Moja ya maswali ambayo huwa napokea sana kutoka kwa watu wanaotaka kuanza biashara huwa ni biashara gani waanze kwa mtaji kidogo wanaokuwa nao. Mfano wa swali huwa, “nina laki tano, naweza kuanza biashara gani kwa kiasi hiki cha fedha?” swali hili huwa linaulizwa mara nyingi sana kwa viwango vidogo na hata vikubwa. Huenda na wewe limekuwa swali ambalo linakutatiza kwa muda mrefu.

Jibu la swali hili ni kwamba biashara yoyote unaweza kuanza na mtaji kidogo, hivyo swali la msingi sio biashara gani ufanye kwa mtaji huo kidogo, bali ufanyeje biashara yako pale unapoanza na mtaji kidogo. Kabla hatujaendelea mbele naomba uwe umeelewa vizuri hapo. Swali sio biashara gani nifanye kwa mtaji kidogo, maana jibu lipo wazi kwamba biashara yoyote unaweza kufanya kwa mtaji kidogo. Swali la msingi sana unalotakiwa kuuliza ni ufanyeje biashara unayotaka kufanya pale unapoanza na mtaji kidogo? Na hapa ndipo utakapopata mbinu nzuri za kukuwezesha kuendesha biashara yako vizuri.

Biashara yoyote ambayo unapenda kufanya, unaweza kuanza na mtaji kidogo na kuanzia ngazi ya chini kabisa huku ukikua kadiri muda unavyozidi kwenda. Kwa mfano unataka kuanza biashara ya usafirishaji ila huna fedha ya kutosha kununua chombo cha usafiri, unaweza kutumia mtaji kidogo ulionao na kukodi chombo cha usafiri, ukakisimamia vizuri na wewe ukapata faida ambayo utaiweka na baadaye kununua chombo chako cha usafiri.

Inawezekana kuanza biashara yoyote kwa ngazi ya juu sana, lakini sio kazi rahisi. Ndio maana hapa leo nitakushirikisha mambo matano muhimu ya kuzingatia ili kuweza kukuza biashara yako unapoanza na mtaji kidogo.

  1. Tumia mtandao ulionao sasa.

Hapo ulipo una mtandao mzuri sana, ndugu jamaa na marafiki wanatengeneza mtandao wako mkubwa. Angalia ni jinsi gani ambavyo unaweza kutumia mtandao huu kuanza na kukuza biashara yako. Labda kati ya hao kuna mtu anamiliki mali unayoweza kuitumia kwenye biashara, au wanaweza kuwa watu wanaofaa kuwa wateja wako. Au kama unaaminika(kitu tutakachojadili hapo chini) wanaweza kuwa chanzo cha kukuza mtaji wako. Kaa chini na angalia kila mtu ambaye yupo karibu yako ana kitu gani kinachoweza kuisaidia biashara yako zaidi. Pia unaweza kufikiria mitandao yao wao inawezaje kukusaidia wewe. Ukifanya hivi utaona nafasi kubwa ya kuweza kukuza biashara yako.

  1. Kuwa mwaminifu na aminika kwa wengine.

Mtaji mkubwa sana kwenye biashara ni uaminifu. Na mtaji pekee kwa mtu anayeanza biashara kwa mtaji kidogo ni uaminifu. Kwa kuwa mwaminifu utaweza kutumia mtandao wako vizuri kwenye kukuza biashara yako. kwa kuaminika na wengine unaweza kuwashawishi wakachangia kwenye ukuaji wa biashara yako. Kwa mfano unaweza kuchukua vitu kutoka kwa wauzaji wa jumla bila ya kulipia na ukaenda kuuza kisha ukaja kulipa. Au ukachukua fedha za wateja na baadae ndio ukawapa bidhaa au huduma wanazohitaji. Hili linahitaji uaminifu mkubwa na ukiweza kujenga uaminifu huu utakuza biashara yako sana.

  1. Kuwa na malengo makubwa na ya muda mrefu.

Wafanyabiashara wengi wanaoanza kidogo huwa wanakazana sana mwanzoni na biashara inakua kweli. Lakini baada ya muda ukuaji wa biashara unadorora na biashara inadumaa. Hii inatokana na wafanyabiashara hawa kuingia kwenye biashara bila ya kuwa na malengo makubwa. Kama huna malengo makubwa, chochote utakachopata kwenye biashara yako utaona ni kikubwa. Ila unapokuwa na malengo makubwa yatakusukuma kuendelea kuweka juhudi ili kuweza kuyafikia. Hutaridhika haraka na kuona kama umepata sana.

  1. Kuwa mbunifu na jitofautishe.

Unapoingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo, usianze kufanya kama vile ambavyo wafanyabiashara wazoefu wanafanya. Usiige jinsi wao wanavyoendesha biashara zao, inaweza kuwa vigumu sana kwako. Kuwa mbunifu na mara zote jitofautishe. Chochote unachofanya kwenye biashara yako hakikisha kinaleta thamani kwa mteja na kuweza kukuza biashara yako. angalia ni fursa gani zinazojitokeza kila siku na hakikisha unazitumia vizuri. Kama wafanyabiashara wengine wanasubiria wateja waje, wewe nenda kawafuate wateja kule walipo. Mbinu za kibunifu kama hizi zitaiwezesha biashara yako kukua sana.

Unaweza kuanzisha na kuendesha biashara kwa kuanza na mtaji kidogo. Kikubwa unachotakiwa kujua sio biashara gani ufanye, bali ufanyeje ile biashara ambayo umechagua kufanya. Tumia mtandao wako, kuwa mwaminifu, weka malengo makubwa na kuwa mbunifu na kujitofautisha na wafanyabiashara wengine. Kitu muhimu zaidi ni kuwa tayari kufanya kazi kwa juhudi sana na kuwa mvumilivu. Kwa njia hii utaweza kukuza biashara yako kwa kiasi kikubwa.

Kila la kheri.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani