Kesho ni siku ambayo haijawahi kufikiwa.

Kesho ni mwizi wa ndoto kubwa za watu wengi.

Kesho ni njia ambayo umekuwa unatumia kutoroka matatizo yako.

Kesho ni siku ambayo inapatikana kwenye kalenda ya wajinga, hakuna kalenda yoyote duniani imeandikwa kesho.

leo sio kesho

Lakini tunaipenda kesho, tunaitumia kesho kila mara, na bado hatujawahi kuifikia hiyo kesho.

Unataka kuanza mazoezi lakini unasema utaanza kesho.

Unataka kuboresha kazi yako au biashara yako lakini hayo yote utaanza kesho.

Kesho kesho kesho, na haijawahi kufika halafu unashangaa mbona maisha yako hayabadiliki.

Amua kufanya sasa au hufanyi kabisa, ondoa kesho ambayo inakujengea uzembe, kwa kujifariji kwamba kesho utafanya, wakati unajua kabisa kwamba hutafanya.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako, anza hata kwa hatua ndogo sana sasa. Ni muhimu kuliko kusubiri kesho

SOMA; Kama Unataka Kuitawala Siku Yako Ya Kesho Fanya Kitu Hiki Kimoja Kesho Asubuhi.

Unakumbuka kauli mbiu ya mwaka huu? JUST DO IT.

Kuna kitu unataka? Anza kukifanya, sio maneno au kelele, onesha kwa vitendo. Lakini kusema kesho haikupi tofauti yoyote kwa sababu kila mtu anaweza kusema kesho.

TAMKO LANGU;

Nimekuwa naitumia kesho kukwepa kufanya mambo ambayo ni muhimu kwangu. Nimekuwa nafikiri kesho ndio nitakuwa na muda zaidi au mambo yangu yatakuwa vizuri zaidi. Lakini kesho hii imekuwa haifiki. Kuanzia sasa ninaacha kutumia neno kesho wakati napanga mambo yangu. Jambo lolote muhimu kwangu nitaanza kulifanya leo, hata kwa kiwango kidogo sana. Hii ndio njia ya uhakika ya kupata kile ninachotaka.

NENO LA LEO.

Never leave that till tomorrow which you can do today.

Benjamin Franklin

Kinachoweza kufanyika leo, kisingoje kesho.

 

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.