Maamuzi yote ambayo kila mmoja wetu anafanya kwenye maisha, yanaendeshwa na moja kati ya nguvu hizi mbili, HOFU au NDOTO.

Maamuzi tunayofanya kwenye kazi, kwenye biashara na hata maeneo yote muhimu kwenye maisha, yanatokana na jinsi tunavyochukulia nguvu hizi mbili.
Maamuzi yanayofanywa kutokana na hofu huwa yanaendeshwa na hofu ya kuaibika, hofu ya kuonekana mjinga, hofu ya kukataliwa, hofu ya kuumizwa, hofu ya kuacha peke yako, hofu ya kufa.
Kwa kuogopa chochote kati ya hiko kinaweza kutokea, watu huchukua maamuzi haraka sana.
SOMA; RICH DAD; Somo la kwanza; MATAJIRI HAWAFANYII KAZI PESA.
Maamuzi yanayofanywa kutokana na ndoto huwa yanaendeshwa na ndoto ya kuleta tofauti, ndoto ya kuonekana, ndoto ya kuwa huru, ndoto ya kuwa imara, ndoto ya kuwafanya wengine wajisikie vizuri, ndoto ya kupendwa.
Je wewe unafanya maamuzi yako kwa kuendeshwa na nini? Hofu au ndoto?
Maamuzi yanayoendeshwa na hofu huwa sio maamuzi bora na huwa hayaleti mafanikio makubwa. Haya ni maamuzi yanayohakikisha unakuwa wa kawaida ili maisha yako yaende kama ya wengine.
Maamuzi yanayoendeshwa na ndoto huwa ni maamuzi bora sana na yanapelekea kufikia mafanikio makubwa. Haya ni maamuzi yanayokufanya ufikie kile kikubwa unachopanga kufikia. Na kama ndoto ni kubwa kweli, utapata mafanikio makubwa sana.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba maamuzi yote ninayofanya kwenye maisha yangu yanatokana na moja kati ya nguvu hizi mbili, hofu au ndoto. Maamuzi yanayoendeshwa na hofu ni yale yanayonisukuma niwe kawaida, niwe kama wengine. Maamuzi yanayoendeshwa na ndoto ni maamuzi yanayonifanya niwe tofauti na nifanye kile ambacho ni bora zaidi. Kuanzia sasa nitafanya maamuzi ambayo yanaendeshwa na NDOTO NA SIO HOFU.
NENO LA LEO.
Too many of us are not living our dreams because we are living our fears.
– Les Brown
Wengi wetu hatuishi NDOTO zetu kwa sababu tunaishi HOFU zetu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.