Wewe kama mfanyabiashara, kipato unachopata kinatokana na fedha ambazo mteja analipa. Gharama zote za kuendesha maisha yako zinazotokana na biashara ni kwa sababu kuna mteja ambaye ametoa fedha zake ili kupata huduma au bidhaa unazotoa. Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba bosi hasa wa biashara yako ni mteja wako. Hii ni kwa sababu mteja ndio anakuajiri wewe na wengine wote wanaohusika na biashara yako. Na pia mteja anayo nguvu ya kuwafukuza wote kwa yeye kuamua kwenda kununua sehemu nyingine badala ya kwenye biashara yako.

Matatizo makubwa sana kwenye biashara yoyote yanaanzia kwenye eneo hili muhimu sana kwenye biashara yako ambalo ni wateja. Huduma mbovu za wateja ni chanzo cha matatizo makubwa sana kwenye biashara. Na kwa ulimwengu wa sasa ambapo wafanyabiashara wapo wengi, wateja wana nguvu kubwa sana ya kuchagua. Kama utashindwa kuwapatia kile hasa wanachotaka, wateja hawaoni shida kuacha kufanya biashara na wewe na kutafuta mtu mwingine ambaye yuko tayari.

Ni jambo la kushangaza sana kwa nini mtu aingie kwenye biashara na hatimaye ashindwe kutoa huduma kwa wateja. Unakuta mtu kaamua kuingia kwenye biashara kama ya hoteli. Anaandaa mazingira mazuri ya kutoa huduma zake. Anaanza kwa kupika vyakula bora sana na wateja wanavifurahia. Baada ya siku chache anaanza kutamani faida kubwa zaidi na hivyo anaanza kutengeneza matatizo kwenye biashara yake. Anaanza kupika vyakula ambavyo sio bora, anaweka kiasi kidogo cha vyakula na pia anaajiri wafanyakazi wasio na uwezo ili awalipe mshahara kidogo. Anafanya yote haya akifikiri anapunguza gharama, lakini anapokuja kustuka anakuta ameharibu biashara. Kwa sababu kwa huduma mbovu ambazo wateja wanakuwa wanazipata wanashindwa kuendelea kuja kwenye biashara hiyo.

SOMA;  Changamoto ya kuendesha biashara wakati bado umeajiriwa.

Kama unataka biashara yako idumu, kama unataka biashara yako iendelee kukua, basi ni lazima uzingatie sana eneo hili muhimu sana. Toa huduma nzuri kwa wateja. Jambo lolote ambalo utalifanya kwenye biashara, anza kumfikiria mteja kwanza. Chochote unachofanya, jiulize je kinaongeza thamani kwenye biashara? Je kinafanya tatizo la mteja kutatuliwa vyema zaidi? Je kinarahisisha maisha ya mteja? Kama jibu ni ndio basi fanya hivyo, kama jibu ni hapana acha kufanya kitu hiko na elekeza nguvu zako kwenye kutoa huduma bora kwa wateja.

Hapa kuna baadhi ya mambo muhimu unayoweza kufanya ili kubadili mtazamo wako juu ya huduma bora kwa wateja.

Mchukulie mteja kama rafiki yako.

Kwanza ni vile tu hatufikirii vyema ila kwa kweli mteja ni zaidi ya rafiki yako. Mteja anakupa wewe fedha za kuendesha maisha yako, za kuhakikisha familia yako inakuwa na maisha bora. Ndio unampa huduma na bidhaa lakini kwani ni wewe pekee unayefanya hivyo? Jali sana imani hii ambayo mteja ameijenga kwako. Mchukulie mteja kama rafiki na hivyo hutafanya jambo lolote ambalo halimnufaishi mteja. Unapoacha kumwangalia mteja kama mtu mwenye shida, bali rafiki ambaye anapendelea kupata bidhaa na huduma kutoka kwako, utaongeza sana huduma unazotoa kwa mteja huyo.

Usiwe na tamaa.

Kuna watu wengi wanaamini kwamba tupo kwenye biashara ya soko huria na kwa sababu mtaji ni wako na biashara ni yako, basi unayo haki ya kufanya chochote unachotaka kwenye biashara yako. Ni kweli kwa maelezo ila katika ufanyaji wa biashara huna uwezo wa kufanya chochote unachotaka. Mwenye uwezo huo ni mteja peke yake, yeye ndiye anayeweza kuamua anunua kwako au aende kwa mshindani wako ambaye wala hayupo mbali kutoka hapo ulipo wewe. Kama utaendekeza tamaa na kutaka kupata faida kubwa kuliko thamani unayotoa, unaweza kupata faida hiyo ila itakuwa ya muda mfupi sana. Uhusiano mzuri utakaojenga na mteja sasa ni muhimu kuliko faida yoyote kubwa ambayo unaifikiria kwa sasa.

Huduma kwa wateja ni eneo muhimu sana kwenye biashara yako. Kama unataka biashara yako idumu hakikisha mteja wako anapata kile ambacho kinaendana na thamani anayolipia. Mfanye mteja kuwa rafiki yako ili umjali zaidi. Pia usiwe na tamaa ya kufaidika haraka, wekeza kwenye kujenga mahusiano mazuri na mteja na mahusiano haya yatakuletea faida kubwa zaidi baadae.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani