Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha 100 Ways To Motivate Others(Njia 100 Za Kuwahamasisha Wengine)

Habari msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Natumaini unaendelea vizuri. Wiki hii nakukaribisha katika utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu. Wiki hii tunaangazia kitabu kinachoitwa 100 Ways to Motivate others, kitabu hiki kimeandikwa na Steve Chandler. Kitabu hiki kinazungumzia Njia 100 za kuwahamasisha wengine, kinazungumzia vizuri sana jinsi viongozi wanavyoweza kuongoza watu na kuwafanya wafikie mafanikio makubwa bila kuwaburuza. Pia kitabu kinaonyesha utofauti uliopo kati ya kiongozi na Meneja.

 
Karibu tujifunze kwenye kitabu hiki
1. Kiongozi unapaswa kuongoza kwa mfano. Hakuna kitu chenye hamasa kama kuongoza kutokea mbele, hii inahamasisha sana wengine. Japo kuongoza ukiwa mstari wa mbele ni kugumu, lakini ndiko kunakodumu muda mrefu kwenye akili za wale unaowaongoza. Kama unataka watu wako wawe na mawazo chanya, anza wewe kwanza kua chanya, Kama unataka wawe wanafika kwa wakati kazini, unapaswa uonyeshe kwa vitendo kwa kua wa kwanza. Show them how it’s done. To really motivate, talk less and demonstrate more.
2. Chanzo kikuu cha msongo wa mawazo (stress) kazini, ni pale akili yako inapojaribu kubeba mawazo mengi, majukumu mengi, wasiwasi mwingi kwa wakati mmoja. Hakuna anayeweza kubeba yote hayo kwa wakati mmoja, hata akili ya genius kama Albert Einstein haiwezi kubeba hayo yote. Akili imeumbwa kubeba jambo moja kwa wakati. Kwa hiyo kuepukana na msongo wa mawazo, kwenye orodha yako ya majukumu yakufanya (to do list) anza kwa kuchagua jambo moja kwanza, litekeleze, ukimaliza nenda kwenye jambo lingine.
3. Meneja wengi hawana ufanisi katika kazi zao, kwa sababu ni watu wa kuzima moto. Hawana mipango, na hata kama ipo haitekelezwi, badala yake muda mwingi kinachotekelezwa ni kile cha kinachokuja haraka. Ukiwa mtu wa kuzima moto katika shughuli, huwezi kuwa kiongozi, maana hutaweza kuongoza timu yako kule inakotakiwa kwenda, na badala yake zile shughuli za zima moto ndio zinazokuamulia mwelekeo gani wa kwenda. Moto tunaweza kufananisha na tatizo ulilonalo sasa hivi. Jitahidi matatizo yasiwe ndio yanaamua mwelekeo wako wa maisha uelekee wapi. Maana matatizo yakikuthibiti hutaweza kuziona fursa, badala yake utakua unazima moto kuyakabili matatizo.
4. Uongozi ni ujuzi (skill) kama zilivyo aina nyingine za ujuzi. Hivyo ujuzi huo unaweza kufundishwa na kujifunza pia bila kujali umri wako, ilimradi uwe na ‘commitment’ ya kufanya hivyo. Kwa hiyo ile dhana ya kwamba viongozi wanazaliwa haina mashiko kwenye zama hizi za taarifa. Kila mtu anaweza kua kiongozi akiamua kwa dhati kufanya hivyo.
5. Kampuni zimeshindwa kuwabadilisha mameneja wake kua viongozi kwa sababu Wenye kampuni kwanza hawajui hasa nini maana ya kiongozi, sasa watawezaje kuwafundisha wafanyakazi kua viongozi. Hawasomi vitabu, hawahudhurii semina za uongozi, wala hawajisumbui kuandaa mikutano ambapo maada ya uongozi inajadiliwa. Kwa hiyo hawawezi kua na ufahamu mzuri kuhusiana na uongozi, wao wanabaki wakiamini kwamba viongozi wanazaliwa. Kama unamiliki kampuni na umeajiri watu ni muhimu sana kujifunza uongozi na kuwafundisha wafanyakazi wako, maana ni ngumu sana kuweza kuwahamasisha wafanyakazi wako kama Wewe mwenyewe hujui nini maana ya Uongozi.
SOMA; AMKA Kila Siku Ukiwa Na Hamasa Kubwa Ya Kufikia Mafanikio Makubwa. Zoezi Moja Muhimu Kufanya Kila Siku.
6. Utendaji kazi wa watu unaowaongoza au uliowaajiri unategemea sana na jinsi wanavyojiona. Kama wanaona hawana thamani ujue hata utendaji kazi utakua duni, na kama wanajiona wenye thamani hivyohivyo utendaji kazi utakua wa kiwango cha juu. Changamoto yako kiongozi ni kufanya timu yako ijione yenye thamani. If you create a new possibility for them, and communicate that to them, their performance will instantly take off.
7. Njia nzuri zaidi ya kutengeneza timu ya watu/ wafanyakazi walio na hamasa, ni kuajiri watu ambao tayari wamehamasika. Badala ya kuchukua mtu yeyote tu na kuja kuanza kumtengeneza kua na hamasa, (kitu ambacho kinaweza kuchukua muda na wakati mwingine anaweza asiwe mwenye hamasa) hakikisha unaajiri mtu ambaye amehamasika. Waajiri makini wanaojua nini maana ya kua na timu nzuri, wanakua makini sana katika kuajiri. Hawaangalii vigezo vya elimu pekee yake, wanakwenda mbele zaidi kujua jinsi gani huyo mtu anavyoweza kuhusiana na watu, jinsi gani anavyoweza kujihamasisha yeye mwenye na kuhamasisha wengine.
8. Kundi la kondoo linaloongozwa na Simba ni bora kuliko kundi la Simba linaloongozwa na kondoo. Kiongozi akiwa ni dhaifu hata awe na wapambanaji hodari kiasi gani hataweza kushinda vita, Kiongozi akishaonyesha udhaifu wale anaowaongoza na wao pia wanaingiwa na hofu, na kuanza kuhoji uwezo wao wa kushinda. Kingozi anapaswa kuwa Shupavu
9. Fanya mjadala na WEWE (Debate with yourself). Japo mara nyingi mtu akionekana anajihoji peke yake anaonekana kama mwendawazimu. Lakini Ukweli ni kwamba unapohoji ufikiri wako, unaanza kwenda kwenye viwango vipya vya kufikiri.
10. Mteja ndiyo bosi. Mteja ndiye anayelipa mishahara ya wafanya kazi, ndiye anayelipa kodi, ndiye anayelipa gharama zote za uendeshaji. Mteja ndiye mwenye uwezo wa kukufukuza kazi kwenye kampuni kwa kwenda kutumia fedha yake kwa kampuni nyingine. Mteja anapaswa kutunzwa sana. Lengo kuu la biashara yako linapaswa kua ni kumjali vizuri mteja wako, kiasi ambacho mteja atatengeneza tabia ya kurudi kwako tena na tena na kununua zaidi na zaidi.
SOMA; Falsafa Tatu(3) Za Maisha Yako Na Jinsi Zinavyoweza Kukuletea Mafanikio Makubwa.
11. Uongozi sio sana kwa habari ya mbinu na njia, bali ni kule kua na moyo ulio wazi. Uongozi sio formula au program, bali shughuli ya kiutu inayotoka moyoni na kufikiria mioyo ya wengine. Leadership is about inspiration— of oneself and of others.
12. Utafurahia sana kuhamasisha wengine kama utachukulia maisha kama mahesabu ya kutoa na kujumlisha. Hii iko hivi: Unapokua na mtazamo chanya (+) basi unaongeza kitu kwenye maongezi au mahusiano au hata kwenye kikao ambacho wewe unashiriki. Unapokua hasi (-) ina maana unatoa kitu kwenye maongezi, mahusiano au kwenye kikao ambacho upo. Ukiwa hasi (-) wewe ni mtu wa kukosoa tu, wa kuona mabaya tu, basi ujue ndivyo unavyoporomosha mahusiano yako. It’s the law of the universe up there on the flip chart of life: positive adds, negative subtracts.
13. Njia nzuri ya kua na mawazo mazuri, ni kua na mawazo mengi. Usichoke kuwaza, kila wazo unalopata, liandike mahali. Tengeneza utaratibu wa kuvumbua mawazo na kuyaandika. Huwezi kua na mawazo 100 haafu yote yawe hayafai. Hakikisha hukaukiwi mawazo, kua mtu wa kuzalisha mawazo mengi, na katikati ya hayo mengi yapo yatakayokua ni mazuri sana.
14. Endelea kujifunza (keep learning). Usionyeshe watu unaowaongoza kwamba unajua kila kitu. Wacha watambue kwamba upo mchakato wa kujifunza. Hii itawafanya watu wakufuate kwa urahisi wakiwa na mawazo mazuri. Ukweli ni kwamba vipo vingi sana vya kujifunza kwa wale unaowaongoza. Ila Meneja wengi wanapenda kuonyesha kwamba wanajua kila kitu, na wanajua kuzidi yeyote. Ukiwa na mtazamo huu basi utaharibu unaowaongoza.
15. Tofauti kati ya Kiongozi na Meneja. Kiongozi anabuni vitu, meneja anatawala vitu. Kiongozi ana focus kwa watu anaowaongoza, meneja ana focus katika mifumo na miundo inayowaongoza watu (systems and structures). Kiongozi anahamasisha watu, meneja anadhibiti watu. Kiongozi anaona mbali meneja anaona karibu. Je wewe ni Kiongozi au Meneja?
SOMA; USHAURI; Kuanzisha SACCOSS Pale Unaposhindwa Kuanzisha Kampuni.
16. Unapaswa kutumia muda mwingi kutumia uimara wako kuliko udhaifu wako (weakness). Mara nyingi hua tunatazama zaidi udhaifu wetu kwa nia ya kutaka kuboresha, hata hivyo hujikuta tukitumia muda mwingi sana katika kurekebisha udhaifu wetu, hadi kukosa muda wa kuendelezea strengths zetu. Hii hufanya kuishia kua mtu wa kawaida tu. Mfano Wewe ni Mzazi na Mwanao ni mwanafunzi wa form IV, kwenye matokeo ya Mock amepata somo la Geography B, Biology A, Chemistry B, Mathematics D, Physics F. Je utamwambia aongeze bidii kwenye masomo yapi? Au kwa maneno mengine, utamwambia atumie muda wake mwingi kwenye masomo yapi? na Kwanini? Hapa tunaona huyu mwanafunzi uwezo wake upo kwenye masomo ya Geography, Biology, Chemistry na Biology, lakini anayo udhaifu kwenye Hesabu na Physics. Hapa asilimia kubwa ya wazazi wangewashauri watoto wao watumie muda mwingi kuweka bidii kwenye yale masomo waliyopata alama za chini sana. Hii ndiyo hali ya kawaida katika maisha, ambapo watu wanatumia muda mwingi kuhangaika na udhaifu wao, huku wakisahau nguvu walizo nazo. Usitumie muda mwingi katika udhaifu wako, badala yake tumia muda mwingi katika strengths zako ili uzidi kufanya vizuri kiasi cha kufunika ya madhaifu yako.
17. Kama wewe ni mwajiri au ni meneja unaongoza au unasimamia watu, hao unaowaongoza wanaweza kua wamegawanyika katika makundi mawili. Moja la wachapakazi wanao zalisha vizuri, na pili la wasiozalisha au wavivu. Tumia muda mwingi kwenye hilo kundi la kwanza kuliimarisha zaidi na tumia muda mchache sana na kundi la pili. Maana ni rahisi kuongeza uzalishaji kwa kutumia wale ambao tayari wana juhudi, kuliko kuanza kutumia wale ambao ni wakuamsha kwanza.
18. Uadilifu ni nyenzo muhimu sana. Wapo watu ambao hata kwao binafsi sio waadilifu, kiasi cha hata kujidanganya mwenyewe. Usipokua mwaminifu hutapata mafanikio, hata ukipata hayatadumu. Uaminifu ni kitu cha gharama hivyo usifikirie kuupata kwa watu rahisi.
19. Watu wanafanya kazi kwa hamasa pale wanapopata mrejesho (feedback). Kama wewe ni Kiongozi au Meneja jenga utaratibu wa kutoa mrejesho wa kazi Kwa wale unaowaongoza au kuwasimamia. Hususani pale, mambo yanapokua yanaenda vyema.
20. Kitu chochote unapokiwekea mawazo yako na juhudi lazima kinakua. Ndiyo maana ni muhimu sana kuwa na mawazo chanya. Ukijikita katika kuona matatizo na kulalamika basi ujue utapata matatizo zaidi na utalalamika zaidi. Hii inatupa fundisho kwamba, tuweke mawazo yetu muda mwingi kwenye yale mambo tunayoyahitaji, na si kwenye yale tusiyoyahitaji.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: