayo inapotea kwa kasi. Na hata ile hali kwamba mali ikishauzwa hairudishwi nayo inapotea kwa kasi sana. Sasa hivi biashara zinatangaza kabisa wanakupa dhamana hata ya zaidi ya mwaka mmoja. Kwamba ukinunua bidhaa na isipofanya kazi basi utapewa nyingine au kufanyiwa matengenezo.
Biashara za sasa wateja sio tena watu wa kuendeshwa, bali ni watu wanaojua ni nini wanataka na wana uhuru mkubwa kwa sababu usipowapatia wewe watapata wanachotaka kwa mfanyabiashara mwingine. Uhuru huu mkubwa kwa wateja sio pigo kwetu wafanyabiashara, bali ndio nafasi nzuri kwetu kuweza kuwahudumia vizuri.
Ufanye nini ili kuendesha biashara yako vizuri?
Kama tulivyoona mabadiliko haya kwenye biashara na kama tulivyoona nguvu kubwa ambayo wateja wanayo kwa sasa, kama utaendelea kufanya biashara kwa mazoea ni dhahiri kwamba tayari umeshashindwa. Utashangaa kuona wateja wanakukimbia na wanaenda kwa mfanyabiashara mwingine anayeweza kuwahudumia vizuri zaidi. Yafuatayo ni mambo muhimu kwa kila mfanyabiashara kuzingatia ili biashara yake iweze kwenda vizuri.
1. Jenga biashara yako kwenye misingi ya uaminifu.
Uaminifu ni muhimu sana kwenye biashara yako. Mteja wako ni lazima akuamini wewe na ni lazima aamini kwamba bidhaa au huduma anayonunua kutoka kwako itamsaidia shida wake na hata kama kutakuwa na tatizo basi wewe uko upande wake. Ni rahisi sana kujenga uaminifu kwa wateja wako kama utawajali na kuweka misingi ya kutoa kilicho bora kwa wateja wako.
Unahitaji pia kuwa mwaminifu kwa wafanyakazi unaoajiri kwenye biashara yako. Hawa ndio wateja wa kwanza kabisa na ni lazima wakuamini wewe na waiamini biashara yako ili waweze kuwahudumia vizuri wateja wako. Kushindwa kufanya hivyo utaiona biashara yako ikiporomoka huku wewe ukifanya kila jitihada ya kuikomboa bila ya mafanikio.
Jambo jingine muhimu kufanya ni kutoa huduma nzuri sana kwa wateja wako.
Kujenga uaminifu peke yake haitoshi, ni lazima wateja wako wapate huduma bora kwenye biashara yako. Hiki ndio kitakachowafanya waendelee kuja kwenye biashara yako, vinginevyo wataenda kwenye biashara nyingine ambapo wanaweza kupewa huduma nzuri zaidi. Ukishajenga misingi ya uaminifu, huduma nzuri sio kazi kubwa kujenga. Ni muhimu sana wateja wako kupata huduma ambayo hawajawahi kuipata kokote.
Ni wakati sasa wa wewe kufanya mapinduzi makubwa kwenye biashara yako kwa kufanya mabadiliko kwenye mtazamo wako. Usiendeshe biashara kwa misingi ya wewe kupata ni wengine kukosa. Endesha biashara kwenye misingi ya uaminifu na kutoa huduma bora kwa wateja wako. Itakuletea wateja wengi na utaweza kufikia mafanikio makubwa kupitia biashara yako.
TUPO PAMOJA.