Katika maisha yetu ya kila siku, kuna watu tunawakosea, kuna watu wanatukosea na pia tunajikosea wenyewe. Kwa vyovyote vile mambo haya matatu yanatuacha sisi na hisia za hasira.
Kwa nini huyu mtu anifanyie hivi, kwa nini nimeshindwa kufanya kitu hiki au kwa nini nimemfanyia mtu kitu kama hiki.

Hasira hizi zinatuumiza, na kutufanya tujione sisi ni wabaya au tukose nguvu na kujiona kama watu wa kuonewa. Kwa kuwa na hasira hizi ni vigumu kuwa na maisha mazuri na yenye furaha,
Inakuja dhana kwamba unahitaji kusamehe au kusamehewa ili maisha yaendelee vizuri, hapa ni kama makosa uliyofanyiwa au kumfanyia mtu yalipelekea hasira kuwa kubwa mpaka ikaingilia mahusiano yenu.
Ni rahisi kusema nimesamehe na watu wengi husema nimesamehe, kwa sababu aliyekukosea kakuomba msamaha au imebidi ufanye hivyo ili kurejesha yale mahusiano yenu vizuri. Lakini kusema tu nimesamehe bado hakuondoi wewe kuumia.
Wengine husema kabisa “NIMEKUSAMEHE LAKINI SITASAHAU” hapa mtu ananunua tiketi yake mwenyewe ya kuendelea kuumia kwa jambo ambalo hawezi kulibadili kwa njia yoyote ile.
Kusamehe peke yake hakutoshi, achilia. Achilia ile dhana kwamba umeonewa, achilia ile dhana kwamba wewe ni mtu mbaya, achulia ile dhana kwamba watu wanakuonea wewe, achilia ile dhana kwamba sitasahau ulichonifanyia. Kila mara unapojikumbusha jambo baya ulilofanya au ulilofanyiwa na mtu unaibua zile hisia za hasira au za kujiona hufai au kujiona unaonewa. Hisia hizi sio nzuri kwa afya yako na maisha yako pia.
SOMA; Unahitaji Kuwa Sahihi Au Kuwa Na Furaha?
Achilia, usidhulumu maisha yako kwa mambo yaliyopita. Jipe nafasi ya kukosea, wape nafasi ya kukosea na songa mbele na maisha yako. Muda wenyewe wa kuwepo hapa duniani ni mchache, usiupoteze kwa mambo yasiyo ya msingi.
TAMKO LA LEO;
Najua nimekuwa nasamehe ila nashindwa kuachilia. Nimekuwa nikiona ni haki yangu kukumbuka jinsi ambavyo nimeumizwa au jinsi ambavyo nimeumiza wengine. Inaweza kuwa haki yangu kweli, lakini kufanya hivi kunaniumiza sana na mbaya zaidi siwezi kufanya chochote kubadili hali iliyopita. Kuanzia sasa naachilia chochote ambacho nimeweka kwenye moyo wangu na kinaendelea kuwa kikwazo kwangu.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.