Kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho, ni kwamba kila mtu mzima na mwenye akili timamu anataka kuwa na maisha bora zaidi ya aliyonayo sasa. au kama aliyonayo sasa ni bora, basi yaendelee kuwa hivyo.

Lakini katika kufikia maisha haya bora, ndio kunakuja changamoto nyingi sana kwenye dunia yetu. Kuna ambao wanatafuta njia rahisi za kufanya hivyo, kuna wengine wapo tayari kusubiri, kuna wengine wanataka sasa na mengine mengi.

UKIWEZAKUJIWEKAKWENYE VIATU KAMA HIVI, UNAWEZA KUJUA KWA NINI MAISHA YA WENGINE YANAWEZA KUWA MAGUMU SANA.
UKIWEZAKUJIWEKAKWENYE VIATU KAMA HIVI, UNAWEZA KUJUA KWA NINI MAISHA YA WENGINE YANAWEZA KUWA MAGUMU SANA.

Katika safari hii ni rahisi sana kunyooshea wengine vidole na kuona kama wao wana matatizo sana zaidi yetu. Au hawajui kile wanachofanya. Au wanafanya makusudi kutuharibia sisi mipango yetu.

Ni rahisi kufikiria hivi kwa juu juu, lakini ukipata nafasi ya kuvaa viatu vya watu hao, utaona ni kwa nini wanajikuta wanafanya hivyo. Wakati mwingine hawafanyi kwa sababu wanapenda, ila wanafanya kwa sababu inabidi.

Kitu kimoja nataka nikuambie ni kwamba kila mtu unayemwona ana matatizo na changamoto zake, ana vita yake anayopigana ndani yake au hata na watu wengine. Unaweza kumwona anacheka lakini ndani ana vitu vingi vinaendelea, ambavyo kama angeamua kuvipa nafasi basi asingestahili kucheka.

SOMA; SIKU YA 8; Mtazamo Wako Ndio Unatawala Maisha Yako.

Hivyo kabla hujalaumu mtu, kabla hujanyoosha vidole, kabla hujalalamikia mtu, jaribu kuvaa viatu vyake na uone wewe ungefanya nini. Kama ungeweza kufanya tofauti, basi badala ya kumlalamikia utakuwa mshauri mzuri. Utamwambia kwa mimi kama ningekuwa kwenye hali hii uliyo sasa, basi ningechukua hatua hii.

TAMKO LANGU;

Kabla sijalaumu au kumnyooshea kidole mwingine, nitajaribu kwanza kuvaa viatu vyake. Nitajaribu kujiweka kwenye hali anayopitia yeye n akuona ni maamuzi gani mimi ningeweza kufanya. Na kama ni tofauti na anachofanya yeye nitamshauri kulingana na jinsi nilivyovaa viatu vyake. Hii ni njia bora ya kuwajua watu na kuwasaidia pia.

NENO LA LEO.

“Always put yourself in others’ shoes. If you feel that it hurts you, it probably hurts the other person, too.”
― Rachel Grady

Mara zote vaa viatu vya wengine. Kama utaona vinakuumiza, jua vinawaumiza na wao pia.

Jiweke kwenye ile hali ambayo mtu mwingine anapitia, ukiona hali hiyo inakuumiza wewe, jua hata yeye inamuumiza pia.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.