Habari za wakati huu rafiki?
Naamini uko vizuri sana, mimi pia nipo vizuri.
Karibu tena leo kwenye mazungumzo yetu haya muhimu, ambapo mimi na wewe tunazungumza kama marafiki.
Leo nataka nikuambie kitu kimoja ambacho nakuhakikishia utakutana nacho mara kwa mara. Na siku utakayoacha kukutana nacho, ni siku utakapoondoka kwenye dunia hii.
Ukijua kitu hiki na kukikubali, unabadili kabisa mtazamo wako wa maisha, na utajikuta unaishi maisha ya furaha na ya kujiamini. Usipojua kitu hiki unaweza kuona maisha yako yana mikosi kila mara na unaweza kukata tamaa kabisa. Kitu ambacho ni marufuku kabisa kwako wewe kama rafiki yangu kufanya.
Halafu sijawahi kukuambia vitu vitakavyofuta urafiki wetu mimi na wewe eh? Nitakuambia siku nyingine.
Kabla sijakuambia kitu hiko muhimu, wacha nikushirikishe kitu muhimu kutoka kwa rafiki yetu.
Kuna kijana mmoja ambaye mimi ni kocha wake, amekuwa akisoma AMKA MTANZANIA kwa karibu miaka miwili sasa na alikuwa mkoani huko. Siku za hivi karibuni alikuja dar na alinitafuta sana tuweze kuonana. Tulionana na tulizungumza mengi sana, na niliona hazina kubwa ambayo ipo ndani yako. lakini pia mazingira yake yalikuwa magumu sana. Ninaposema magumu namaanisha magumu kweli, na hata nikikueleza unaweza usiamini.
Lakini ujasiri wa maisha aliokuwa nao ulinifanya nione ana kitu cha tofauti kabisa. Napenda sana kujifunza tabia za watu, kwa kukaa na mtu kwa dakika kadhaa nakuwa nimeshajua mengi kutoka kwake.
Basi kijana huyu aliniomba niwe kocha wake na kwa sababu niliona shauku yake kubwa ya kutaka kuboresha maisha yake, nilimkubalia. Tulikaa chini na kukubaliana ni biashara gani aanze nayo, hii iwe kama sehemu yake ya kujifunza, kupata uzoefu, kuonesha kile alichonacho na kadiri siku zinakwenda aendelee kuongeza biashara hiyo na baadae aje kufanyia kazi ndoto zake nyingine.
Nilipenda sana mwitikio wake kwani siku chache baada ya mazungumzo yale alinipigia simu kwamba tayari ameanza biashara ile tuliyokubaliana. Siku tatu baada ya kunipigia kunijulisha ameanza biashara, alinipigia tena kunijulisha amemaliza mzigo wa aliokuwa amechukua na alikuwa amepata faida ya zaidi ya asilimia 50 ya mtaji alioweka. Alikuwa na furaha sana wakati tunaongea kwenye simu na aliniuliza, kwa hiyo kocha hii faida yote niweke kwenye mtaji eh? Nikamwambia hapana, endelea na mtaji ule ule tuliokubaliana mwanzo, hivyo faida iweke pembeni kwa sasa.
Baada ya wiki kuisha alinitafuta tena akitaka tuwe na mazungumzo kwa simu. Tulipanga mazungumzo ambayo ilikuwa ni mwanzoni mwa wiki hii. Wakati naongea naye nilijua kuna kitu hakiko sawa kwa sababu alikuwa anaongea kwa chini sana, aliniambia alichukua mzigo mwingine kwa mtaji ule ule, ila kwa wiki nzima hajaweza kuuza hata nusu ya mzigo aliochukua. Alikuwa anaelekea kukata tamaa.
Fikiria mzigo wa kwanza kauza ndani ya siku tatu na faida kubwa, mzigo mwingine wiki imeisha na hajauza hata nusu, ni jambo linaweza kukuumiza sana hasa kama hujawahi kufanya biashara.
Na hiki ndio nilikuwa nakisubiri kwake, hiki ndio kilinifanya nimwambie asiweke ile faida kwenye mtaji. Kwa sababu alikuwa hajakutana na changamoto bado.
Tulifanya mazungumzo na tulikubaliana kuna makosa mengi sana alikuwa anayafanya ambayo yalimletea changamoto hiyo. Tulikubaliana ayafanyie kazi halafu tuwasiliane tena.
Huyu ni mmoja wa vijana ambao naona atadumu kwenye coaching na kama atakwenda vizuri siku nyingine nitakuletea hadithi yake kwa ukamilifu.
Watu wengi wanaokuwa wanahitaji niwe kocha wao wamekuwa wanaishia njiani kwa sababu mbalimbali. Wengi wamekuwa wakitaka vitu vitokee haraka sana na sababu kubwa sana ambayo tutajadili leo ni wanapokutana na changamoto wanaharibikiwa kabisa.
C.H.A.N.G.A.M.O.T.O.
Nimeandika hivyo kwa msisitizo ili unaposoma uone ni muhimu.
Changamoto ndio kitu ambacho ninakuhakikishia utaendelea kukutana nacho kila siku mpaka siku unaondoka hapa duniani. Ukiwa huna hela unaweza kufikiri ukiwa nazo changamoto zinaisha, ni kweli zinaisha ila unakaribisha changamoto nyingine za kuwa na hela.
Hivyo kama kuna kitu unatakiwa kukipenda, kama kuna kitu unatakiwa kuwa tayari nacho kwenye maisha yako, basi ni changamoto.
Kwenye jambo lolote unalofanya kwenye maisha yako, hata uwe una uhakika nalo kiasi gani, hata uwe umebobea kiasi gani, ni lazima utakutana na changamoto. Hakuna mtu ambaye mambo yake yamemnyookea. Wewe kwa nje unaweza kuona wengi wana maisha muruwa, lakini ungepewa siku moja kuishi maisha ya mtu huyo usingeweza.
Hivyo rafiki yangu, kama kuna kitu cha kukubaliana nacho na kukitumia vyema basi ni changamoto.
USITOROKE CHANGAMOTO.
Moja ya mambo ya hovyo tunayoweza kufanya tunapokutana na changamoto ni kujaribu kuitoroka au kuikwepa changamoto hiyo. Hili ni jambo la hovyo kwa sababu haijalishi utakwepa kiasi gani, changamoto itaendelea kuwa pale, ikikusubiri. Ni lazima uifanyie kazi changamoto kama kweli unataka kuondokana nayo na kusonga mbele zaidi.
KAMA HUIWEZI CHANGAMOTO.
Sasa inakuwaje kama changamoto ni kubwa sana na huiwezi? Changamoto imekuzidi na huna cha kufanya kuitatua?
HILI NALO LITAPITA, pia ni dawa nzuri sana ya kuondokana na changamoto.
Kama huwezi kuifanyia kazi mara moja basi kubaliana nayo na jiambie kwamba hili nalo litapita. Kuna mengi yamepita na hilo litapita. Na muda ni tiba nzuri sana kwenye jambo lolote. Jukumu lako wewe ni kutokubali kupotezwa na changamoto hiyo na kutokukata tamaa, wewe endelea na kile ulichopanga kufanya, na upe muda nafasi yake ya kutenda. Utashangaa umebaki kuwa imara na changamoto imeyeyuka yenyewe.
Kwa vyovyote vile huna sababu ya kukata tamaa, huna sababu ya kuwa na maisha ya hovyo au mabovu kwa sababu ya changamoto, ifanyie kazi, au uachie muda nafasi ya kuifanyia kazi.
Kuna chochote umeokota hapa kinachoweza kukusaidia kwenye changamoto? Basi kitumie vyema.
MAKALA NZURI ZA KUSOMA;
Rafiki soma makala hizi nzuri ambazo zitakupa maarifa na hamasa ya kuweza kuendelea na safari yako ya mafanikio;
1. Fikra hasi ni sumu kubwa kwako kuwa na maisha bora, soma hapa uondokane nazo; Dalili Sita(6) Kwamba Una Fikra Hasi Zinazokuzuia Kufikia Mafanikio Na Jinsi Ya Kuondokana Nazo.
2. Umewahi kupima ni kwa kiasi gani watu wanapokea kile unachotoa? Kama bado soma hapa na ufanye kipimo hiki muhimu sana kwako; Watagundua Kama Haupo?
3. Najua kuna marafiki zangu wengi hapa mnaingia kwenye biashara huku umri wenu ukiwa umekwenda kidogo, soma hapa ujue faida uliyonayo; Je Unaingia Kwenye Biashara Ukiwa Na Umri Mkubwa? Zingatia Mambo Haya Muhimu.
4. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, hii ni sehemu muhimu sana unayopaswa kuwepo. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA
Nakutakia kila la kheri kwenye utekelezaji wa haya uliyojifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,