Kama unataka kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, ni lazima ujue kitu ambacho wengine hawakijui. Hii ni siri ambayo watu wanaijua kwa muda mrefu sana, ila sasa wakawa wanaitumia vibaya.

JUA ZAIDI NA UTAKUWA BORA ZAIDI.
JUA ZAIDI NA UTAKUWA BORA ZAIDI.

Kwa kujua kwamba wanahitaji kujua kitu cha tofauti na wengine, watu walikuwa wanatengeneza siri kubwa sana. Kwenye kazi, biashara na hata maisha, watu walikuwa na siri nzito sana ambazo hawakujaribu kuzisema kwa mtu yeyote.

Hii iliweza kuwasaidia baadhi ya watu kwa kipindi kifupi, ila kwa sasa haiwezi tena kukusaidia. Hii ni kwa sababu kila kitu kipo wazi, huwezi kuweka siri yoyote kubwa. Hata ukijaribu utafanikiwa kwa muda mfupi tu, baadae kila kitu kitajulikana na wengine.

Ufanye nini sasa?

Kwa kuwa unahitaji kujua kitu ambacho wengine hawajui ili ufanikiwe, basi lengo lako la kwanza liwe kujua zaidi na zaidi. Ukijua kitu fulani leo usiridhike na kuona maisha ndio umeshayaweza, endelea kujua vitu vingine vingi zaidi. Utakapofanyia kazi kitu kimoja na wengine wakakiona, wewe tayari una vingine vingi.

Usiwe mchoyo kwa kujua kidogo na kukifanya siri kubwa, jua vingi na wasaidie wengine pia. Utazidi kuwa mbali zaidi na zaidi. Kwa sababu wale wanaochukua kwako watazidi kuja kwako kwa sababu wewe ni kama chemchem.

Kwa mfano kama unataka kutafuta kitu ambacho hujui kinapatikana wapi kwenye mtandao unakwenda wapi? Moja kwa moja utakwenda google na kutafuta kile unachotaka, kwa sababu google inajua kuliko wewe. Lakini je google ikishakuonesha ulichokuwa unatafuta ndio unaacha kuitumia? Hapana, kwanza ndio unazidi kuitumia zaidi na zaidi.

Kuwa google kwenye maisha yako, kuwa chanzo cha watu kujifunza zaidi na zaidi. Hakuna fursa chache useme kwamba unahitaji kuwa na siri kubwa sana. Wewe jua vitu na endelea kujua vingi zaidi na zaidi.

Utajuaje vingi, jifunze kila siku. Japo njia nyingi za kujifunza zipo wazi, sio wote watakaoweza kufanya hivyo, hivyo utaendelea kuwa juu na hata wengine wakijifunza kama wewe, bado fursa zipo nyingi sana.

Usiwe na siri zinazokaribia kukuua, kuwa chanzo ambacho watu watakutumia wewe kama rufaa kwa sababu wanajua wakija kwako wanapata zaidi na zaidi na hii itakufanya ufikie mafanikio makubwa zaidi.

Je ni kitu gani utafanya kwenye kazi, biashara na maisha yako leo ili kuweka mtazamo wako sawa kwenye hili? Tushirikishe kwenye maoni hapo chini.

TAMKO LA LEO;

Najua ya kwamba ili nifanikiwe nahitaji kujua kitu ambacho wengine hawakijui. Ila sitakiwi kuwa mchoyo kwenye hili, sitakiwi kuwa na siri nzito, natakiwa kujifunza kila siku na kujua vitu vingi ili watu waje kwangu kwa vingi zaidi na zaidi na hii itanifikisha kwenye mafanikio makubwa sana.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.