Ili biashara yako iweze kukua, unahitaji ongezeko la mtaji kadiri muda unavyokwenda. Na mtaji wako unaweza kuuongeza kutokana na faida unayopata kwenye biashara, japo hii itakuchukua muda mrefu. Lakini pia unaweza kuongeza mtaji wa biashara yako kwa kupokea fedha nyingi kwa wakati mmoja kutoka kwa watu au taasisi mbalimbali. Fedha hizi zinaweza kuwa ruzuku, uwekezaji au mkopo.

Katika aina hizi za fedha unazoweza kupokea kutoka kwa wengine, mkopo ndio njia ambayo wafanyabiashara wanaweza kupata. Ni wachache sana wanaopata ruzuku au fedha za wawekezaji. Na kwa sababu kwa sasa taasisi nyingi za fedha zinategemea biashara ya mikopo, mikopo imekuwa rahisi sana kupatikana kwa wafanyabiashara.

Upatikanaji huu rahisi wa mikopo umeleta matatizo kwa wafanyabiashara wengi pia. Wengi huingia kwenye mikopo na baadae kujikuta wanashindwa kuilipa mikopo ile na hivyo biashara zao kufilisiwa. Katika watu ambao wameumizwa na mikopo nimewahi kuzungumza nao kwenye kuwapa ushauri wengi wanalaani sana mikopo ya biashara na kuona ndiyo imepelekea biashara zao kufa.

Lakini katika watu hawa ambao nimewashauri baada ya kuingia kwenye matatizo ya mikopo, nimekuta kitu kimoja kipo kwa karibu watu wote. Wengi wanakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu mikopo ya biashara. Wao wanakuwa na shida ya fedha kwa ajili ya kuendesha biashara zao, benki inawafanyia tathmini na kuwaambia wanakopesheka. Wakishaambiwa wanakopesheka hiko tu ndio wanachofurahia, hawajali kingine kuhusu mikopo husika. Hivyo wengi wanajikuta wana rejesho kubwa kiasi kwamba biashara zao zinaathirika sana.

Kama ulishaingia kwenye tatizo la mkopo wa biashara au hata kama bado, leo hapa utajifunza mambo muhimu sana unayotakiwa kujua kabla hujasema NDIO nipeni huo mkopo wa biashara.

1. Jua riba ya mkopo mzima mpaka pale unapokamilisha kulipa.

Watu wengi wanapoambiwa mkopo huu ni wa riba nafuu hukimbilia kuchukua bila ya kufanya tathmini halisi ya mkopo ule. Hivyo unapoomba mkopo na ukaambiwa riba ni kiasi gani, omba kuelezwa gharama zote za mkopo na kiasi halisi utakachorejesha katika kipindi hiki cha kulipa mkopo. Wafanyabiashara wengine huogopa kuuliza taarifa kama hizi wakiona wanaweza kukosa mkopo, lakini hii ni haki yako kujua na anayekupa mkopo ana wajibu wa kukujuza yote haya.

Angalia mkopo wako kwa jumla utarejesha kiasi gani na angalia kama kweli itawezekana kwa jinsi biashara yako inavyokwenda.

2. Jua kiwango cha rejesho na oanisha na mapato ya biashara yako.

Kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wengi hufanya ni kufikiri kwamba ukishachukua mkopo basi unaweza kulipa rejesho lolote utakalopewa na taasisi iliyokupa mkopo. Hii sio sahihi na imesababisha baadhi ya wafanyabiashara kuwa na rejesho kubwa kuliko mapato ya biashara zao. Kwa rejesho la aina hii ni lazima mkopo utaacha matatizo kwenye biashara.

Wewe jua kwanza mzunguko wa biashara yako, kwa siku, kwa wiki na hata kwa mwezi. Jua mauzo yako na jua faida unayopata kwenye vipindi hivi. Baada ya kujua mzunguko huu wa fedha hakikisha rejesho unalolipa halizidi faida unayopata kwenye biashara yako. kama rejesho likiwa kubwa maana yake unakopa na kurejesha mkopo huo bila ya kuutumia kuzalisha.

Na usifikiri kwamba ukichukua mkopo faida yako itaongezeka, unaweza kuongeza mzunguko lakini faida isiongezeke. Hivyo ni vyema ukatumia hali yako ya biashara ya sasa kujipima kama utaweza kurejesha mkopo unaochukua.

3. Jua taratibu zinazochukuliwa kama utashindwa kurejesha mkopo kwa wakati.

Japokuwa hatutegemei hili kutokea, lakini wote tunajua mipango sio matumizi. Unaweza kuwa na mipango mizuri sana lakini kwenye utekelezaji ukakutana na changamoto ambazo zinakwamisha mipango hiyo. Ni vyema ukajua taratibu zinazochukuliwa na taasisi husika pale unaposhindwa kurejesha mkopo kwa wakati. Taasisi hizo zinatofautiana, kuna ambao unaweza kukaa nao chini na mkaongeza muda wa wewe kulipa mkopo, kuna wengine watachukua hatua ya kupata fedha zao ndani ya muda. Unahitaji kujua hili kabla ya kuchukua mkopo ili ujiandae mapema.

Mikopo ni mizuri sana katika ukuaji wa biashara kama itatumika vizuri. Pia kuujua mkopo kabla hata ya kuuchukua kutakusaidia sana kuweza kulipa mkopo wako bila ya kuacha biashara yako ikiwa na hali mbaya. Zingatia mambo hayo matatu kabla hujachukua mkopo ili kuhakikisha unanufaika na mkopo. Kama una changamoto yoyote kwenye biashara tunaweza kuwasiliana kwa namba zangu hapo chini na tukashauriana unawezaje kuitatua ili biashara yako iende vizuri.