Wahenga walisema, chunga ulimi wako, kwa sababu ulimi ni kiungo kidogo ila kinaweza kukuingiza kwenye matatizo makubwa. Walikuwa sahihi sana. Ila nafikiri kama wahenga hawa wangekuwa wanaishi kipindi hiki, wangeongeza kitu kingine muhimu sana ambacho ni vidole. Kipindi wanaishi wahenga vidole havikuwa shida sana, ila sasa hivi vidole vyako vinaweza kukuingiza kwenye matatizo makubwa.

KUWA MAKINI NA VIDOLE VYAKO, VINAWEZA KUKUINGIZA KWENYE MATATIZO MAKUBWA.
KUWA MAKINI NA VIDOLE VYAKO, VINAWEZA KUKUINGIZA KWENYE MATATIZO MAKUBWA.

Kwa sasa tunahitaji wahenga wengine wa kutuonya kuhusu vidole. Kwa kuwa hawapo, naomba mimi niwe mhenga wako kwa dakika chache tu, baada ya hapo mambo mengine yatakwenda vizuri.

Karibu kwa mhenga Kocha Makirita.

Kadiri teknolojia inavyokua, njia za mawasiliano zimerahisishwa sana. Sasa hivi vidole vyetu vimekuwa njia kuu ya mawasiliano. Unatumia vidole vyako kuandika ujumbe wa simu au hata wa kwenye mitandao mbalimbali, halafu unabonyeza tuma, au send, au post na mengine kama hayo.

Kama ulichoandika hukuwa makini nacho kinaweza kukuingiza kwenye matatizo, kama ilivyo kwa mtu aliyeongea hovyo. Wakati mwingine mtu anaweza kukukasirisha tu kwenye hii mitandao, kwa hasira zako na wewe ukamjibu vibaya, na majibu yako yakaleta matatizo makubwa zaidi.

Halafu kuna tofauti kubwa sana ya kujibu ujumbe na kuongea ana kwa ana. Unapokuwa ana kwa ana na mtu unaweza kuona aibu kuzungumza baadhi ya maneno, ila kwa kutuma ujumbe, unaweza kuandika kitu ambacho usingethubutu kukitamka mbele yake.

Nimekuwa naona watu wakiumbuliwa na jumbe zao mbalimbali walizotoa siku za nyuma na sasa wakabadilika. Labda mtu aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii, siwezi kufanya kitu fulani kamwe, watu wanatunza ule ujumbe, siku akifanya wanamwonesha na kuanza kumbeza kwamba hana msimamo.

Halafu kibaya zaidi rafiki yangu ni kwamba kuna sheria imekuja na ni kali sana. Unaweza kuona unaandika kitu kwa mzaha au kwa utani tu lakini ukaishia kwneye mikono ya sheria. Kama mtu aliyewapongeza majambazi kwenye mtandao wa kijamii alivyoishia mikononi mwa polisi.

Hivyo mimi kama mhenga wa muda, nakusihi sana chunga vidole vyako. Usiandike kitu chochote ukiwa na hasira. Usijibu kitu chochote ukiwa na hasira. Kama una wasiwasi jiulize je hichi nachotaka kuandika nitajisikia vizuri kama kitachapwa kwenye ukurasa wa mbele kabisa wa gazeti na kila mtu akakisoma kwamba mimi ndio nimeandika? Kama jibu ni ndio endelea, kama jibu ni sio acha mara moja. Tatizo unapokuwa na hasira huwezi kufikiri hayo yote, hivyo nimalizie kwa kusema kwamba ukiwa na hasira kaa mbali na simu yako.

TAMKO LA LEO;

Nitakuwa makini na vidole vyangu kama nilivyo makini na ulimi wangu. Najua vidole vinaweza kuniweka kwenye matatizo makubwa na hata kunizuia mimi kufikia mafanikio makubwa. Nitaandika kitu ambacho nitakuwa na ufahari nacho hata kama kitawekwa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti. Nitakaa mbali na simu yangu pale ninapokuwa na hasira.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.