Tunapoangalia mafanikio ya watu wengine, mara nyingi huwa tunaona matokeo.

Alianza kuuza karanga na sasa anamiliki mahoteli…

Alianza kuuza chipsi na sasa anamiliki viwanda…

Alikuwa hana pa kulala ila sasa ni tajiri.

Ni hadithi nzuri sana hizi kuzisikia, zinatia moyo na ninatupa uhakika kwamba inawezekana.

Tatizo kubwa ni kwamba watu wengi huwa wanaishia kwenye kuangalia na kufurahia haya matokeo.

Hawaangalii mchakato ambao watu hawa wanakuwa wametumia mpaka kutoka chini na kufika juu sana.

Na watu wote hao wanakuwa wamepitia mchakato mgumu sana, wanakuwa wamekutana na vikwazo vingi, wanakuwa wamefanya vitu ambavyo watu wengine wasingethubutu kabisa kufanya. Ndio maana wanakuwa wamefika pale.

SOMA; Usidharau Ushindi Mdogo Mdogo Unaoupata Kila Siku, Ni Muhimu Kwa Mafanikio Yako, SEHEMU YA PILI.

Watu wanapofurahia kwamba huyu alianza kwa kuuza karanga, wanasahau kwamba hakuwa anauza karanga peke yake. Mbona wauza karanga wengine hawakufikia kiwango hiko cha mafanikio?

Watu hawapendi kuangalia na kujifunza kuhusu mchakato mzima, kwa sababu mchakato hauna hadithi nzuri, mchakato umejaa maumivu, kwa kifupi hadithi ya mchakato haina utamu wa kusikiliza, na watu wanachotaka ni utamu wa kusikiliza.

Kuanzia sasa, wewe kama mtu makini, usiishie tu kufurahia matokeo na kuona kama fulani aliweza na wewe utaweza. Sio rahisi hivyo, zama ndani na anza kuchunguza mchakato mzima uliomfikisha pale na jiulize je upo tayari kujitoa kisi hiko? Uko tayari kujiweka kwenye hatari kubwa kama aliyopitia yeye.

Hapa kweli ndio utakuwa umeanza kufikiri kimafanikio zaidi na sio ulevi wa hadithi tamu ambazo kila mtu anazifurahia.

 

TAMKO LA LEO;

Najua mafanikio yoyote ninayoyaona kwa watu yana mchakato mrefu na mgumu sana ndani yake. Najua tunachoona na ambacho wengi wanafurahia ni matokeo. Na matokeo hayawezi kunisaidia mimi kwenda mbele zaidi. Kila nitakapoona mtu aliyepata mafanikio, wakati wengine wanafurahia matokeo, mimi nitakazana kujua mchakato aliopitia. Najua nitajifunza mengi sana kwenye mchakato kuliko kwenye matokeo.

NENO LA LEO.

Success consists of going from failure to failure without loss of enthusiasm.

Winston Churchill

Mafanikio ni kuweza kuendelea kwenda mbele hata baada ya kushindwa bila ya kupoteza hamasa.

 

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.