Habari ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri n michakato ya kila siku ya maisha. Wiki hii tunajifunza kutoka kwenye kitabu cha How to stop worrying and Start ling (Jinsi ya kuachana na hofu na kuanza kuishi maisha ya furaha). Kitabu hiki kimeandikwa na mwandishi mbobevu wa vitabu hususani kwenye tasnia ya public speaking. Kitabu hiki kinaelezea vizuri sana kwa habari ya hofu na woga, visababishi vya woga pia kinatoa mbinu mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia kupambana na hofu na kuishi maisha ya furaha. Kitabu hiki ni kizuri sana. Zaidi ya asilimia 70, Hapa nimekufupishia baadhi ya mambo 20 ambayo nimejifunza. 

 
Karibu sana
1. Tatizo letu kubwa sio ujinga (ignorance) bali ni kukosa utendaji (Inaction). Watu wanajua vitu vingi, lakini linapokuja swala la kutenda ndio tunakua wazito kutokana na hofu ya kushindwa.
2. Maisha ni sasa hivi. Tulipokua wadogo, tulikua na mawazo ya kama haya “ ngoja nikikua mkaka au mdada yaani nitafanya hili na lile”, baada ya kua mkaka au mdada, tukasema yaani nikiwa mkubwa nitafanya kile na kile lakini wapi, tukawa wakubwa, tukasema yaani subiri niolewe au nioe, nitafanya hiki na kile. Maisha ni sasa na sio yale unayoyasubiria, maisha ni wakati huo unaoishi kwa sasa.
3. Hofu ndio kisababishi kikubwa cha vifo vingi, kifo cha ugonjwa kinaongezewa kasi na hofu. Hofu inakua na mchango mkubwa sana katika kifo chochote kile. Hofu pia huharibu kinga ya mwili. Wapo watu wanapopatwa na hofu hupata hadi tumbo la kuharisha.
4. Kwa wafanya biashara wanaoshindwa kukabiliana na hofu hufa wangali wadogo. Biashara ni moja ya tasnia zenye kukumbwa na misukosuko mingi sana, kudumu kwa biashara hizo hutegemea zaidi uimara wa wamiliki wa biashara zenyewe. Kama wakiwa ni watu wakutishwa na hofu, ni wazi kwamba biashara itakufa, mbaya zaidi na hata mmiliki mwenyewe anaweza kufa kutokana na matokeo ya hofu.
5. Kanuni ya kwanza kutatua tatizo ni kufahamu ukweli wa tatizo (facts). Kwanini ni muhimu kupata facts kwanza? Ni kwa sababu bila facts hatuwezi hata kujaribu kutatua tatizo ipasavyo.
SOMA; Mambo 4 Yakukumbuka Wakati Unapokuwa Na Hofu Zaidi Katika Maisha Yako.
6. Chanzo kikuu cha hofu ni kuchanganyikiwa (Confusion). Ukiwa umechanganyikiwa ni kwamba huoni mbele badala yake unakua unaona vikwazo tu, kutokana na kutokujua nini hatima yake, hofu inakutawala.
7. Nusu ya hofu zote duniani husababishwa na watu kufanya maamuzi bila kua na uelewa wa kutosha kuhusu msingi wa maamuzi yao. Mfano kama utahitajika kukabiliana na tatizo Jumatano wiki ijayo, usifanye maamuzi leo kabla hujalifahamu tatizo vizuri, tumia muda huo kujikita katika kujifunza tatizo husika, hakikisha una taarifa sahihi za kutosha na ikifika siku yenyewe ya Jumatano tatizo litajitatua lenyewe. If a man will devote his time to securing facts in an impartial, objective way, his worries will usually evaporate in the light of knowledge.”
8. Ukikumbana na tatizo katika biashara yako unaweza kujiuliza maswali haya ili kukabiliana na tatizo kwa usahihi:
· Tatizo nini (What is the problem). Hapa unapaswa kulifahamu tatizo hasa ni nini (be specific)
· Nini kisababishi cha tatizo? (What is the CAUSE of the problem?)
· Suluhisho zote zinazowezekana ni zipi? (What are all possible solutions to the problem?)
· Je katika hizo ni suluhisho gani unapendekeza? (What solution do you suggest?)
9. Tiba ya hofu sio kuikimbia, bali kukabiliana nayo. Unapokabiliana na kile kinachokusababishia hofu unaimarika na kuongeza confidence ya kukabiliana na changamoto.
10. Hofu inaua uwezo wetu na nguvu zetu. Ukigubikwa na hofu akili inashindwa kufikiri katika kiwango cha uwezo wake.
11. Njia nyingine ya kuishinda hofu ni kwa wewe Kuwa ‘bize’ ukifanya mambo ya msingi yenye kujenga. Ukigubikwa na hofu, tafuta kazi ambayo itakufanya uwe ‘bize’, ukihusisha akili yako na mwili wako kisha jikite kwenye hiyo kazi, kwa kadri utakavyokua unafanikisha kazi hiyo ndivyo hofu itakua inapotea kwako
12. Asilimia 99 ya vitu tunavyovihofia hua havitokei lakini bado tunaendelea kung’ang’ana kuhofia vitu zaidi na zaidi. Watu wanahofu ya vitu ambavyo ni nadra sana kutokea
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kufaidika na Hofu Ulizonazo.
13. Njia moja pekee ya kua na furaha, nayo ni kuachana na kuhofu vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako. Vitu ambavyo huwezi hata kuvibadilisha usijisumbue kuvihofia maana utakua unajinyima furaha bure. Kama umekabiliana na hali ngumu, kama kuna kitu unaweza kufanya kuhusu hali hiyo basi fanya, ila kama huna uwezo achana nalo, hapa ina maana kama hali hiyo ngumu, imesababishwa na vitu ambavyo viko nje ya uwezo wako, basi achana navyo.
14. Maisha yetu yanatengenezwa na mawazo yetu. Kile unachowaza muda mwingi ndicho kinachoamua hatima ya maisha yako. Ukiwa unawaza mawazo ya furaha, utakua na furaha, ukiwaza mawazo yakuumwa au ugonjwa utaugua, ukiwa unawaza mawazo ya huzuni au hofu, ndivyo hivyo maisha yako yataendana na kile unachokiwaza. Jichunguze muda mwingi katika siku hua unawaza nini. A man will find that as he alters his thoughts towards things and other people, things and other people will alter towards him.
15. Hakuna anayeweza kukusumbua, kukufedhehesha au kukudhalilisha labda wewe mwenye umeruhusu. Tunaruhusu watu kutudharau kwa kukubaliana na mawazo yao juu yetu ama kwa kukubaliana na tafsiri zao kutuhusu sisi. Mfano mtu anakutukana, kinachokuumiza wewe sio lile tusi bali ni ule mtazamo wako kuhusu tafsiri ya lile tusi. Na ndio maana kuna mwingine anaweza kuitwa mjinga tu akakasirika hata kufikia kuleta madhara makubwa, wakati mwingine anaweza hata akatukanwa matusi yanayoitwa ya nguoni, lakini akawa mpole wala asibabaike. Mtu wa namna hii ni kwamba yeye anayotafsiri yake kumhusu yeye mwenyewe ambayo ni kubwa kuzidi matusi yenyewe. Uwezo wa kubadili fedheha kuwa fursa uko ndani yetu. Mfano mtu anapokwambia wewe unaongea broken English, kwanza unaweza kufikiri uhalisia wa ulichoambiwa, na kuona je nini ufanye ili kesho stori iwe tofauti, hivyo ukaichukulia hiyo kama fursa uliyoipata kwa kupata mrejesho, ambao umekusaidia kujiboresha. Kisha unaweza kumwambia nashukuru sana kwa mawazo yako mazuri kuhusu makosa ninayofanya kwenye kiingereza, naamini una lengo zuri la kuona nimepiga hatua, asante sana kwa kunionyesha njia, sasa nina mpango wa kuanza masomo ya lugha ya kiingereza wiki ijayo. Nakwamba kama alisema vile kwa lengo la kukudhalilisha na kukufanya ukasirike, ukimjibu kama hivyo lazima ataduwaa. Nafsi itamsuta, na atakuja kwako kujifunza mengi.
16. Usitafute furaha kwa kutaka kushukuriwa kwa vile umetoa bali toa kwa ajili ya furaha inayopatikana katika utoaji. Watu wengi tunapenda tunapomsaidia mtu kitu tupate shukrani ya msaada tuliotoa, na mara tunapokosa kushukuriwa, tunakasirika na kukosa furaha. Ni kwa sababu tunatafuta furaha kwa kupewa shukrani kwa wema tuliowatendea wengine. Kumbuka Bwana Yesu aliponya wakoma 10, lakini mmoja tu ndiye aliyerudi kumshukuru. Lakini hilo halikumvunja moyo na kumnyima furaha, bali aliendelea kuitenda kazi yake na kutimiza kusudi lake akijua kwamba furaha ya kweli ipo katika kutoa na kuwasaidia wengine pasipokujali wameshukuru ama la.
SOMA; Mbinu Saba(7) Za Kuondokana Na Hofu Ya Kuongea Mbele Ya Kundi Kubwa La Watu.
17. Janga kubwa katika dunia ya leo, ni watu kutumia muda mwingi kufikiria vile wasivyokua navyo, badala ya vile walivyokua navyo. (We seldom think of what we have but always of what we lack). Hii hufanya watu kukosa furaha, na kujihisi watupu, na kusahau vile walivyonavyo. Janga hili pengine ndilo ambalo limesababisha taabu kubwa sana kuliko vita vyote au magonjwa yoyote yaliyowahi kutokea katika historia ya dunia. Kama tunataka kuepukana na hofu na kufurahia maisha yatupasa kuhesabu baraka tulizonazo na sio matatizo tuliyonayo. Count your blessings-not your troubles!
18. Kua wewe halisi (Be yourself) maana hakuna kama wewe dunia nzima. Ukitaka kufanana na Fulani utakua hujitendei haki maana wewe ni orijino hupaswi kua kopi ya mtu mwingine. Tengeneza historia yako badala ya kufuata historia za watu wengine. Ni kweli tunapaswa kujifunza kwa wengine, lakini hatupaswi kua kama wao. Mafunzo tunayojifunza kwa wengine si kwa ajili ya kufanana kama wao, bali kutusaidia katika kujitengeneza katika uhalisia wetu. Kama mtu mwingine hawezi kua wewe jiulize kwa nini wewe uwe mtu mwingine? Why should we be the copy of others. Maintain your originality.
19. Fanya maombi. Unapokabiliwa na tatizo linalokufanya kua na hofu, hebu nenda mbele za Mungu wako na umweleze shida hiyo inayokukabili. Maana anasema njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha (Matayo 11:28). Pia Mungu huyo huyo anasema tumtwike fadhaa zetu yeye. “… huku mkimtwika YEYE fadhaa zenu zote, kwa maana YEYE hujishughulisha sana kwa mambo yenu” (1Petro 5:7). Hivyo basi hakuna haja ya kua mtumwa wa hofu kwa mambo ambayo hatuwezi kuyabadili, badala yake tumweleze Yule mwenye UWEZO huo. Prayer helps us to put into words exactly what is troubling us.
20. Hakuna anayempiga teke mbwa aliyekufa (No One Ever Kicks A Dead Dog). Unapofanya kitu kikaleta attention kwa watu, utakosolewa. Ukiona hakuna mtu anahangaika na wewe ujue basi wewe si wa muhimu, lakini ukiona kila mtu anakusema na kukukosoa ujue wewe ni wa muhimu, na yamkini wanafanya hivyo maana hawawezi kua kama wewe kwa maana umewaacha mbali. Wale wanaokukosoa hufanya hivyo ili kujihisi na wao ni wa muhimu. Watu hua hawakosoi wale walio chini, bali wale walio juu kuliko wao aidha kwa mafanikio au elimu. Ukiona unakosolewa ujue basi wewe sio mbwa aliyekufa, wewe ni wa muhimu. Angalizo: hapa haimaanishi upuuze kila ukosoaji, la hasha, ukosoaji unaozungumziwa hapa ni ule usio sahihi au usiostahili (unjust criticism).
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com