Habari Mpenzi Msomaji, na karibu katika makala yetu ya leo. Leo tutazungumzia juu ya malezi ya watoto, watoto wanahitaji mwongozo mzuri angali au tokea wanapokuwa wadogo ndio maana wahenga walisema samaki mkunje angali mbichi na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Usemi huu unatufundisha kuwa watoto wanatakiwa waonyeshwe malezi na njia nzuri angali bado wabichi. Katika familia zetu au jamii zetu kuna changamoto kubwa sana katika malezi ya watoto. Wazazi au walezi ndio wanatakiwa kuwajibika kwanza juu ya malezi ya watoto wao. Watoto wa siku hizi wanakosa malezi bora kutoka kwa wazazi yaani baba na mama na kuwaachia malezi au majukumu ya watoto wasaidizi wao wa kazi za nyumbani.

KULEA WATOTO WENYE FURAHA NI JUKUMU LAKO MZAZI.

 
Watoto wanakosa malezi bora pamoja na upendo kutoka kwa wazazi wao. Wengi wanasingizia kazi zinawabana je baada ya kazi huwa unatenga muda wa kuzungumza na mtoto wako? Muda wa kukaa baa unao, kubishana kuhusu siasa ,michezo nakadhalika, tumia muda huo ambao hutengenezi faida chanya katika maisha yako kukaa na watoto au mtoto wako umuonyeshe upendo halisi kutoka kwa wazazi na siyo wasaidizi wa kazi za nyumbani, mpe dira aweze kuifuata na njia bora za kuishi hapa duniani.
Ndugu mpenzi msomaji, jukumu la malezi kwa watoto ni baba na mama usijisahau hata kama una mtu wa kukusaidia kulea mtoto au watoto wako. Wazazi yawapasa kuwalea watoto wenu vema katika njia ambayo hawataiacha hata akiwa mzee hatoisahau kamwe katika maisha yake. Watoto wanahitaji kusikilizwa na muda mwingine wanakosa hata mtu wa kuwaelezea matatizo yao ya ndani. Watoto wanapata majeraha na mipasuko katika mioyo yao wakiwaona wazazi wao jinsi wanavyoishi bila ya upendo na amani ndani ya nyumba hii inamsababishia mtoto matatizo ya kisaikolojia na kuathirika kabisa kiakili na kudhoofika kimwili pia.
SOMA; Punguza Nafasi Za Watu Kukuumiza Kwa Kufanya Hivi.
Wazazi ndio adui namba moja wa kumharibu mtoto au watoto, kwa nini nasema hivyo? Hii ni kwa sababu mzazi anakila sababu ya kuwajibika katika malezi ya mtoto au watoto. Wapo wazazi ambao wanadiriki kusema kuwa huyu mtoto amenishinda, mbele ya huyo mtoto unafikiri hapo unamtengenezea mtoto mazingira gani na wewe pia unajitengenezea mazingira gani?
Mambo muhimu ya kuzingatia katika malezi;
1) Mpe malezi bora
Mlee katika njia impasayo naye hatoiacha mpaka atakapokuwa mzee. Mlee kwa upendo naye atakulipa kwa upendo, hakika mtoto wako ukimlea vizuri anafuata maadili mazuri na maadili mazuri anayapata kutoka kwa mzazi, waweke watoto wako katika hali ya usafi hata mgeni akitokea atavutiwa na mtoto wako na hata kumpakata kuliko kumuacha mtoto mchafu muda wote hana uangalizi anacheza katika mazingira hatarishi. Wazazi siyo vema kuwatukana watoto chunga sana ulimi wako, unapomtukana mtoto anaiga matusi na tabia mbaya kutoka kwako mzazi, ataona ni kitu cha kawaida hata mama au baba anafanya. Kwa mfano wazazi wengine wanawatukana watoto wao kama vile, ashakumu si matusi (naomba uniwie radhi kwa maneno haya) mbwa wee, mshenzi wee na matusi mengine ambayo matusi hayo yanawaharibu watoto kiakili kabisa hatimaye watoto wanaathirika kisaikolojia.
2) Mfundishe mtoto jinsi ya kuvua samaki na siyo kumpa samaki
Anza kumjengea tabia nzuri mtoto angali akiwa mdogo mpe njia za kufanikiwa, wewe kama mzazi umepitia mengi hivyo basi kupitia makosa yako umejifunza mengi sana kwa hiyo mfundishe mtoto apite njia nzuri ili asije kurudia makosa kama yako ,mfundishe mabadiliko ya yanayoendelea duniani ili ajiandae na mabadiliko hayo. Usimlee tena katika mfumo wetu wa elimu ambapo unaandaliwa kuwa mwajiriwa, mlee katika mawazo ya kujitegemea, kujiajiri, jinsi ya kuona fursa katika jamii na kuzitendea kazi, jinsi ya kutengeneza ajira na siyo kuajiriwa tu kwani kazi za maofisini siku hizi zimekuwa changamoto hivyo basi ni vema kumwandaa mwanao katika mabadiliko haya ambayo yapo na yataendelea kuwepo.
3) Usimnyime mtoto adhabu anapokosea
Mtoto ana haki ya kuadhibiwa pale pale tu anapofanya makosa ambayo anastahili kuadhibiwa. Sasa kuna wazazi wengine wanalea mtoto kama yai mtoto anageuka mfalme ndani ya nyumba au mtawala, mzazi hana kauli mtoto anafanya chochote anachojisikia ndani ya nyumba kama vile kuvunja vitu na kuharibu bila hata kumpa adhabu ili akome tabia hiyo. Mtoto anatukatana watu, na wakati wengine wazazi nao huwa wanatukanwa na watoto wao yote haya ni kwa sababu ya kukosa malezi bora, unamnyima adhabu ndio matokeo yake tabia inakuwa na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo na samaki mkunje angali mbichi.
Kwa hiyo, mtoto kuwa na kutokuwa na heshima chanzo ni mzazi umeridhika na hali hiyo ambayo mtoto wako anayo bila kuchukua hatua.
SOMA; Mambo Matano (5) Yanayoweza Kuhamasisha Watu Wote Wanaokuzunguka Kufikiria Kibunifu.
4) Mfundishe mtoto kukosa
Maisha ya binadamu ni mafupi kwa hiyo huwezi kukaa na mwanao siku zote inakupasa kumfundisha mtoto kukosa pia wakati mwingine ni vizuri sana mfano mtoto anataka kitu fulani analia ameshasoma saikolojia yako mzazi, wewe ukiona tu mtoto analia unamtimizia hata kama kitu siyo cha maana anampa tu hata kama una hela muda mwingine mwambie sina ili ajifunze kukosa mpe hata siku nyingine ,waingereza wanasema hivi’’ teach your child to learn or to face disappointment’’ maana yake tuwafundishe watoto kukosa au kukutana na changamoto ili wajifunze.
5. Mwisho, wape watoto chakula bora ambavyo vitawapa afya bora ya mwili na kinga dhidi ya magonjwa na hapa nazungumzia vyakula vya asili na siyo vya viwandani kama vile matunda, mboga za majani na siyo soda, pipi biskuti nk. Mpe mtoto ratiba ya kusoma vitabu au mambo yake ya darasani na siyo kuangalia tv kwa muda mrefu.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com