Habari za leo mwanafalsafa?

Unaendelea kujifunza kuhusu falsafa yako mpya ya maisha? Hongera sana.

Na je umeshaanza kuyaweka haya unayojifunza kwenye maisha yako? kama ndio hongera sana. Kama sio unasubiri nini? Maisha uliyonayo ndio haya, na wakati huu ulionao ndio una uhakika nao, hivyo ndio wakati wa kuishi yale maisha unayoyapenda. Usisukume mambo mpaka kesho, utashindwa kuishi maisha unayoyafurahia.

Kuna kitu kimoja ambacho wanafalsafa wote wakubwa kuwahi kutokea hapa duniani, wanakubaliana ni muhimu sana katika kujenga maisha ya mtu yeyote.

Kitu hiki ndio ambacho kimeyafanya maisha yako kuwa kama yalivyo sasa. Na kama utataka kubadili maisha yako basi kabla ya kuhangaika kubadili vile ambavyo unaona kama vikwazo ni muhimu ukaanza na kitu hiki kimoja na muhimu sana.

Ni kitu gani hiko ambacho kimebeba nguvu kubwa kiasi hiki? Utajifunza leo kupitia FALSAFA HII MPYA YA MAISHA.

Kama ningekwambia kuna kitu kimoja, ambacho unacho wewe na kaka ukiweza kukibadili utaweza kubadili maisha yako na yawe vile unavyotaka, na uzuri ni kwamba huhitaji gharama kufanya hivyo, je ungechukua hatua? Najua jibu lako ni ndio, lakini nikishakwambia kitu hiko hutachukua hatua. Kwa nini, sijui, lakini nitajaribu kukushirikisha sababu hapa na wewe utaona ni kipi kinachokuzia hasa.

SIRI MOJA KUBWA YA MAISHA.

Ni siri lakini sio siri, yaani ni kitu kilicho wazi kabisa lakini wengi hatukioni, ndio maana kinabaki kuwa siri. Siri hiyo ni hii, UNAKUWA KILE UNACHOFIKIRI.

Yaani maisha uliyonayo, jinsi unavyoishi leo, mafanikio uliyonayo sasa, furaha uliyonayo na hata hofu ulizonazo, vyote ni zao la kitu hiki kimoja, FIKRA ZAKO. Kile unachofikiri kina nguvu kubwa sana kwenye maisha yako. fikra zako ndio zinajenga mtazamo wako, mtazamo wako unahamasisha matendo yako, matendo yako yanajenga tabia na tabia ndio inakujenga wewe.

Tabia yoyote uliyonayo sasa, maisha yako unavyoyapeleka, sio bahati au ajali, bali ni zao la kile ambacho kipo ndani ya fikra zako.

Wanafalsafa wote wanakubaliana kwa jambo hili moja, na ndio maana wengi wamekuwa wakisisitiza kuyadhibiti maisha yako kwa kuanza kudhibiti fikra zako. Na hata dini zote kubwa za dunia, zinaanza na fikra. Kupitia dini unajengewa fikra ambazo zitakuwezesha wewe kutenda mema kwako na kwa wale wanaokuzunguka.

MCHEZO ULIANZA ZAMANI SANA.

Sasa kama ndio rahisi hivi kwa nini kila mtu asifikiri vyema ili awe na maisha bora. Kama maisha yako ni zao la fikra zako, kwa nini kila mtu asiwe na fikra nzuri ili awe na maisha mazuri?

Kuna sababu nyingi sana zinazozuia mtu kuweza kuwa na fikra sahihi. Na moja ya sababu kubwa kabisa ni kwamba mchezo huu wa fikra ulianza zamani kabla wewe hujajua kumiliki fikra zako.

Ulipokuwa mdogo, ulikuwa huru kufikiri. Uliulizwa ukiwa mkubwa unataka kuwa na i na ulijibu kwa kujiamini na bila shaka yoyote. Uliweza kujibu unataka kuwa daktari, polisi, mwalimu na vingine vingi kwa wakati mmoja. Na wakubwa walicheka waliposikia ukisema vile, hawakukupinga, na kikubwa walijua ni utoto na ukishakua na kuweza kufikiri vizuri utaachana na fikra hizo.

Kadiri ulivyoendelea kukua, mchezo ukaanza kuuelewa. Jamii ikaanza kukujaza fikra. Huwezi kufanya hiki, huwezi kufanya kile. Watu wa aina yako hawafanyi hiki. Ukaanza kuwekewa vikwazo vingi pale ambapo ulitaka kutumia fikra zako kama zilivyokuwa zinakujia. Na wakati mwingine ulipokuwa unajaribu kuendelea kuzifanyia fikra zako kazi, licha ya kukatazwa, ulipata adhabu kali.

Kwa misukosuko yote hii ukakubali, ukaona ya nini kuhangaika, kwa nini nisiende tu kama vile ambavyo kila mtu anaenda, nikawa na maisha ya kawaida na mambo yakaenda. Ulipokubali hili tu ndio ukawa umeharibu kila kitu. Kwa sababu maisha yako yote yamekuwa yakijengwa kwenye fikra ambazo sio sahihi kwako kulingana na uwezo wa tofauti uliopo ndani yako.

Jamii inayokuzunguka inakusukuma kufikiri vile ambavyo kila mtu anafikiri na hivyo kuishia kuwa na maisha yale ambayo kila mtu anayo.

MAWAZO YAKO YANAVUTA VITU.

Kinachofanya maisha yako yawe zao la fikra zako ni kwamba mawazo yako yanavuta vitu. Kile kitu ambacho unafikiria kwa muda mrefu ndio ambacho utakuwa unakiona mara nyingi. Hii sio kwa sababu ni hiko tu kinapatikana, bali kwa sababu wewe umekazana kuona hiko basi utakiona kwa wingi. Kila kitu kipo, kila fursa ipo, lakini kama wewe unatafuta matatizo, kama unatafuta changamoto kwenye kila fursa, utaishia kuziona nyingi sana.

Hata ile tunayosema ni bahati nzuri au bahati mbaya/kisirani inatokana na mawazo.

Mtu ambaye anaambiwa na kuamini kwamba ana bahati nzuri, maana yake fikra zake zinakuwa zinafikiri vitu vizuri. Na kwa sababu dunia imejaa vitu vizuri na vibaya, basi yeye ataona vizuri zaidi. Na hivyo atazidi kupata bahati na ataonekana kweli ana bahati.

Mtu ambaye anaambiwa na kuamini kwamba ana bahati mbaya au kisirani, chochote anachofanya, fikra zake zipo kwenye kufanya vibaya na kushindwa. Na pale anapokutana na changamoto, anatangaza kushindwa na kukubali kwamba yeye hawezi kwa sababu ana bahati mbaya.

Yote haya yanaanzia kwenye fikra zako halafu yanajitokeza kwenye maisha yako.

KUSHINDWA NA UTUMWA UNAANZIA KWENYE FIKRA.

Kushindwa na utumwa unaanza na fikra zako. Hata kama ungefungwa kwenye gereza gani, bado hakuna anayeweza kufunga fikra zako ila wewe mwenyewe.

Hata kama ungekuwa unateswa na kunyanyaswa kiasi gani, hakuna anayezinyanyasa fikra zako ila wewe mwenyewe.

Watu wengi wanaoona wananyonywa, kunyanyaswa na kuteswa, ni kwa sababu wameruhusu fikra zao kuchukua mawazo haya na kuishi kulingana nayo. Kama mtu angeweza kubadili fikra hizi angeweza kuona njia nyingi za kuweza kuondokana na hali aliyonayo sasa.

Hakuna hali yoyote ambayo ni ya kudumu kwenye maisha yetu. Bali fikra zetu ndio zinafanya hali zile zidumu.

Masikini ataendelea kuwa masikini kwa sababu ana fikra za kimasikini. Anafikiria ataondokana na umasikini pale ambapo atashinda bahati nasibu, au atakapopewa msaada mkubwa. Hivyo fedha ndogo ndogo anazopata anatumia zote, akijua fedha kubwa ikija ndio itamletea utajiri.

Tajiri ataendelea kuwa tajiri kwa sababu ana mawazo ya kitajiri. Anajua hakuna njia rahisi ya kupata utajiri kama vile masikini wanavyoamini kwenye bahati nasibu. Anajua hakuna atakayekuja kumpa msaada mkubwa wa kumfanya awe tajiri. Anajua ya kwamba kipato kidogo anachopata, akikitumia vizuri ndio kitamjengea utajiri.

Hata ule usemi kwamba mwenye nacho huongezewa, hauendi kwenye mali tu, bali chochote ambacho unacho sasa utaongezewa. Hii ni kwa sababu utaendelea kufikiri vile na fikra hizo zitaendelea kukuletea kile unachopata sasa. Hivyo masikini ataongezewa umasikini na tajiri ataongezewa utajiri.

UNAISHI KULINGANA NA PICHA ILIYOPO KWENYE AKILI YAKO.

Hapo ulipo, kuna picha ambayo umejitengenezea kwenye akili yako. unajua kabisa jinsi ambavyo unafanya kazi zako au biashara yako, jinsi ambavyo unaendesha maisha yako, jinsi unavyotumia kipato chako na kila eneo la maisha yako.

Kila siku unaishi kulingana na picha hii na huwezi kufanya jambo lolote ambalo liko nje ya picha hii ambayo umekuwa unaitunza kila siku. Picha hii inatokana na mawazo ambayo umekuwa nayo kwenye akili yako kwa muda mrefu.

Picha uliyojitengenezea kwenye akili yako unaweza kuwa umeitengeneza mwenyewe, kulingana na unavyofikiri au ukawa umetengenezewa na jamii inayokuzunguka kutokana na wanavyokuchukulia.

Kwa mfano mtu anaweza kuwa anaambiwa yeye ni mvivu yangu akiwa mdogo. Hivyo anakua akiamini kwamba yeye ni mvivu. Hivyo hata kwenye kazi zake akitaka kuweka juhudi anakumbuka kwamba yeye ni mvivu na kila mtu anajua ni mvivu hivyo anarudi kuishi picha yake hii.

Mtu ambaye tangu anakua anaambiwa wewe ni mkorofi, basi atakua akiamini hilo na hata atakapojikuta kwenye changamoto atajikumbusha yeye ni mkorofi na kutumia ukorofi wake.

MAMBO MUHIMU YA KUFANYA ILI KUWA NA MAISHA BORA.

1. Jua kwamba maisha yako yanatokana na fikra ambazo umekuwa unaweka kwenye akili yako. jua hakuna kinachotokea kama ajali kwenye maisha yako, bali dunia inakujibu kile ambacho unauliza na unauliza kwa fikra ambazo unakuwa nazo kwa muda mrefu.

2. Pitia fikra zote ambazo unazo kwenye akili yako, pitia tabia zote ambazo watu wanakusifu kuwa unazo. Halafu angalia katika hizi ni zipi zinazofanya maisha yako kuwa bora. Katika yale mambo ambayo unaamini, ni yapi ambayo yatakuletea maisha bora. Katika zile tabia ulizonazo, ni tabia zipi ambazo zitakufanya uwe na maisha bora.

3. Amini kwamba unaweza kubadili chochote ambacho hakikuletei matokeo unayotaka. Baada ya kujua tabia au fikra ambazo zinakurudisha nyuma, jua kwamba unaweza kubadili. Na kubadili huko huhitaji kutumia nguvu kubwa, bali unahitaji kuanza kwa kubadili fikra ulizonazo, unahitaji kujijengea picha mpya ya maisha yako na kuiweka kwenye akili yako. kwa mfano kama ulikuwa unaamini siku moja utakuwa tajiri baada ya kushinda bahati nasibu au kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja, ondokana na mawazo haya kwa kufikiri kuanza kutumia kipato ulichonacho sasa na kukikuza mpaka kufikia kile kiwango cha utajiri unachotaka.

4. Kuwa na mawazo chanya muda wote kwenye akili yako. na yasiwe chanya kwako tu bali hata kwa wengine. Usifikiri ukishakuwa na amwazo chanya juu yako basi umemaliza. Wazo lolote hasi utakalokuwa nalo juu ya mtu mwingine linakurudia wewe pia. Kwa mfano kama hutaki umasikini, na unataka utajiri, hatua ya kwanza ni kuanza kufikiri mawazo ya kitajiri, kuacha kulalamika na kuchukua hatua. Lakini wakati huo huo kama unawasema vibaya matajiri kwa kuona ni watu wenye roho mbaya, wanadhulumu wengine na mawazo mengine kama hayo, hutaweza kuwa tajiri. Kwa sababu mawazo haya hasi juu ya wengine yatarudi kwako mwenyewe na kukuzuia kufikia hali hiyo.

5. Epuka mawazo hasi na yatakayokurudisha nyuma. Hofu ni moja ya mawazo hasi ambayo yanaweza kukurudisha nyuma. Kupitia hofu unapata picha ya vitu vibaya ambavyo bado hata havijatokea. Na kwa kuwa mawazo yako yanaumba, basi unajikuta ukipata yale ambayo unayahofia. Mawazo mengine hasi ni kama kukosa uaminifu, kutaka kuwadhulumu wengine, kutaka kupata zaidi kwa kutoa kidogo.

6. Nena mambo chanya kwako binafsi. Kila mmoja wetu kuna mambo ambayo huwa anajinenea. Kuna wakati ambapo unazungumza wewe na nafsi yako. hakikisha mazungumzo yoyote unayofanya na wewe binafsi yanakuwa mazungumzo chanya. Na pia tengeneza maneno chanya ambayo utakuwa unayatumia wakati unapotafakari maisha yako. Maneno haya yatakusaidia kubadili fikra zako kwa kiasi kikubwa na hivyo kuweza kubadili maisha yako.

Ondoka hapa na kitu hiki kimoja muhimu sana. UKO HIVYO ULIVYO, UKO HAPO ULIPO, UNAPATA KIPATO UNACHOPATA, UNA MAHUSIANO ULIYONAYO KUTOKANA NA MAWAZO ULIYONAYO KWENYE AKILI YAKO. MABADILIKO YOYOTE UNAYOTAKA KULETA KWENYE MAISHA YAKO, YAANZE NA MAWAZO YAKO.

Ongeza msingi huu muhimu kwenye falsafa yako mpya ya maisha, na ufanyie kazi, maisha yako hayawezi kubaki kama yalivyo sasa.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz