Tulipokuwa watoto, chochote ambacho tulikuwa hatujui au hatuelewi, tulikuwa tunauliza.
Na wala hatukuona aibu kwamba tutaonekana hatujui.
Tuliuliza bila ya kuwa na wasi wasi na pale tulipoona majibu hayaridhishi tuliuliza tena na tena.
Kuna wakati tulikuwa ving’ang’anizi mpaka aliyekuwa anakataa kitoa jibu anaamua kutoa ili tu kuondokana na kelele za kuulizwa kila mara.
Kuuliza huku kulitusaidia sana kuyajua mengi kwenye maisha.
Lakini sehemu fulani kwenye safari yetu ya maisha mambo yalibadilika. Ikawa sasa hutakiwi tena kuuliza maswali bali kuwa na majibu.
Ni kama kasheria fulani kwamba ukishakuwa mtu mzima basi unatakiwa kuwa na majibu.
Na ukiuliza sana utaonekana mjinga, ni afadhali ukae kimya.
Lakini kukaa kimya kunakufanya usiwe mjinga, hapana, kunazidisha ujinga.
Kwa kulazimika kuwa na majibu basi kumekuwa kunawafanya wengi wadanganye. Si unataka kuonekana una majibu? Na wakati huna majibu? Hivyo njia rahisi ni kudanganya. Na hii inazidi kuongeza ujinga na kukuzuia kufikia mafanikio.
Siri ipo kwenye kuuliza.
Kama unataka kupata maarifa zaidi uliza.
Kama unataka kupata fursa zaidi uliza.
Uliza uliza uliza, atakayekuona mjinga hiyo ni juu yake na sio tatizo lako.
Siri ya mafanikio na siri ya maarifa ni kuuliza.
Uliza kila kitu, na sio lazima kuuliza tu wengine, bali jiulize hata wewe binafsi.
Kwa mfano chochote unachofanya jiulize ndio kitu muhimu zaidi?
Jiulize kwa njia unayotumia itakufikisha unakotaka kufika?

TAMKO LANGU;
Najua jamii inategemea mimi niwe na majibu ya kila kitu. Lakini mimi sina majibu hayo. Ila najua njia bora ya kupata majibu, na njia hii ni kuuliza. Kuanzia sasa nitauliza na kuhoji kila kitu. Nitajiuliza mimi mwenyewe kwenye jambo lolote ninalofanya ili niweze kupata majibu bora kwangu.

NENO LA LEO;
Take the attitude of a student, never be too big to ask questions, never know too much to learn something new.
Og Mandino
Chukua hali ya uanafunzi, usijione ni mkubwa sana kuuliza maswali, usijione unajua sana kiasi kwamba huna kipya cha kujifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz