Ni rahisi sana kutabiri kama biashara yako itafanikiwa au haitafanikiwa. Japo watu wengi huwa hawachukui hatua hii muhimu. Kwenye biashara yako, kwa bidhaa au huduma unayotoa, wewe mwenyewe kwenye moyo wako unaweza kuwa unajua kama unatoa thamani kweli au hutoi thamani. Leo tutajadili swali moja muhimu sana unalotakiwa kujiuliza kila siku kwenye biashara yako ili uweze kuikuza zaidi.
Swali hili linaegemea sana kwa upande wa wateja kwa sababu bila ya wateja biashara hakuna. Hata kama ungekuwa na bidhaa au huduma bora kiasi gani, kama huna wateja basi huna biashara. Kwa sababu wateja ni sehemu muhimu sana ya biashara yako, basi wanastahili kupewa uzito wa kipekee.
Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba walianzisha biashara na kuwa na wateja wengi, ila baadaye walikuja watu na kuanzisha biashara kama ile ambayo wanafanya wao na hii ikasababisha wateja wote kuhamia kwenye biashara za washindani. Watu wanalalamikia hili kwamba ushindani umekuwa mgumu kwao. Lakini kiuhalisia sio jambo la kulalamikia, kama wewe ni mfanyabiashara makini na ambaye unaijali biashara yako ulitakiwa kuliona hilo kabla hata halijatokea.
Njia rahisi sana ya kuliona hilo kabla hata halijatokea ni kujiuliza swali hili muhimu kila siku na kila mara, je mteja wa biashara yangu akaamua kuondoka kwenye biashara yangu, je atakwenda kwenye biashara ya aina gani? Kama mteja ataondoka kwangu kwa sababu hajaridhishwa, je atakwenda kwenye biashara ya aina gani ambayo itamridhisha? Kwa kujiuliza swali hili na kulijibu kwa ufasaha, utazuia wateja wengi sana kuondoka kwenye biashara yako.
Hutawazuia kwa kuwalazimisha waendelee kufanya biashara na wewe, ila utawazuia kwa kuhakikisha chochote watakachotaka kupata kwingine wanaweza kukipata kwako pia. Kwa njia hii utaweza kutoa huduma bora sana kwa wateja wako na wakawa wateja wa kudumu. Kama mtu mwingine atafungua biashara kama yako, wateja wanaweza kwenda kujaribu ila wakikuta kule hawapati vitu vizuri kama walivyokuwa wanapata kwako unafikiri watafanya nini? Ni lazila watarudi kwako, hakuna mtu ambaye hapendi vitu vizuri. Hakuna mtu ambaye hapendi kufaidi kile kinachopatikana zaidi. Kuweza kufanyia kazi hili kutajenga uhusiano wako na wateja wako vizuri.
Kwa biashara za sasa, huna haja ya kutumia nguvu nyingi kujua kama mteja anaridhika au la. Mteja mwenyewe yuko tayari kukuambia na hata asipokuambia wewe atawaambia wengine. Lengo lako kubwa wewe mfanyabiashara ni kuhakikisha kila kilicho ndani ya uwezo wako ambacho kinamsaidia mteja unakitoa. Ukishindwa kufanya hivyo wewe kuna wenzako ambao watakuwa tayari kufanya hivyo. Na kama watafanya vizuri, watakuondoa kwenye biashara yako ambayo huenda umekaa kwa muda mrefu.
Kamwe usiendeshe biashara yako kwa mazoea. Usifanye kitu kwa sababu ndio umezoea kufanya. Fanya kitu ambacho kinaongeza thamani kwenye biashara yako, kinafanya maisha ya mteja kuwa bora zaidi. Na endelea kuboresha biashara yako kila siku kulingana na mabadiliko yanayoendelea kutokea. Ubaya ni kwamba kama wewe hutafanya hivi, aliyeko pembeni yako atafanya, na utashangaa kuona wateja wanakimbilia kwake. Kama huelewi vizuri mambo haya utaishia kulaumu kwamba mwenzako anatumia dawa au amekufanyia machezo ambao sio mzuri. Ukweli ni kwamba dawa anayotumia ni kuhakikisha wateja wanapata huduma nzuri na mchezo mbaya umefanya mwenyewe kwa kuendesha biashara yako kwa mazoea.
Mteja rahisi kumpata kwenye biashara yako ni yule ambaye tayari unafanya naye biashara, na mteja huyu pia ndio rahisi kukuletea wateja wengine wengi zaidi. Ni jukumu lako kuhakikisha mteja huyu anakosa sababu ya kuondoka kwenye biashara yako na anakuwa tayari kuwaambia wengine nao waje kwenye biashara yako. Sio kazi ngumu kufanya, inaanza na swali; kama mteja wangu ataacha kufanya biashara na mimi, je atakwenda kwenye biashara ya aina gani? Ifanye biashara yako kuwa vile ambavyo mteja angekwenda kutafuta, na hatakwenda mbali maana ataipata kwako.
TUPO PAMOJA.