Msingi wa kwanza kabisa wa wewe kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako ni kuchukua majukumu yote ya maisha yako.
Yaani chochote kitakachotokea kwenye maisha yako ni juu yako mwenyewe. Huna wa kumlaumu au kumlalamikia, ni wewe mwenyewe umesababisha na hivyo unahitaji kufanya kazi kurekebisha, kama ni kosa.
Lakini msingi huu una upekee wake, yaani kuna wakati tatizo sio lako tena bali ni la wengine. Na hapa hata ukichukua hatamu bado haiwasaidii.

Kwa mfano kama upo kwenye kazi na ukaamua kwamba unataka kuweka thamani kubwa kwenye kazi yako na hivyo kuwahi kazini, kumaliza majukumu yako kwa haraka na kuomba majukumu mengine zaidi, wafanyakazi wenzako watakuchukua. Wataona wewe una kiherehere, wataona wewe unajipendekeza, wataona unataka uonekane wewe ndio uko hodari zaidi. Watakuambia kila maneno na kukufanyia kila visa. Lakini hapa wewe huna tatizo, umeamua kuwa bora na hilo linawaumiza wao, kwa sababu wanataka kila mtu awe kama wao. Hili lisikuumize, ni matatizo yao wenyewe, endelea kuweka juhudi.
Kama upo kwenye biashara, na ukaamua unafanya biashara zako kwa viwango tofauti, ukaamua unawapa wateja huduma ambayo hawawezi kuipata kokote, wewe ukawa hushindani lakini unaweka ubora zaidi, ukawa unapata faida kuliko wenzako. Watachukia. Watasema unatumia dawa, watakuambia una chuma ulete. Watakuletea kila visa kwa sababu tu umeamua kuwa tofauti. Hapa tatizo sio lako, tatizo ni lao na hilo lisikurudishe nyuma.
SOMA; Binadamu Ni Viumbe Wa Kuhukumu, Hivi Ndivyo Unaweza Kuepuka Madhara Ya Hukumu Zao.
Hata kwenye familia, labda ndugu zako wote wanaishi maisha fulani, ambayo wewe unaona hayana mantiki, na kuchagua kuishi maisha ambayo yatakupa uhuru, watachukua. Watakusema unajiona unajua sana, watasema ngoja wakuone. Na mengine mengi, hapa tatizo sio lako, tatizo ni lao binafsi.
Chochote utakachoamua kufanya, japo huingilii maisha ya mtu moja kwa moja, kuna wengi watachukia na wengine watakwenda mbali zaidi na kufanya jitihada za kukurudisha nyuma.
Usirudi nyuma, endelea kuweka juhudi, tatizo sio lako, tatizo ni lao wenyewe. Na kama unavyokumbuka vyema, hii sio safari rahisi.
TAMKO LANGU;
Najua kwa kuamua kuwa bora kwa kile ninachofanya na hata kwa maisha yangu kwa ujumla nitatengeneza maadui wengi. Najua hili sio tatizo langu bali ni tatizo la wale ambao wanakasirika pale ninapofanya shughuli zangu na maisha yangu kuwa bora. Hii ni safari ambayo nimeamua mwenyewe kuichukua na sitorudi nyuma kwa sababu yoyote ile.
NENO LA LEO.
The opinion which other people have of you is their problem, not yours.
Elisabeth Kubler-Ross
Maoni ambayo wengine wanayo juu yako ni matatizo yao, siyo matatizo yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.