Moja ya vitu vikubwa ambavyo huwa nawashauri watu wanaotaka kubadili maisha yao ni kuanza na zoezi hili la siku kumi. Zoezi lenyewe linakutaka wewe usilalamike kwa chochote kile kwa siku kumi mfululizo, na kama ikitokea umelalamika basi unaanza tena(ni zoezi zuri sana, kama hujalifanya bado bonyeza maandishi haya kulisoma).

Sasa watu huniandikia na kuniuliza, nitaachaje kulalamika wakati naona mambo hayaendi vizuri? Ni haki yangu kulalamika bwana, kama isingekuwa serikali, leo maisha yangu yamekuwa mazuri sana.

UKIWA NA FURAHA, HAKUNA NAFASI YA KULALAMIKA
UKIWA NA FURAHA, HAKUNA NAFASI YA KULALAMIKA

Labda nikubaliane na wewe kwa muda mfupi tu ya kwamba ni haki yako kulalamika. Ila naomba unisaidie kujibu maswali haya;

Umewahi kuona mtu akilalamika siku ya harusi yake? Yaani kama ni bwana au bibi harusi amepewa nafasi ya kuongea maneno machache akaanza na malalamiko kwa serikali au chochote ambacho ana haki ya kulalamikia?

Umewahi kuona mtu akimlalamikia bosi wake siku anayopandishwa cheo? Yaani mtu amepandishwa cheo na akapewa nafasi ya kuongea machache, halafu aanze na malalamiko, ujue huyu bosi wangu amekuwa akininyanyasa sana, ananizuia mambo yangu mengi n.k

Umewahi kuona mtu anayehitimu masomo yake akiwalalamikia walimu wake? Yaani siku ya sherehe ya mahafali, halafu mhitimu anapopata nafasi ya kusema machache anaanza na mlolongo wa malalamiko yake kwa walimu ambao walikuwa wanamsumbua shuleni au chuoni?

Na swali la mwisho, kama umeshajibu hayo, umewahi kuwa umekutana na marafiki zako wa muda mrefu, mna furaha, mnapata chakula kizuri halafu kitu cha kwanza mnaanza nacho ni malalamiko kwa kitu chochote kile?

Mengi ya majibu ya hayo maswali hapo juu ni hapana. Sasa turudi kwako, muda mfupi uliopita umesema ni haki yako kulalamika, je kwa nini ukiwa kwenye hali nzuri, ukiwa kwenye furaha hulalamiki? Au tubadili, tuseme ni haki yako kulalamika ukiwa katika hali mbaya au ngumu. Kama ndivyo basi, tatizo sio yule unayemlalamikia, bali tatizo ni wewe kushindwa kuwa na furaha kwenye maisha yako.

Tunapenda kulalamika pale ambapo tunaona mambo yetu hayaendi vizuri. Na badala ya kutumia muda wetu vizuri kuyarekebisha yaende vizuri, tunautumia kulalamika, kwa sababu ni rahisi kufanya hivyo, kuliko kukaa na kuumiza akili ili uboreshe maisha yako.

Najua unajua vizuri kabisa ya kwamba kama unataka kufikia mafanikio makubwa inabidi uache kufanya vitu ambavyo ni rahisi kufanya, vitu ambavyo kila mtu anaweza kufanya. Na kulalamika ni moja ya vitu hivyo.

Unapojisikia kulalamika, jiulize ni kitu gani ambacho hukipendi kwenye maisha yako, halafu kibadili. Ni rahisi kama hivyo na maisha yako yanakuwa bora sana.

TAMKO LA LEO;

Najua nimekuwa nalalamika ili kujiondoa kwenye jukumu la kuboresha maisha yangu. Najua sijawahi kulalamika nikiwa kwenye hali ya furaha. Kuanzia sasa nitahakikisha naboresha maisha yangu badala ya kulalamika. Wakati wowote nitakapokuwa najisikia kulalamika, nitafikiria ni kitu gani ambacho sikipendi kwenye maisha yangu, halafu nitakifanyia kazi. Najua sio rahisi, lakini ndivyo ilivyo, vitu bora kwenye maisha sio rahisi.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.