USHAURI; Kuanzisha SACCOSS Pale Unaposhindwa Kuanzisha Kampuni.

Ni siku nyingine ambayo tunakutana kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia sisi kufikia mafanikio makubwa.
Naamini unaendelea vyema kabisa na unaendelea kutumia yale unayojifunza katika kuboresha maisha yako. Hongera sana kwa hilo.
Kuwepo kwa tatizo la ajira, yaani nafasi za ajira kuwa chache kuliko wanaozihitaji, kumewafanya watu wafikiri zaidi nje ya ajira. Hii ni nzuri sana kwa sababu italeta mabadiliko ya kifikra na pia itachochea watu kuweza kutumia uwezo wao walionao, badala ya kuamini tu kile walichofundishwa.

UMIZA KICHWA UPATE WAZO BORA.

 
Lakini pamoja na watu kuumiza kichwa kuhusiana na tatizo hili la ajira, watu wengi hawapati mfumo sahihi wa kufikiria ni kitu gani wanaweza kufanya. Wengi wamekuwa wakifikiria vitu ambavyo sio muhimu kwao kufanya au hata wakifanya havitawafikisha pale wanapotaka. Na mara nyingi hii inatokana na watu kuwa na taarifa chache kuhusiana na kitu chochote wanachotaka kufanya. Yaani pamoja na upatikanaji mkubwa wa taarifa, bado watu wengi wanashindwa kuzitafuta na kuzitumia kufanya maamuzi.
Kwa mfano tumeshatoa ushauri mara kadhaa juu ya kipi bora kufanya, kuanzisha kampuni au kuanzisha NGO. Lakini bado watu wamekuwa wakiuliza swali hili. Kama hukupata nafasi zakusoma makala hizo mbili ziko hapa;
USHAURI; Usianzishe NGO Anzisha Kampuni.(Usianzishe Msaada Anzisha Biashara)
USHAURI; Kuanzisha Asasi Zisizo Za Kiserikali(NGO) Kama Njia Ya Kutengeneza Kipato.
Katika changamoto ya leo, msomaji mwenzetu ametupeleka mbali kidogo juu ya mawazo haya ya kujitengenezea ajira. Tusome kwa pamoja maoni ya msomaji mwenzetu.

Natamani muda mrefu kuanzisha SACCOSS changamoto kubwa kuwapata washirika lakini nilitamani kuifanya kama taasisi yangu nawezaje kubadilisha wazo kwani kuanzisha kampuni inahitaji mtaji mkubwa. Naomba ushauri.
S. P

Kama tulivyoona hapo juu, msomaji mwenzetu amefikiria kwenda hatua ya mbele zaidi baada ya kuona, kwa uelewa wake yeye kwamba kuanzisha kampuni inahitaji mtaji mkubwa. Hivyo ameona ni bora aanzishe SACCOSS kwa sababu inahitaji mtaji mdogo. Lakini na hapo pia ana changamoto ya jinsi ya kuwapata washiriki.
Ningeweza kumshauri msomaji wetu hapa kuhusu uanzishwaji wa SACCOSS na jinsi gani anaweza kuwapata watu. Na pia ningeweza kumshauri juu ya uanzishwaji wa kampuni, na sio kweli kwamba unahitaji mtaji mkubwa, unaweza kuanzisha kampuni hata ukiwa na laki tatu. Lakini leo sitafanya lolote kati ya hayo, nitafanya kitu cha tofauti kabisa ambacho msomaji hakutegemea.
Ndugu msomaji ambaye unasumbuliwa na changamoto hii, na msomaji mwingine yeyote ambaye unafikiria kama hivi, napenda kukuambia kwamba, kwa sasa USIANZISHE KAMPUNI NA WALA USIANZISHE SACCOS. NARUDIA TENA, USIANZISHE KAMPUNI WALA SACCOSS, na hapa nitakupa sababu kwa nini nakukataza usifanye hivyo;
1. Huna uelewa juu ya chochote kati ya hivyo.
Kulingana na maelezo yako, huna uelewa wa kutosha juu ya vitu hivyo viwili, huna uelewa wa kutosha juu ya uanzishwaji wa SACCOSS na huna uelewa wa kutosha juu ya uanzishwaji wa KAMPUNI. Unahitaji kupata uelewa wa kutosha kwanza ndio ufanye maamuzi. Utapataje uelewa huu? Tembelea tovuti ya BRELA na utapata maelekezo yote ya kuanzisha kampuni. Kuhusu SACCOSS nenda kwa afisa ushirika kwenye wilaya unayoishi.
Sisemi huna uelewa kwa lengo la kukukatisha tamaa, ila kama ungekuwa umepata taarifa hizo mbili, juu ya kampuni au juu ya saccoss, ungekuwa umeshajua kwamba ni rahisi zaidi kuanzisha kampuni kuliko kuanzisha saccoss.
2. Unatafuta kitu rahisi cha kufanya.
Kulingana na maelezo uliyotoa hapa pia, unatafuta kitu rahisi cha kufanya, ambacho hakitakusumbua wewe ulazimike kutafuta fedha ndio ufanye. Na ndio maana ukafikiri kuanzisha saccoss ambapo watu watachangia ni rahisi kuliko kuanzisha kampuni ambayo itakuhitaji wewe utoe fedha zako.
Lakini kitu kimoja nikuambie kwenye maisha, hakuna kitu rahisi kufanya. Na hata kikiwepo kina changamoto zake kubwa. Fuatilia kwa makini uanzishwaji wa saccoss, na utakuja kuona inahitaji milolongo mirefu kuliko uanzishwaji wa kampuni.
3. Unataka iwe taasisi yako.
Unataka utakachoanzisha kiwe taasisi yako, SACCOSS haiwezi kuwa taasisi yako, hiki ni chama cha ushirika, kinahitaji watu wengi, kinahitaji uongozi, na hivyo maamuzi hutafanya wewe binafsi. Hivyo kuhusu kuwa taasisi yako binafsi, haiwezekani. Na ndio maana nakwambia usihangaike kufungua saccoss kwa sasa.
Ufanye nini sasa?
Sijakuambia usianzishe saccoss wala kampuni kwa sababu nakukatisha tamaa, au na nakuona huwezi. Niamini mimi ni mtu wa mwisho kumwambia mtu huwezi au haiwezekani.
Ila hapa nataka kukushauri kitu kimoja ambacho ni muhimu na cha kwanza kabisa kabla hata hujaamua kusajili kampuni au saccoss.
Na kwa kuwa kwenye ujumbe wako umeomba kushauriwa ni jinsi gani unaweza kubadili wazo, basi naamini utakuwa tayari kufanyia kazi kitu hiki muhimu ninachokwenda kukushauri.
Kitu hiki kinaweza kisiwe rahisi kufanya, ila ni cha uhakika zaidi. Na hakitakuhitaji utumie gharama kubwa mwanzoni.
Kabla hujafikiria uanzishe SACCOSS, KAMPUNI au hata NGO kitu muhimu kabisa kufanya ni KUTAFUTA MTEJA.
Ndio tafuta mteja kwanza, achana na hayo mambo ya usajili. Kama una wazo lolote la kibiashara, tafuta kwanza mteja wa wazo hilo. Hakikisha umeweza kumuuzia mtu kitu ambacho unataka kukigeuza biashara, na amefurahia ulichomuuzia. Tengeneza mteja wa kwanza, kisha mteja wa pili, kisha watatu halafu ukishaona wateja ni wengi ndio unaweza kufikiria ufanye kama kampuni au kama saccoss.
Dhana hasa hapa ni kukufanya wewe ufikiri vizuri zaidi ni nini hasa unataka kufanya na kujua unawezaje kukifanya.
Kwa mfano kama lengo lako halisi ni kuanzisha SACCOSS, ukiwa unajua kwamba unataka kuwawezesha watu kujiwekea akiba zao na kupata mikopo rahisi pia. Njoo na mpango huo, na tafuta watu unaoweza kuongea nao na wakakubaliana na wewe. Labda anza na fedha zako kidogo, wakopeshe watu wachache na kisha waambie kwamba wakitaka kupata mikopo mikubwa zaidi baadae, waanze kuweka akiba kidogo kidogo . kumbuka saccoss inaanzishwa na watu ambao wanajuana au wako eneo ambalo ni karibu, labda mtaani au kazini au vyovyote vile. Hivyo anza kujenga imani na watu wachache, waweke fedha na uendelee kuwakopesha, kwa kiwango cha chini sana. Sasa unapoona mpango huo unaweza kuwasaidia wengi, kaa nao chini sasa na leta wazo la kuisajili kama saccoss ili iweze kukua zaidi ya pale na watu waweze kuchangia kiwango kikubwa kuliko cha awali walichokuwa wanachangia na hivyo kuweza kuchukua mikopo mikubwa pia.
Kama lengo lako hasa ni kuanzisha kampuni, labda ya kukopesha watu, anza na fedha zako kidogo na toa mikopo midogo kwa watu ambao wana sifa za kukurudishia, fuatilia kwa makini na kadiri unavyoweza kurudisha fedha nyingi na kukua sasa unaweza kushawishi mtu mwingine mwenye uwezo akuchangie mtaji, huku ukimwahidi kwamba mtafungua kampuni pamoja na yeye utampa hisa. Kama biashara inakuendea vizuri na unaweza kuisimamia basi unasajili kampuni na unaweza kuwa na wanahisa wasio zidi hamsini lakini wewe ukajipa nafasi ya kuwa ndio mkurugenzi, kulingana na mtakavyoandaa katiba yenu ya kampuni.
Yote hayo tuliyozungumza hapo juu, kama ni kuanzisha saccoss, au kuanzisha kampuni, anza na kupata mteja kwanza, hayo mengine yatafuata.
Hivyo kama kweli upo makini, anza leo kutafuta mteja na wakati huo endelea kujifunza mfumo sahihi kwako kutumia.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: