Kila mmoja wetu ni mhanga wa hili;
Unaanza kazi mpya, unakuwa na ari kubwa sana, una imani pia ya kwamba utafanya makubwa na mambo yako yatakuwa vizuri ila baada ya muda ari ile inakuwa imeisha kabisa na unasukuma tu siku ziende.

Unaanza biashara mpya, unakuwa na hamasa kubwa sana, una amini biashara ile itakuwa ya kipekee na utaweka juhudi zako zote kuikuza, ila baada ya muda unajikuta hujui hata ni wapi hamasa ile imepotelea, kwani huna tena nguvu hata kidogo ya kuendelea.
Unapanga mpango mpya, labda kuanza mazoezi, au kubadili tabia yako, au kuanza kuandika, unajipanga vizuri, unaanza kwa hamasa, lakini muda mchache baadae unapotea kabisa.
Unabisha hujawahi kukutana na hali kama hii?
SOMA; Njia Rahisi Ya Wewe Kuondokana Na Tabia Usiyoipenda.
Unafanya nini sasa?
Kwanza lazima ujue hali hii inasababishwa na nini.
Hali hii inasababishwa na kusahau ile picha kubwa baada ya changamoto kuingia.
Ulipokuwa unaingia kwenye kazi mpya, ulichokuwa unaona ni picha kubwa ya mafanikio, huenda siku moja ungekuwa bosi, kipato kinakuwa bora, kazi ya kuheshimika. Lakini ulipoingia kwenye kazi yenyewe, umekutana na changamoto nyingi, siasa za ofisini, unafanya kazi mwingine anachukua sifa, watu wanakutengenezea majungu na mengine mengi. Matatizo kama haya yanakufanya usahau ile ndoto/picha kubwa uliyokuwa nayo na hivyo hamasa yote kuisha.
Ulipokuwa unaingia kwenye biashara mpya, ulichokuwa unaona ni faida, huenda kwa wengine wanaoendesha biashara kama ile. Lakini hukuwahi kuona changamoto zake, sasa umeingia na umekutana na changamoto, na changamoto hizi zinateka akili yako kiasi kwamba unasahau ile picha kubwa.
Kikubwa cha kufanya…
Chochote kinachotokea, hakikisha hupotezi ile picha kubwa uliyokuwa nayo. Hata kama mambo yamekuwa magumu kiasi gani, tenga muda kila siku na jikumbushe ile picha kubwa. Tengeneza kabisa taswira ya picha ile kwenye akili yako na jione uko pale ambapo unataka kufikia.
Kwa kufanya hivi utaruhusu moto uendelee kuwaka hata kama utakuwa unapitia changamoto.
TAMKO LA LEO;
Najua hamasa kubwa ninayoanza nayo kwenye mambo mapya hupotea pale ambapo ninasahau picha/ndoto kubwa niliyokuwa nayo kutokana na changamoto ninazokuwa napitia kwa wakati huo. Kuanzia sasa sitakubali tena kupoteza picha hii, kila siku nitatenga dakika chache za kupitia tena picha hii, kujikumbusha kwa nini nimeingia kwenye jambo hili na kuendelea kuweka juhudi. NI LAZIMA MOTO UENDELEE KUWAKA NDANI YANGU, HAPA NDIPO MAFANIKIO HUANZIA.
NENO LA LEO.
Karibu kwenye kipengele kipya cha neno la leo ambapo tunapata kauli iliyopata kusemwa na watu ambao waliweza au wameweza kufanya mambo makubwa kwenye jamii zao.
Today is life-the only life you are sure of. Make the most of today. Get interested in something. Shake yourself awake. Develop a hobby. Let the winds of enthusiasm sweep through you. Live today with gusto. – Dale Carnegie
Leo ndio siku pekee ambayo una uhakika nayo kwenye maisha yako. Itumie siku hii vizuri. Kuwa na nia ya kufanya kitu. Jisukume. Fanya kitu unachopenda kufanya. Acha upepo wa shauku ukupepee. Ishi leo ukiwa na hamasa kubwa.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.