Kama kuna kitu muhimu kwa kila mfanyabiashara, basi ni muda. Kuna wakati unatamani siku ingekuwa na masaa mawili au matatu ya ziada ili uweze kukamilisha majukumu yako ya kibiashara. Katika wakati huu unakuta umeacha kuimiliki biashara na biashara inaanza kukumiliki wewe. Hii ni hali ya hatari sana kwenye maisha yako ya kibiashara, kwani biashara inapokumiliki huwezi tena kuifurahia na hata juhudi zako za kuikuza zinakuwa ndogo.

Leo tutajadili jinsi unavyoweza kurudisha umiliki wako wa biashara ili uweze kuendesha biashara yenye faida na itakayokufikisha kwenye malengo yako.

Ni wakati gani ambapo unaimiliki biashara? Huu ni ule wakati ambapo wewe unaweka mipango yako ya kibiashara na unaweza kuifikia. Unajua biashara yako inaelekea wapi na unaweza kufanya mabadiliko kwenye biashara yako. Kwa mfano kama biashara haifanyi vizuri unaweza kujua ni eneo gani linasua sua na kulifanyia kazi. Kuendesha biashara ambayo unaimiliki ni rahisi na unaweza kuona mafanikio kupitia biashara unaofanya.

Ni wakati gani ambapo biashara inakumiliki wewe? Huu ni ule wakati ambapo unajikuta unafanya vitu vingi kuliko muda ulionao. Unajikuta unashughulika sana lakini biashara haioneshi mabadiliko yoyote. Katika wakati huu unaona biashara haikui au inapata hasara, lakini huwezi kujua chanzo ni nini. Katika aina hii ya biashara unajikuta ukiendeshwa zaidi na matukio ya kila siku badala ya kuendeshwa na ratiba zako mwenyewe au mipango yako ya kibiashara uliyojiwekea.

Wewe kama mjasiriamali na mfanyabiashara makini, unahitaji kuimiliki biashara na sio kuiacha biashara ikumiliki wewe. Unawezaje kudai ukombozi wako kutoka kwenye biashara yako? Hapa kuna baadhi ya njia nzuri unazoweza kutumia.

Kwanza ijue vizuri biashara yako.

Hatua ya kwanza ya kuweza kuimiliki ni kuijua vizuri biashara yako. Jua ni aina ya biashara gani unayofanya, jua wateja wako ni watu wa aina gani, jua ni tatizo gani la wateja biashara yako inatatua. Kwa kujua maeneo haya muhimu ya biashara yako, unaweza kuweka nguvu zako nyingi kwenye maeneo hayo na kuacha mambo mengine ambayo sio ya msingi.

Unaweza kuona ni rahisi lakini ukweli ni kwamba kama hujui biashara yako vizuri na kujua yale maeneo muhimu, utajikuta unafanya mambo mengi, unachoka sana lakini faida ni kidogo. Yajue yale maeneo yanayomsaidia mteja na yenye faida kubwa, kisha kazana kufanyia kazi maeneo hayo tu.

Hatua ya pili kuwa na malengo na mipango.

Kama huna malengo ya kibiashara utakuwa unaelekea wapi na biashara yako? Kama huna mipango ni kitu kipi kitakuwa na kipaumbele na kipi utaachana nacho? Kama huna malengo ya kibiashara maana yake hujui biashara yako inaelekea wapi, na kama hujui biashara yako inakoelekea itakufikisha popote na kwa kuwa hata huko popote hupajui utaona ni sawa tu. Wewe utaona unafanya kazi sana lakini faida hakuna, hii ni kwa sababu hutakuwa na kipaumbele chochote kwenye biashara yako.

Unahitaji kuwa na mipango ya kila siku ambayo unaifanyia kazi. Dunia tunayoishi sasa ina kelele nyingi sana, kuna mambo mengi ambayo ungependelea kufanya, lakini hayana umuhimu mkubwa kwenye biashara yako na hata maisha yako ya kawaida. Ni vyema ukawa na mpango wa kila siku ili kuwa na kipaumbele kwenye matumizi ya muda wako wa kila siku na uweze kuona mabadiliko ambayo umeleta kwenye biashara yako.

Hatua ya tatu, tengeneza timu.

Huwezi kufanya kila kitu mwenyewe, na hata ungeweza huna nguvu hizo na muda huo wa kuweza kuhakikisha kila kitu kipo vizuri kwenye biashara yako. Hivyo basi ni muhimu kutengeneza timu ambayo itaisaidia biashara yako kukua. Kuwa makini sijasema uwe na wafanyakazi, nimesema uwe na timu. Unapokuwa na timu, kila mtu ana eneo lake muhimu ambalo mkiyakusanya kwa pamoja, yanaleta mabadiliko makubwa kwenye biashara yako. Unapoajiri watu wa kukusaidia kwenye biashara, hakikisha unawajengea utamaduni wakufanya kazi kama timu. Hii itaisaidia sana biashara yako kukua zaidi.

Kama mpaka sasa huifurahii biashara yako, na kila juhudi unazoweka hupati faida kuna uwezekano mkubwa biashara imekumiliki wewe. Unachohitaji kufanya sasa ni kudai uhuru wako ili uweze kuimiliki biashara yako. Unahitaji kuwa na malengo na mipango, kuijua biashara yako vizuri na kuwa na timu nzuri ya ushindi.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz