Habari za wakati huu rafiki?

Naamini uko vizuri sana, hongera kwa hilo. Na hata kama haupo vizuri usiwe na shaka, mambo yatakwenda vizuri. Kikubwa ni wewe uendelee kufanya yale ambayo umepanga kufanya.

Kabla hatujaingia kwenye mazungumzo yetu ya leo naomba kuna mambo mawili muhimu ya kukuambia;

  1. Kwanza nashukuru sana wewe kama rafiki yangu kujiunga kwenye mpango wa kutumiwa ujumbe mzuri kila siku asubuhi. Mwitikio wa mpango ule ambao nilikushirikisha jana umekuwa mkubwa sana. Bado mipango inaendelea ili uanze kupokea jumbe zile. Kama hukupata taarifa kuhusu mpango huo wa ujumbe soma; AMKA Kila Siku Ukiwa Na Hamasa Kubwa Ya Kufikia Mafanikio Makubwa. Zoezi Moja Muhimu Kufanya Kila Siku.
  2. Kuna baadhi wameuliza kuhusu kujiunga na kundi la WASAP, naomba nitoe ufafanuzi kwa hilo. Ili uunganishwe kwenye kundi la wasap unahitaji uwe mwanachama wa GOLD kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Unaingia kisimachamaarifa.co.tz unabonyeza sehemu ya kujiunga kisha unaweka taarifa zako. Baada ya hapo unatuma ada ya uanachama ambayo ni tsh elfu 50 na unapata nafasi ya kusoma makala zote kwenye KISIMA na kuingia kwenye kundi hilo la wasap ambalo lina watu wenye mtizamo chanya tu. Karibu sana.
  3. La mwisho kabisa, samahani nilisema mawili ila kuna hili la kuongezea kwa hapo juu kuhusu mpango wa ujumbe kila siku asubuhi. Najua kuna watu unaowajua ambao hawana mtandao na hawajaweza kujifunza kupitia blog tunazoendesha. Lakini watu hawa wana simu za mkononi. Tafadhali waandikie ujumbe kuwajulisha kwamba kuna huduma nzuri ya kutumiwa ujumbe mzuri kila siku asubuhi na kama watapendelea hilo, wao wenyewe watume ujumbe wa maneno kwenda namba 0717396253 wakiandika majina yao na namba ya simu wanayotaka ujumbe uwe unatumwa. Fanya hivyo ili kuwasaidia wengi zaidi kupata mambo haya mazuri. Nilifurahi sana jana kuna wengi walifanya hivi.

Asante sana, naamini utakwenda kufanyia kazi mambo hayo matatu muhimu.

Tayari nimeshaandika maneno mengi hapa na leo nilitaka tuongelee kitu kikubwa sana ambacho kitabadili maisha yako kwa kiasi kikubwa, kwa sababu kimebadili maisha yangu sana. Nitaomba uniwie radhi tukijadili kwa undani sana siku nyingine, nafikiri jumanne ijayo kwa sababu alhamisi tayari kuna kitu kingine kizuri cha kukushirikisha. Si tupo pamoja? Asante sana rafiki.

Basi tufanye nini hapa basi?

Tuangalie kwa kifupi kuhusu kukatishwa tamaa na kukata tamaa. Narudia haya mara nyingi kwa sababu nimekuwa naiona sana nguvu ya kukatishwa tamaa kwenye jamii zetu. Akili za kila mtu anayekuzunguka zipo tayari kukukatisha tamaa kuliko kukuunga mkono. Ni jambo la kusikitisha sana lakini ndio ukweli wenyewe. Sasa kwa nini iko hivi?

Unakumbuka nilishakwambia napenda sana kujifunza tabia za watu, yaani kwa nini watu wanafanya kile ambacho wanafanya? Huwa naiuliza kwa nini kwa kila kitu, halafu naanza kutafuta majibu hayo ya kwa nini.

Nilianza kulifuatilia hili kwa undani baada ya kuona kwamba naweza kuandika makala nzuri sana, ambayo najua kabisa itakwenda kumsaidia mtu atakayeifanyia kazi, mtu anaisoma lakini anatafuta kitu kimoja cha kukataa kwenye makala hiyo. Lakini ukiangalia kuna vitu vingi vizuri vya kujifunza, ila yeye kachagua kimoja cha kupinga na anakisimamia hiko.

Siku nyingine kwenye mtandao wa kijamii kuna mtu aliweka picha yake akiwashirikisha watu nafasi aliyopata ya kuongea kwenye mkutano wa mafunzo na uhamasishaji kwa vijana wanaoingia kwenye ujasiriamali, mimi binafsi niliona ni kitu kizuri, lakini nilipoangalia maono ya wengine, machache ya juu walimsifia kwa kile alichofanya, akaja mmoja na kuweka maoni yake kwamba, mbona sasa hivi unapata kitambi, basi baada ya hapo kila mtu aliweka maoni yake kuhusu kitambi. Wote wakasahau kazi nzuri aliyoifanya nakuanza kumwambia kuhusu kitambi chake ambacho kimeanza kujitokeza.

Kwa nini yote haya, kwa nini watu wanapenda kutafuta kibaya kati ya vitu vizuri?

Baada ya kujifunza kwa muda nimejua ya kwamba kutafuta mabaya ni tabia ambayo binadamu tumejijengea kwa muda mrefu. Binadamu tumekuwepo hapa duniani kwa zaidi ya miaka bilioni(samahani kama imani yako inasema tofauti), katika kipindi hiki, kuna viumbe wengi ambao wametoweka, kwa sababu mazingira yalikuwa magumu sana. Ili kuhakikisha binadamu tunapona yote haya, binadamu tumejiwekea umakini mkubwa sana ndani yetu. Tupo makini sana kutafuta tatizo lolote kwenye kitu. Ni rahisi sana kuona kosa au kitu kibaya ili tuweze kujiandaa kukabiliana nacho.

Sasa tabia hii imekwenda mbali zaidi na kuwa sehemu ya kukatishana tamaa. Kwa sasa hatuishi tena kwenye hatari ambayo vizazi vilivyotangulia waliishi, lakini bado tumeendelea na tabia hii na imekuwa kikwazo kwa wengine kupiga hatua.

Kutokana na historia hii ya kujikinga na hatari ambayo binadamu tumejijengea, kitu chochote ambacho hukijui ni hatari kwako. Nafikiri ungekuwa unaishi kati kati ya msitu mwaka 1520 na ukakutana na mnyama ambaye hujawahi kumuona kwenye macho yako, ni salama zaidi kufikiria mnyama yule ni hatari na hivyo kujiokoa. Lakini ulimwengu tunaoishi kwa sasa hauna tena hatari hizo, ila sisi wenyewe tumeendelea kuzitengeneza.

Kitu chochote ambacho hukijui unakichukulia kwamba ni hatari. Kitu ambacho hujawahi kufanya unachukulia ni hatari. Na hivyo hii inakuweka kwenye hali ya kujiona upo salama hata kama sio kweli.

Kwa mfano, mtu ambaye amezoea kuwepo kwenye ajira imani yake kubwa ni kwamba maisha nje ya ajira ni hatari sana. Hivyo ajira inaweza kuwa ngumu sana kwake, inaweza kuwa haikupatii kipato cha kutosha, inaweza kuwa haikufurahishi, lakini kwa kuwa tafsiri yako ya maisha nje ya ajira ni hatari, utaendelea kung’ang’ana na ajira ile.

Kama unataka kufanya kitu ambacho watu wengine hawajawahi kufanya, na ukawaambia mpango wako huo, wengi watakukatisha tamaa, watakuambia huwezi, watakuambia utashindwa. Sio kwa sababu wana uhakika na hilo, bali kwa kuwa hawajawahi kuona kikifanyika, hata kama wamewahi kuona basi hawajawahi kuona mtu wa aina yako akifanya. Wanarudi kwenye tafsiri iliyojengeka kwenye akili zao kwamba chochote usichokijua ni hatari. Na kwa kuwa wanakupenda sana, hawataki kukuona ukiingia kwenye hatari hiyo.

Sasa leo nataka nikushirikishe kitu kimoja muhimu sana.

Kitu hiko ni wewe kuwa hatari kwa wale ambao wanakuonesha hatari.

Kwa mfano utakapowaambia watu kwamba unataka kufanya kitu fulani, watakimbilia kukuambia kwamba ni hatari. Kwa sababu wewe umeshapima na kuona inawezekana na umeshaamua kwamba liwalo na liwe ila lazima ufanye kitu hiko, endelea kufanya. Utakapoanza kufanya watasema subiri tuone, utakapoendelea na kutojali maneno yao watastuka na kukuona wewe sio wa kawaida ni hatari. Na utakapofikia kile ambacho uliwaambia unataka kufikia watakuona wewe ni kiumbe hatari sana. Na heshima itakuwa kubwa kwa sababu umeonesha kiwango cha juu cha utofauti kuliko waliokuwa wanakukatisha tamaa.

Hivyo nimalize kwa kukuambia kwamba usipokata tamaa, wakatishaji tamaa watakata tamaa wao wenyewe. Kwa sababu watakuona wewe sio wa kawaida na watarudi kwenye msingi kwamba chochote usichoelewa ni hatari kwako. Na wewe utakuwa hatari kwa wengi pale ambapo utaweza kufikia ndoto kubwa ambazo wengi wanafikiri haziwezekani.

Kichwa cha habari cha mazungumzo yetu ya leo nitaomba uweke USIPOKATA TAMAA, WATAKATA TAMAA WENYEWE. Halafu hiki tulichopanga kujadili leo tutajadili wiki ijayo.

Je unachagua kuendelea kufanya au unachagua kuwasikiliza ambao hawajui? Maisha ni yako na chaguo ni lako. Ila kwa kuwa wewe ni rafiki yangu, naomba nikusihi kwamba endelea kufanya, usikubali kununua hadithi za bei rahisi kwamba fulani alianza kama wewe na aliishia kushindwa, huyo ni fulani, sio wewe. Hakuna anayejua wewe unaweza nini na huwezi nini.

Usiniangushe rafiki yangu, nakutegemea sana wewe ulete mapinduzi kwenye maisha yako na ya wale wanaokuzunguka, ili siku moja tutakapokutana kileleni tuwe na hadithi nzuri za kuambiana na kuwaambia wengine pia.

MAKALA ZA KUSOMA;

  1. Hapa kuna sababu tatu kwa nini hufanikiwi kwneye kazi yako licha ya kujitahidi sana; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
  2. Kama unapanga kuleta mabadiliko popote ulipo jiandae kwa changamoto hizi mbili; Changamoto Mbili Kubwa Utakazokutana Nazo Wakati Wa Mabadiliko.
  3. Bado mpaka sasa unafanya biashara kienyeji? Unakosa mambo haya mazuri; Faida Tano(5) Za Kurasimisha Biashara Yako Na Kuiendesha Kitaalamu.
  4. Unataka kujenga timu nzuri ya kazi/biashara au kikundi ambacho mtaweza kufanya makubwa? Zingatia aina hizi tatu za watu; Kuna Aina (3) za Watu Unahohitaji Kwenye Timu Au Kikundi Ili Kufikia Malengo Makubwa.
  5. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya.

Nikutakie mapambano mema rafiki yangu, jifunze, fanyia kazi na boresha zaidi, KILA SIKU.

Rafiki na Kocha wako.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz