Watu wengi hukubali kwamba maisha yao yanahitaji mabadiliko….
Ndio inabidi nibadili jinsi ninavyofanya kazi zangu…
Inabidi nibadili jinsi ninavyofanya biashara zangu….
Inabidi nianze kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya baadae….
Inabidi niache kupoteza muda kwa kuzurura kwenye mitandao na hata kufuatilia habari zisizo na msingi…

Lakini…..
Lakini kwa sasa wacha niendelee kufanya kazi ninavyofanya, baada ya kitu fulani ndio nitaanza mpango huo mpya.
Lakini kwa sasa wacha niendelee kufanya biashara kama nilivyozoea kufanya, haya mabadiliko nitaanza kuyatekeleza baadae.
Kwa sasa sitaanza kuweka akiba na kuwekeza, wacha kwanza nimalizane na madeni, halafu pia kipato changu kikiongezeka itakuwa rahisi kwangu kuweka akiba.
Nitaacha kupoteza muda baadae huko, sasa hivi kwanza kuna habari nyingi za kufuatilia, nani asiyejua kuna uchaguzi, nina haki ya kujua kila kinachoendelea.
SOMA; KITABU; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.
Mipango ni mizuri kabisa, ila utekelezaji unasubiri kwa sababu wengi tunaamini ni sawa kwa sasa kuendelea kufanya kile ambacho tumekuwa tunafanya. Sio mbaya, ni kama tunamalizia tu, lakini tumeshabadilika.
Lakini kwa bahati mbaya sana, mabadiliko hayatokei kwa sababu umesema utabadilika, mabadiliko yanatokea pale vitendo vyako vinapoonesha dhahiri umebadilika. Na mbaya zaidi, unachofanya sasa ndio utakachoendelea kufanya. Kama unabisha jiulize ni vitu vingapi umewahi kujiahidi utafanya ila mpaka sasa hujaanza kufanya?
Kama kweli unataka kubadili maisha yako na yawe bora sana maamuzi ya mabadiliko unayoamua leo, anza kuyatekeleza leo. umeamua utaboresha kazi yako au biashara yako anza leo, kwa hatua ndogo kabisa. Umeamua unataka kuweka akiba na kuwekeza, anza kwa kuweka elfu moja leo, na kuendelea kuanzia hapo.
Maamuzi magumu ya kubadilika utakayofanya leo ni muhimu kuliko maamuzi utakayokuja kufanya siku za mbeleni. Kwa sababu siku zote mwanzo ni mgumu, ndio maana umekuwa unakwepa sana kuanza.
Wakati mwingine utakaposema nitaanza kutekeleza mabadiliko yangu baada ya kitu fulani kutokea, jua ya kwamba unakwepa kuanza kitu hiko.
TAMKO LA LEO;
Nimejua ya kwamba mabadiliko ya kweli yanaanza sasa na sio siku zijazo. Chochote ambacho nasema nitabadili kwenye maisha yangu inabidi kianze wakati huu. Kama nitapeleka mbele maana yake nitakuwa sitaki kutekeleza mabadiliko hayo kwenye maisha yangu. Kusema nitafanya ni njia ya kukimbia mwanzo mgumu wa kutekeleza mabadiliko. Kuanzia sasa nitatekeleza mara moja kitu chochote ninachotaka kubadili kwenye maisha yangu.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.