Habari rafiki?

Naamini unaendelea vizuri sana, hongera kwa hilo.

Karibu tena kwenye mazungumzo haya baina yangu mimi na wewe rafiki yangu wa karibu. Sisi wote tuna lengo kubwa la kuwa na maisha bora kwetu na wanaotuzunguka. Kwa kufanyia kazi malengo na mipango tuliyojiwekeza.

Kupitia mazungumzo haya tunashirikishana mambo muhimu sana kwenye safari hii tuliyochagua. Inaweza kuwa changamoto, inaweza kuwa mbinu nzuri na chochote kile ambacho kinaweza kutusaidia.

Leo tutajadili eneo muhimu sana la maisha yetu ya kawaida na mafanikio pia. Eneo hili ni kwa wale ambao wanatuzunguka.

Kwenye kundi la SEMINA YA MIMI NI MSHINDI, mshindi mmoja aliniuliza swali;

Nitamsaidiaje mtu wa karibu yangu mfano rafiki yako kipenzi asiyependa kusoma wala kujifunza japo naona kuna umuhimu wa yeye kubadilika.

Mimi nikamjibu;

Huna njia ya kumsaidia, kama umeshamweleza umuhimu wa yeye kujifunza na kumpa mifano hai jinsi maisha yake yanaweza kuwa bora kwa kujifunza, na bado akagoma, huna tena jinsi. Wewe subiri kadiri maisha yake yatakuwa magumu atachukua hatua.

Mshindi mwenzetu akauliza tena;

Japo tuliumbiwa huruma kama binadamu, baadaye unaona anakuwa labda mzigo, je hii itatokea hata ni mwanao?

Mimi nikamjibu;

Ukishafanya sehemu yako huna tena cha kufanya. Ni lazima ukubali huwezi kudhibiti kila kitu. Huwezi kumshikia mtu mzima viboko ajifunze au achukue hatua. Na wala hilo lisikuumize kwa sababu mwisho wa siku kila mtu ana jukumu na maisha yake. Na usikubali mtu mzima mwenye akili zake timamu na mwenye nguvu ya kufanya kazi kuwa mzigo kwako. Kwa kubeba mizigo ya aina hii itakuwa vigumu kwako kufikia ushindi.

Hivyo ndivyo ilivyokwenda.

Nimeona tushirikishane hili kwa pamoja kwa sababu ni changamoto kubwa sana katika safari yetu ya mafanikio.

Kama wewe unaweka juhudi kubwa kwenye kazi yako na maisha yako, ni lazima maisha yako yatakuwa tofauti na ya wale wanaokuzunguka. Na utofauti huo ni kwamba yatakuwa bora zaidi. Kwa sababu wanaokuzunguka ni watu wa karibu kwako, ndugu zako au marafiki zako, huwezi kuwaacha hivi hivi, ni lazima uwasaidie si ndio?

Sasa unawezaje kuendelea kuwasaidia kama unaona wana nafasi ya kuchukua hatua lakini hawafanyi hivyo? Hata kama una huruma kiasi gani, kwa watu kama hawa ni lazima utajisikia unabeba mzigo mkubwa, na watazidi kukurudisha nyuma.

Changamoto moja ya kuwa mwenye mafanikio pekee kwenye kundi kubwa la wasio na mafanikio ni kwamba kila mtu anakuangalia wewe. Sasa kama na wewe ukiwa ni mtu wa huruma na kuona wanastahili kupata tu msaada wa moja kwa moja, itakuumiza sana.

Badala ya wewe kutoa msaada wa moja kwa moja kama fedha, wawezeshe na wao kuboresha maisha yako, waoneshe njia ulizopita na wao wapite. Na kama hawatataka, na wengi hawataki, basi huna njia nyingine ya kuendelea kuwasaidia.

Kama unafikiri kuendelea kuwapatia msaada wa moja kwa moja basi jua unajitengenezea maadui wakubwa sana.

Kwa sababu kama ni ndugu zako, msaada wowote ambao utakuwa unawapa, bado wataona hautoshi. Huwa wanakuwa na mawazo yao ya ajabu sana kuhusu wewe, wanaweza kuona una fedha nyingi sana na wao unawapa kidogo. Hawajui hata kama fedha unazo nyingi una mipango nazo na sio za kutoa tu kiholela.

Na wengine watafikiri wewe huna mipango mizuri na fedha zako. Wataona wao wana maoni bora zaidi ya matumizi yako ya fedha kuliko uliyonayo wewe. Kwa kifupi unakuwa unajitengenezea mzigo mzito na ambao hautaisha lawama.

Hivyo wasaidie sana wale walio karibu yako, kama ni watu wazima na wana nguvu z akufanya kazi, nao waweze kuboresha maisha yao. Wasaidie watu kuwa na njia zao za kujitengenezea kipato, hii itawajengea nidhamu na kuweza kujijengea maisha yao ya kujitegemea, na mwishoni mtaheshimiana.

Vipi kama ukiwapa mwongozo hawafanyi?

Unaweza kuwasaidia watu kuweza kuboresha maisha yao ila wakawa hawataki. Ndio kuna watu wengi ambao wamewasaidia ndugu zao labda mitaji ya biashara na mwishowe wakafanya hovyo na kuua biashara, wakasaidiwa tena na tena lakini bado wakaendelea kuharibu.

Katika nafasi kama hii huna njia nyingine ya kumsaidia, ni kusubiri kama maisha yakombana sana anaweza kubadilika mwenyewe. Japo utatamani sana kuleta mabadiliko kwake lakini atakukwamisha.

Nakumbuka siku moja niliwahi kupigiwa simu na mzazi ambaye alinieleza kuhusu kijana wake ambaye amehangaika naye sana lakini anaharibu. Hivyo alikuwa ananiomba niwasiliane naye nijaribu kumshauri ili aweze kujenga maisha yake vizuri. Mzazi huyu alitaka anipe namba ya kijana wake halafu nimpigie simu kwa ajili ya ushauri. Nikamwambia sitaweza kufanya hivyo. Akaniambia atalipia gharama zote ambazo nitahitaji ili niweze kuwa kocha wa huyu kijana wake, yaani niwe mshauri wake wa moja kwa moja. Nilimwambia tatizo sio fedha, tatizo ni utayari wa mtu. Kama yeye mwenyewe hana utayari wa kupata ushauri hawezi kuufanyia kazi, sana sana ataona nafuatilia maisha yake. Nilimshauri aongee naye kwamba anaweza kupata ushauri mzuri na ampe namba yangu anipigie. Sikusikia tena kutoka kwake wala kwa mtoto wake.

Hata ukilipia gharama nyingi kiasi gani, kama mtu hajawa tayari kubadili maisha yake, atasumbua tu.

Hivyo kama umefanya kadiri ya uwezo wako, lakini bado mtu amegoma, usijisikie vibaya, usitake maisha yako hovyo kwa sababu ya mtu mzima ambaye amechagua kuwa na maisha ya hovyo. Endelea kufanya maisha yako kuwa bora na kama mambo yakiwa magumu sana kwao watakuja wakiwa tayari kubadilika. Na hata utakuwa umewasaidia vizuri sana.

Hata uwe na mapenzi mema kiasi gani na mtu, mwisho wa siku yeye mwenyewe ndiye mwenye maamuzi ya mwisho juu ya maisha yake, kama anataka yawe bora au la.

Fanya kadiri ya uwezo wako, ila usikubali kabisa mtu mzima mwenye akili timamu na mwenye nguvu za kufanya kazi awe mzigo kwako. Utajizuia sana kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Naamini umetoka na kitu cha kwenda kufanyia kazi, kifanyie kazi ili kuwa na maisha bora kwako na kwa wale wanaokuzunguka.

MAKALA ZA KUSOMA LEO;

Soma makala hizi ambazo zitakuandaa vyema kwenye safari yako ya mafanikio makubwa;

1. Biashara za familia zina changamoto nyingi. Mwenza wako au wanafamilia wenzako wanaweza kuwa chanzo cha biashara yako kufa. Soma hapa ujue njia ya kuepuka hilo; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Mwenza Wako Anapokuwa Chanzo Cha Biashara Zako Kufa.

2. Najua wote tuna ndoto nzuri sana za kuibadili dunia, ila kabla hatujafanya hivyo hebu tumalize hili muhimu sana kwa kila mmoja wetu kufanya; Kabla Hujafikiria Kutatua Matatizo Ya Dunia, Fanya Hili Muhimu…

3. Hofu ya kukataliwa imekuwa kikwazo cha wengi kushindwa kuingia kwenye biashara. Soma hapa ujue jinsi ya kuishinda hofu hii; Jinsi Ya Kuishinda Hofu Ya Kukataliwa Kwenye Biashara.

Soma makala hizo tatu na fanyia kazi yale utakayojifunza.

Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako;

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

AMKA CONSULTANTS.