Katika maisha haya tunakutana na vitu vingi ambavyo tusipopata namna sahihi ya kukabiliana navyo tunaweza kujikuta tumepoteza dira au hata kutoka nje ya kusudi la sisi kuwepo hapa duniani. Maana kuna mwingine anakuwa anategemea maoni ya wengine ili aweze kuendelea kufanya kile anafanya, mwingine anapokea na kuamini kila anachosikia kuhusu wengine wanavyomuona, na hiyo inamfanya aishi kwa namna hiyo, naweza sema ni anakuwa ameruhusu aendeshwe kutoka nje, aendeshwe na dunia . 

LICHA YA UGUMU, ENDELEA KUNG’ANG’ANA.

 
Sisemi kwamba tusisikilize ushauri au maoni ya wengine, lakini ni vyema zaidi kama utajijua na kuelewa kwa nini upo ulipo na kwa nini unafanya unachofanya, ukiyaelewa hayo hakutakuwa na kitu chochote cha nje cha kukufanya uache au kupunguza kasi ya kufanya kile unafanya, maana wewe ndiwe mwenye kujua kwa nini unafanya na si mtu wa nje, hivyo inakuwa ni wajibu wako wewe kuwafanya wale waje waone kuwa vile walivyofikiri upo si sahihi, waone kuwa walivyoona si sahihi, kipo kitu utakuwa umewafundisha hata hao wenye mtazamo hasi juu ya kile unafanya, huko kutojali au kukatishwa tama na maoni yao mitazamo yao itawafanya kwa wenye akili na hekima kukaa chini na kutafakari upya, inaweza kuwasaidia hata wakati mwingine watafikiria kidogo kabla ya kuanza kutoa maoni kwa watu katika shughuli zao, unaweza kuwafanya wakawa ni watu wa kuwafanya watu wazidi kuendelea vizuri badala ya kuwa ni waua ndoto za watu kwa kuwakatisha tama.
SOMA; Hakuna Nguvu Inayopotea, Endelea Kuweka Juhudi.
Lakini bado hata kama unakutana na watu wa namna hiyo, unatakiwa usiwachukie , wapende tu hata kama hupendi namna wanavyokupinga katika yale unayafanya. Ndio namaanisha wapende tu lakini kwa kuwa nawe una akili timamu upime yale wanakuambia, usiwe mtu wa kumeza au mtu wa ndio tu kila wakati, umepewa akili na muumba wako itumie, mtu akikuambia uko hivi, waweza kaa na kujiuliza au kuchunguza kweli niko kama anavyosema huyu mtu? Lakini ikiwa unaelewa kuwa upo kama vile muumba wako alivyokuumba sidhani kama itakupa shida, upo kufanya kile alichokuleta uje kufanya duniani, lakini ukielewa zaidi kuwa wewe ni wa peke yako, yaani hakuna mwingine kama wewe kabisa hapa duniani, ukiyaelewa yote haya itakusaidia sana kukabiliana na mtu anayekuja na mambo ya ajabu, labda ya kujaribu kukulinganisha na watu wengine, unaweza kumkumbusha tu ikiwa amesahau au kumjulisha kuwa wewe haufanani na mwanadamu mwingine awaye yote, wewe ni wewe, akuone wewe kama wewe, asitake kuona mtu mwingine kwako, na waweza fanya haya kwa kuendelea kufanya kile unafanya ili mradi unajua upo sahihi. Kifupi unaweza kumsaidia mtu huyu hata naye akapata muda wa kujielewa zaidi , kuelewa utambulisho wako na wengine, utamfundisha hata namna ya kuhusiana na watu vizuri.
Kwa mfano kuna baadhi ya watu wanasema watanzania wengi ni wavivu, si watendaji wazuri kazini, kunaweza kuwa na ukweli kwenye hilo lakini labda kwa kuwa hao watu kweli wamekutana na watu wa aina hiyo, unaweza kuwafanya wafikiri upya kwa kuwa mchapa kazi bila kujali utaifa wako, ndiyo wewe unao uwezo wa kuwafanya wabadili vile wamekariri, kuwafanya wajue kuwa maisha si kukariri, yaliyojiri jana yaweza badilika leo, au kwa kuwa yule alikuwa hawezi haimaanishi kuwa wote hawawezi.
Huenda katika maisha yako, kuna jambo unalifanya na hauoni faida au maana ya kufanya hilo jambo. Inaweza kuwa hata ni kazini kwako, umekuwa ukifanya kazi kwa bidii kama inavyotakiwa kuwa lakini bado haujaona faida ya hilo au bado umeonekana kwa mtazamo mwingine tu. Na pengine hali hiyo inakufanya uanze kujiangalia upya na kufikiri kuwa labda kipo kitu ambacho hakiendi au kufanyika sawasawa, labda kuna wakati hata mawazo ya kuacha jambo hilo kabisa yanakuja kichwani mwako, pengine unafikiria kuahirisha kwa muda na kufikiria jambo jingine.
SOMA; Sababu 7 Zinazokufanya Upoteze Hamasa Kwa Kile Unachokifanya.
Pengine wewe ni dada /kaka wa nyumbani tu, unafanya kazi za nyumbani na kila mtu anakuona kama wewe si kitu, wewe si wa maana kabisa na hiyo inakufanya uanze kufikiria sana vile jamii inakuona, vile wengine wanakuona na hali hiyo kwa namna moja au nyingine yaweza kuathiri namna unatekeleza majukumu yako. Ni kweli kwamba hakuna mtu anaona maana ya unachofanya au pengine wanaona wakikusifia au kuonyesha kukubali watakuwa wamejishushia heshima, ikiwa wewe mwenyewe ndani mwako unaona na kusikia kabisa kuwa umefanya vyema kwa kadri ya uwezo uliojaliwa basi hupaswi kuacha kufanya mema kwa sababu yoyote ile, pengine hupendwi, huheshimiwi na kero nyinginezo nyingi tu. Kuna wengine wamechagua kukuona wewe kama mfanyakazi wa ndani tu, hawataki kuona zaidi ya hapo, hivyo kama kipo cha zaidi kwako hawawezi kukiona na si kwakuwa hakipo bali kwa kuwa wao hawawezi kuona zaidi ya ile nafasi waliyokuweka au namna wanavyokukadiria.
Tambua haupo kama wanavyokuona hao, lakini pia ujue kuwa haufanyi hilo jambo ili mtu akusifie au kukufurahia, fanya na endelea kufanya kwa kuwa wewe mwenyewe unafurahia kufanya mambo mema, kufanya mambo mazuri, ndiyo si unajua tunatakiwa wote kwa kutumia vipawa vyetu tuzidi kuifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi, hivyo endelea kufanya kile umewekewa na Mungu ndani mwako, usisubiri kukubaliwa na wanadamu wote, pengine wewe unatakiwa tu kugusa maisha ya mtu mmoja na kumsaidia huyo tu, hivyo usiache kufanya kitu kwa kuangalia wingi wa wale wanakukubali, watu wengine wapo kwa ajili ya kukatisha tamaa au kulaumu tu, kuna mwingine yeye hawezi kukubali kuwa mwingine kafanya cha maana , yaani yeye hana hiyo kabisa, anafurahia kukatisha watu tama tu, hivyo ili kukabiliana na hilo ndio maana upo umuhimu wa wewe kuelewa nafasi yako ili uwe hapo na asiwepo wa kukuyumbisha.
Imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255 755 350 772