Unapofanya kitu cha tofauti, iwe ni kwenye kazi, biashara na hata maisha ya kawaida, kuna watu wachache watakuelewa na wengi sana hawatakuelewa. Hili sio tatizo kubwa.
Tatizo kubwa ni hili, wale wengi ambao hawatakuelewa watatumia nguvu yao ya wingi kukuzuia wewe kuendelea kufanya unachofanya sasa.

Watakukatisha tamaa kwa kukuambia haiwezekani au unakosea au watu hawataki hiko unachofanya. Lakini wale wachache ambao wanakuelewa watakaa kimya huku wanafurahia kile unachofanya.
Ni rahisi hawa wengi kukurudisha nyuma.
Lakini kama utarudi nyuma jua unawaumiza hawa wachache wanaokuelewa, wanataka kile unachofanya, wanaotaka kusikia kutoka kwako. Na hawa ndio wa muhimu sana kwako.
Katika hali kama hii usiogope kuwaambia walio wengi kwamba HII SIO KWA AJILI YAKO.
Na ukweli ni kwamba sio kila unachofanya kitamfaa kila mtu. Hakuna kitu kimoja ambacho kimewafaa watu wote. Imani ni moja lakini inazaa madhehebu mengi, na watu wanachagua kwenda kule ambako kunawafaa, japo wote kwa pamoja wanaamini kitu kimoja.
SOMA; Kuwa Kawaida Ni Kupoteza Muda Wako Na Siri Moja Ya Mafanikio Mwaka 2015
Hivyo na wewe usiumie au usione unapoteza pale ambapo baadhi ya watu wanaona unachofanya hakiwafai. Bali tumia muda wako vizuri kuwatafuta na kuwafikia wale ambao kinawafaa, na watafurahia na kunufaika sana kwa kile ambacho unafanya.
Na pia sio kila kitu ambacho watu wanafanya ni lazima uelewwe au uendane nacho. Jipe uhuru wa kuchagua kile ambacho kinakufaa wewe. Kuwa tayari kusema hiyo sio kwa ajili yangu. Usilazimike kufanya kitu kwa sababu watu wanafanya au wanategemea ufanye, fanya kwa sababu kinakufaa au ndio unachotaka kufanya.
TAMKO LANGU;
Najua sio kila kitu ambacho ninafanya watu wote watanielewa na hivyo badala ya kulazimisha watu wanielewe nitatumia muda huo kuwafikia wale wanaonielewa. Na wengine ninajua sio kwa ajili yao. Pia najua sio kila kitu ambacho wengine wanafanya lazima nielewe au niendane nacho. Nina haki ya kusema hiko sio kwa ajili yangu.
NENO LA LEO.
I don’t know the key to success, but the key to failure is trying to please everybody.
Bill Cosby
Sijui ufunguo wa mafanikio, lakini ufunguo wa kushindwa ni kujaribu kumridhisha kila mtu.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.