Pamoja na malengo na mipango mizuri ambayo unaiweka kabla ya kuanza kufanya jambo lolote, bado huna uhakika wa asilimia 100 kwamba utafanikisha kufanya.
Na nafasi ya kushindwa ni kubwa kuliko ya kushindwa.
Kwa kifupi utashindwa, katika baadhi ya mambo ambayo utakuwa umepanga kufanya.
Sasa kushindwa sio tatizo, ila kinachotokea baada ya kushindwa ndio kinaweza kuwa tatizo au kisiwe tatizo. Hiki ndio kinaamua kama utakuwa na maisha ya mafanikio au maisha ya hivyo.

Unaposhindwa, unaweza kufanya moja kati ya mambo haya mawili;
Moja; “nilijua sitaweza”, nilijua tu lazima nishindwe, mimi siwezi kufanya jambo lolote kubwa, siwezi kubadilika, nina kisirani kwa kila kitu ninachofanya. Unaweza kujilaumu kwa kila kitu ambacho kimetokea na kuona labda hukupangiwa kupata mafanikio, au kuna mtu anakuzibia au chochote kile ambacho kinaweza kukupa ahueni kidogo kutokana na kushindwa kwako.
Lakini zao la njia hii ni kutokujaribu tena, au hata ukijaribu tayari unakuwa na mtazamo wa kushindwa na unashindwa tena.
SOMA; Kushindwa Hakutokei Mara Moja Kama Ajali.
Mbili; “nimejaribu kila kilichohitajika kufanyika”, najisifu kwa juhudi nilizoweka, japo sijapata majibu niliyotarajia nimejifunza mambo mengi ambayo wakati mwingine nitakuwa makini zaidi. Ninakubali kwa sasa sijapata nilichotaka, lakini nina ufahari kwa juhudi nilizoweka na ninajua wakati mwingine nitafanya kwa ubora zaidi. Hapa unajiwekea mazingira ya kufanikiwa zaidi baadae.
Na kwa njia hii unakuwa na hamasa kubwa sana ya kufanya tena na unapoanza kufanya unakuwa unafikiria kushinda na hatimaye unashinda kweli.
Je wewe unaposhindwa huwa unapita njia ipi kati ya hizo mbili?
Na je baada ya kujifunza leo umeona njia sahihi ni ipi?
Na je utaifuata njia hiyo?
Kama jibu ni ndiyo, fungua hapa usome kuna mkakati mzuri kwako kuweza kufikia ushindi mkubwa.
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba kunakonirudisha nyuma au kunipeleka mbele sio tukio la kushindwa, bali kile ninachofanya baada ya kushindwa. Baada ya kushindwa kuna njia mbili naweza kupita, njia ya kwanza ni ya kukata tamaa na kuona kwamba siwezi na hivyo kutokujaribu tena. Njia ya pili ni ya kuona kwamba nimeweka juhudi za kutosha ila mambo hayakuenda sawa, na hii inatoa hamasa ya kuendelea zaidi. Kuanzia sasa ikitokea nimeshindwa kupata nilichotaka, nitapita njia ya pili, njia ya kwanza ni mwiko kwangu.
NENO LA LEO.
I can accept failure, everyone fails at something. But I can’t accept not trying.
Michael Jordan
Naweza kukubali kushindwa, kila mtu anashindwa kwenye kitu fulani. Ila siwezi kukubali kutpkujaribu tena.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.