Kwa kawaida huwa tunachukulia uvivu kwa vile vitu ambavyo ni rahisi kuonekana.

Mtu ambaye hamalizi majukumu yake kwa wakati ni mvivu. Mtu ambaye haonekani kwenye kazi yake kwa muda wa kazi huyo ni mvivu. Na pia mtu ambaye anakwepa majukumu yake ya kazi huyo ni mvivu.

Kwa uelewa huu wa uvivu umetufanya tuamini kama tunaonekana kwenye kazi zetu na kuzimaliza basi sisi sio wavivu. Kitu ambacho sio kweli.

KAMA KUNGEKUWA NA MASHINDANO YA UVIVU UNAFIKIRI HUYU ANGESHIKA NAFASI YA NGAPI?
KAMA KUNGEKUWA NA MASHINDANO YA UVIVU UNAFIKIRI HUYU ANGESHIKA NAFASI YA NGAPI?

Kuna aina nyingine nyingi za uvivu ambazo huenda unazitumia kila siku na zinaendelea kukurudisha nyuma.

Kupanga wewe mwenyewe kwenye nafsi yako kwamba utafanya kitu halafu usifanye ni uvivu. Kwa sababu kwa akili zako timamu ulikubali kwamba kuna kitu utafanya au kubadili kwenye maisha yako, sasa mbona hufanyi kitu hiko? Ulisema utawahi kuamka, mbona hufanyi hivyo? Ulisema utaanza kuweka akiba, mbona hufanyi hivyo? Ulisema utaacha kupoteza muda mbona hufanyi hivyo? Uvivu.

Kusubiri watu wafikirie kwa niaba yako kwamba uishi vipi nao ni uvivu mkubwa sana. Kama huna mipango na maisha yako na unafanya kile ambacho kila mtu anafanya, samahani sana, lakini wewe ni mvivu. Ndio hakuna kundi jingine tunaloweza kukuweka. Kwa nini usikae chini na kuamua ni maisha gani unayotaka kuishi wewe, kwa nini utake tu kwenda kama hujui unakoelekea? Acha uvivu.

Kuogopa kufanya jambo kwa sababu huna uhakika au ni jambo jipya nao ni uvivu. Ndio, uvivu unakufanya uone ni kitu ambacho hakiwezekani kufanyika. Kama ukiondokana na uvivu na kuweza kufanya huenda ukaleta mabadiliko makubwa sana.

Kuahirisha mambo nao ni uvivu tena mkubwa sana. Yaani kwa nini upange mwenyewe kwamba muda fulani utafanya kitu fulani, halafu wewe mwenyewe useme hutafanya tena, tena bila sababu ya msingi? Uvivu.

Kutafuta njia ya mkato, hasa kwenye kufikia mafanikio, nao ni uvivu mkubwa sana. Na mara zote unaposhawishika kupita tu njia ya mkato ili upate mafanikio, ni lazima upotee.

Kuanzia sasa acha uvivu, huwezi kufikia mafanikio makubwa kama utaendelea na hizi aina nyingine nyingi za uvivu. Ndio fanya kazi vizuri na mipango yako nenda nayo vizuri basi.

TAMKO LA LEO;

Nimegundua kwamba kuna aina nyingi sana za uvivu ambazo nimekuwa nazitumia kila siku. Kwa kuwa nimeshaamua kuishi maisha ya mafanikio, sina budi kuachana na hizi aina zote za uvivu. Nitafanya kile ninachopanga kufanya, sitasubiri watu waniambie ni nini cha kufanya, nitaacha kuahirisha mambo na kama ninavyojua, hakuna njia ya mkato ya kufikia mafanikio. Najua nikiweza kuondokana na hizi zina za uvivu hakuna kitakachoweza kunizuia kufikia mafanikio.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.