Jamani hii ni vita,

Halafu ni safari ndefu sana.

Halafu maisha yako ndio haya, huwezi kuyasimamisha uje uyaishi baadae.

Mara nyingi tunapozungumzia mafanikio, watu huwa na picha ya vitu vikubwa ambavyo wamevifikia, ni vizuri sana, kwa sababu mafanikio yana maana tofauti kwa watu tofauti.

FURAHIA MAISHA, MAFANIKIO SIO KILA UNACHOPATA, BALI MAISHA ULIYOISHI.
FURAHIA MAISHA, MAFANIKIO SIO KILA UNACHOPATA, BALI MAISHA ULIYOISHI.

Na mafanikio haya yanaweza kumfanya mwingine afurahie maisha na mwingine aone maisha ni machungu na hayana maana.

Mafanikio yanaposhikizwa kwenye vitu, maisha yanaweza kuwa machungu sana.

Kwamba nikishakuwa na nyumba kubwa ya ndoto yangu ndio mafanikio, nikishakuwa na biashara kubwa ya ndoto yangu ndio mafanikio, nikishakuwa na cheo kikubwa kazini ndio mafanikio. Na mengine mengi.

SOMA; Usidharau Ushindi Mdogo Mdogo Unaoupata Kila Siku, Ni Muhimu Kwa Mafanikio Yako

Lakini je haya ndio mafanikio yoyote. Vitu vingi unavyopanga vitakuchukua muda kuvifikia, je kwa wakati huu huna maisha?

Yafanye mafanikio kuwa ni kila siku ambayo umeweza kuweka juhudi na kuleta mabadiliko.

Yafanye mafanikio kuwa ni kila ulichojaribu leo kuyafanya maisha yako na ya wengine kuwa bora zaidi. Kwa njia hii utaifurahia safari ya mafanikio na kila siku kwako itakuwa na mafanikio.

Na unapoifanya kila siku kuwa mafanikio unajikuta moja kwa moja unafanya kile kilicho bora kila siku.

Na ukweli ni kwamba, mafanikio sio tukio moja, bali ni mkusanyiko wa matukio mengi madogo madogo unayofanya kila siku.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba njia rahisi ya kuyafanya maisha yangu kuwa ya hovyo ni kushikiza mafanikio kwenye vitu. Kusubiri mpaka niwe na kitu fulani ndio nione nimefanikiwa. Mafanikio hayaji kutokana na kitu, bali yanakuja kutokana na ninavyoweza kuishi siku zangu vizuri, kufanya yale ambayo ni muhimu kwangu na kwa wanaonizunguka kila siku.

NENO LA LEO.

I am not bound to win, but I am bound to be true. I am not bound to succeed, but I am bound to live by the light that I have. I must stand with anybody that stands right, and stand with him while he is right, and part with him when he goes wrong.

Abraham Lincoln

Sio lazima nishinde, lakini lazima niuwe mkweli. Sio lazima nifanikiwe lakini ni lazima niishi kwa mwanga nilionao. Nitasimama na yeyote anayesimamia ukweli, na nitasimama naye wakati yuko sahihi, na kuachana naye wakati anapoacha ukweli.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.