Habari za leo rafiki? Upo vizuri?
Hongera sana, leo ni siku mpya ya mwezi mpya. Mwaka ndio unakatika hivyo, vipi malengo na mipango yako kwa mwaka huu? Vinaenda sawa na kazi ya siku zinavyokwenda? Hebu tumia muda mchache leo kutafakari hilo.
Wiki iliyopita nilikuahidi kuandika makala niliyokusudia kuandika wiki ile lakini kutokana na muda kutotosha nikashinda kuiandika na badala yake tukajadili kitu kingine muhimu sana.
Sasa leo ndio leo na ninataka nikuambie ushindi mdogo sana unaopata kila siku ndio chanzo kikubwa cha mafanikio yako, kama utaweza kuutumia vizuri. Lakini kwa kuwa watu wengi huwa wanadharau vitu vidogo wamekuwa wakijinyima wao wenyewe fursa za kufikia mafanikio makubwa
Siku moja rafiki yangu David aliniuliza swali moja kwa uchungu sana, aliniuliza “hivi Amani yale ma maksi mengi tuliyofaulu nayo yametusaidia nini kwenye maisha?” lilikuwa swali la uchungu sana. Ili twende sawa, wacha nikueleze kidogo kuhusu David.
David tumesoma naye kidato cha tano na cha sita shule ya sekondari kibaha. Mwanzoni hatukuwa karibu lakini mwishoni, wakati tunakaribia mtihani wa mwisho wa kidato cha sita tulianza kuwa tunasoma pamoja na kufanya maswali pamoja. Mimi nilikuwa na lengo la kupata A kwenye masomo yote matatu, yeye pia alikuwa na malengo ya kufaulu vizuri. Yeye alikuwa akiweza zaidi somo la biolojia kuliko mimi, na mimi nilikuwa naweza zaidi somo la fizikia kuliko yeye. Somo la kemia ilikuwa tunaweza sawa.
Ushirikiano ule ulikuwa muhimu sana kwani ulitusaidia sana wote, mwisho mimi nilipata A masomo yote matatu, na yeye alipata A masomo mawili na B somo moja. Kwa vipimo vyovyote hizo ni maksi za juu sana za ufaulu.
Tukajiunga kusomea udaktari kwenye chuo kikuu cha afya MUHIMBILI. Na mwaka 2011 tulipofukuzwa, tulifukuzwa na yeye pia. Sasa aliniuliza swali lile wakati anatafakari sisi na maksi zetu kubwa bado hatujamaliza masomo ya udaktari na wakati huo kuna wengine walikuwa na maksi ndogo sana lakini kwa sasa ni madaktari.
Nilimjibu swali lake hili kwamba hatulingani hata kidogo. Maksi kubwa tulizozipata katika masomo yetu zinatujengea kujiamini kwa kiasi kikubwa sana ambacho mtu ambaye hajawahi kupata vitu vikubwa hawezi kuwa nacho. Hakuna kitu kinakupa nguvu kama kuweza kuweka lengo kubwa na ukalifikia. Ushindi wowote ambao unaupata unakujengea kujiamini ambapo kutakusaidia zaidi baadae. Mwaka 2011 baada ya kufukuzwa chuoni, mimi nilienda kufundisha na David naye alienda kufundisha, wakati kuna vijana wengi walikuwa wamehitimu na degree zao lakini hawakuwa na kazi yoyote. Ni kitu gani kilitufanya sisi tuweze kupata kazi bila hata ya kuwa na uhitimu wa chuo kikuu? Kwa sababu tulikuwa tunajiamini, kwa sababu tumewahi kufanya kitu kikubwa na kwa sababu tunaamini tunaweza kufanya tena. Na hii haitaishia hapa bali itakwenda hivi kwenye maisha yetu yote.
Usikubali kabisa kuchukulia ushindi wowote unaoupata kirahisi, huo ni mtaji mkubwa sana wa wewe kufikia mafanikio makubwa baadaye.
Kuna watu huwa wananiambia huwa najiamini sana, na wengine hudiriki kusema kujiamini kwangu kutanigharimu au ndio kumekuwa kunanigharimu. Lakini sio kweli kabisa, ndio ninajiamini sana na sijawahi kujishuku hata mara moja kwamba kuna kitu kinaweza kunishinda. Najua nitaanguka hapa na pale lakini mwisho wa siku mambo yatakuwa bora sana.
Kwa mfano ngoja nikupe historia fupi sana ya ushindi mdogo mdogo ambao nimewahi kuupata kwenye maisha yangu na ambao kila siku unanisukuma kwenda mbali zaidi.
Nilipomaliza darasa la saba, kwenye mtaa tuliokuwa tunakaa kulikuwa na fundi wa kushona viatu. Nilianza kukaa pale na nikawa namwangalia jinsi anavyoshona, baada ya siku chache nikamwomba na mimi nimsaidie kushona, alisita lakini akanipa kiatu kimoja, nikakishona vizuri, akanipa kingine tena nikashona vizuri. Basi nikawa namsaidia kushona viatu na kupaka rangi viatu karibu kila siku. Na akawa ananilipa fedha kidogo kila siku, japo ilikuwa ndogo, haikuwa sawa na mtoto mwingine aliyekuwa anashinda tu nyumbani. Fundi yule aliniamini sana kiasi kwamba hata alikuwa akisafiri kwa siku kadhaa ananiachia kila kitu, nafungua ofisi nafanya kazi na akirudi namkabidhi fedha nilizofanyia kazi. Mpaka nakwenda kuanza kidato cha kwanza nilikuwa nimekusanya fedha kiasi na nikazitumia kununua vitu vyangu binafsi.
Nilipomaliza kidato cha nne, sikumaliza hata wiki moja nyumbani. Nilikuwa nafikiria kutafuta watoto wa kufundisha nikaona inaweza kuwa changamoto. Basi nilikwenda kuongea na mjomba wangu. Yeye ni fundi ujenzi na huwa anachukua nyumba nzima ya kujenga, anaanzia msingi mpaka nyumba inahamiwa. Nilimwomba anipe kazi ya kibarua, kwanza hakuamini, aliniambia mimi ni laini sana sitaweza kazi ngumu. Nikamsisitiza ajaribu tu kunipa hata kwa bure, basi akanikaribisha kwenye kazi. Tulifanya kazi vizuri sana, nilianza kwa kubeba mchanga, kuchanganya mchanga na sementi, kusaidia kazi zinazohusiana na mahesabu na baadae nikawa naangalia kwa makini sana jinsi wanavyopanga matofali na mimi nikaanza kufanya kama wao. Kwa muda mfupi sana nilikuwa nimejifunza mambo mengi sana yanayohusu ufundi. Malipo hayakuwa makubwa sana kwa wakati ule lakini yalinitosheleza mahitaji yangu na pia niliweza kujinunulia simu yangu mwenyewe. Nakumbuka siku matokeo ya kidato cha nne yanatoka tulikuwa site na niliandikiwa ujumbe matokeo yametoka, niliondoka na kwenda kuyaangalia mjini, nilikuwa nimefaulu vizuri sana. Niliwapigia simu kule site kwamba nimefaulu vizuri sana. Wengi walisema sitarudi tena pale, lakini nilirudi na tukaendelea na kazi kwa wiki nyingine kabla sijaanza maandalizi ya kwenda kidato cha tano.
Nilipomaliza kidato cha sita, nilikaa nyumbani siku moja, siku iliyofuata niliandika barua za kuomba kazi ya kufundisha na kupeleka shule tatu, shule moja nilipofika tu nilipewa kazi pale pale na kesho yake nikaanza kufundisha, nilifundisha mpaka wiki moja kabla ya kuanza chuo kikuu. Malipo hayakuwa makubwa sana lakini niliweza kununua kompyuta yangu mwenyewe. Nakumbuka enzi zile nilikuwa mmoja wa watu wachache sana tulioingia chuoni tukiwa na kompyuta zetu wenyewe. Wengi walikuja kuzinunua wakiwa chuoni. Na kama kuna kitu kimebadili maisha yangu kwa kiasi kikubwa basi ni kumiliki kompyuta yangu mapema, nilijifunza mengi sana ninayoyatumia sasa. Nitakuja kuliandikia hili vizuri siku nyingine.
Na nilipofukuzwa chuoni, mwaka 2011, nilikaa kama mwezi mmoja tukiwa tunafuatilia mustakabali wetu, baada ya hapo niliona hakuna dalili nzuri, niliandika barua ya kuomba kazi ya kufundisha na kuisambaza shule kama sita hivi. Shule mbili waliniita wakiwa tayari kunipa kazi na nilichagua kufanya kazi na shule moja wapo. Mshahara haukuwa mkubwa sana lakini nilipata fursa nzuri sana za kuongeza kipato na baada ya siku chache tu nilianza kujiingiza kwenye shughuli nyingine za kutengeneza kipato na kuishi maisha ya kujitegemea moja kwa moja.
Wakati wowote ambapo naweza kupata hofu kwamba mambo yatakwendaje huwa najikumbusha yote hayo na nazidi kuona fursa nyingi sana sana sana. Yaani kwa mfano mtu akiniambia tunakunyang’anya kila ulichonacho sasa na utakwenda kuanza upya, hilo wala halitaniumiza. Kwa sababu najua nina uwezo, najua ninaweza kufanya vitu vingi sana, ambavyo watu wapo tayari kunilipa kwa kufanya vitu hivyo.
Kwa vyovyote vile hesabu ushindi wowote mdogo umewahi kupata, na huu utakusaidia wewe kusonga mbele zaidi. Hakuna kitu kinachotokea kwenye maisha yako ambacho hakikupi funzo.
Na huo nimekushirikisha ni ule ushindi angalau kwangu ni mkubwa kiasi, ila kuna ushindi mdogo mdogo ambao napata kila siku na unazidi kunisukuma zaidi. Kwa mfano kama kuna kitu nauza, naweza kukaa chini na kufikiria nani wanaweza kuwa wateja wa kitu hiki ambao nawafahamu au nimeshawahi kuwasikia au hata kuwaona kwenye mitandao. Natafuta majina matano kisha nawasiliana nao kuwaambia kuhusu kitu hiko, haijawahi kutokea wote wakasema hapana.
Hesabu kila ushindi unaopata na utumie kukaribisha ushindi mwingine mwingi zaidi. Hata kama ni ushindi mdogo kiasi gani, una msaada mzuri sana kwako. Kwa mfano leo nimeamka saa kumi asubuhi, nimemeditate, nimeandika makala ya KURASA, nimetuma ujumbe wa kuwaamsha na kuwahamasisha watu, na nimemaliza kuandika makala hii ambayo itamsaidia mtu ambaye amekwama kwenye maisha yake. Huu ni ushindi mkubwa sana kwangu kwa sababu kwanza nimetekeleza ratiba yangu ya kila siku, hivyo mimi ni mtu ambaye natekeleza mambo ninayopanga. Kwa kuwa najiona mtu w akutekeleza yale ninayopanga, sitakubali kuahirisha jambo lolote, litaharibu ile sifa yangu niliyojitengenezea.
Kama kuna mtu yeyote ambaye anaona maisha yake yamekwama, ambaye anaona hakuna tena njia, ambaye anaona hakuna kinachoweza kufanyika, namwambia aache kujidanganya. Tafakari maisha yako leo na chukua hatua, tunaweza kuwasiliana pia ila usije ukiwa na haraka, njia ninazokupa mimi zinafanya kazi lakini zinahitaji muda. Kama unataka fasta fasta tafuta sehemu nyingine ya kupotezea muda wako.
MAKALA ZA KUSOMA;
- Unaanza biashara na mtaji kidogo? Zingatia sana mambo haya muhimu; USHAURI; Kuanza Biashara Kwa Mtaji Kidogo, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuikuza.
- Kila siku kuna zawadi nzuri unayopewa, je unaitumiaje? Soma hapa kujua zaidi; Pokea Na Tumia Zawadi Hii Vizuri.
- Unakosa muda wa kusimamia biashara zako? Fanya mambo haya matano, yasome hapa; Huna Muda Wa Kuendesha Na Kusimamia Biashara? Fanya Mambo Haya Matano Na Utakuwa Na Muda Wa Kutosha.
- Kama mpango wako wa maisha hauhusishi maeneo haya matano muhimu unajidanganya. Yajue hapa; Kama Unataka Kuweka Mipango Bora Na Itakayotekelezeka Hakikisha Unagusa Maeneo Haya Matano Muhimu.
Soma makala hizo rafiki na utapata maarifa yatakayokuwezesha kusonga mbele zaidi. Na pia ni muhimu sana ufanyie kazi yale ambayo unajifunza. Hata kama unapitia magumu kiasi gani, jua kwamba haupo mwenyewe na wewe sio mtu wa kwanza kupitia hayo.
Rafiki Na Kocha wako,
Makirita Amani,