Tunapenda sana mabadiliko kwenye maisha yetu, lakini hakuna viumbe wagumu kubadili kama sisi wenyewe.
Ni rahisi sana kuona wengine ndio wanahitaji kubadilika.
Ni rahisi sana kuongea kuhusu mabadiliko.
Ni rahisi sana kulalamika na kulaumu pale unapoona mambo hayaendi sawa.
Lakini inapofika kwamba unahitaji kubadilika, hapo ndipo ugumu unapoanzia.

Sasa sikiliza, wewe ni mwana mafanikio, na ili ufikie mafanikio makubwa zaidi, na uendelee kubaki kwenye kilele cha mafanikio, unahitaji kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kwenye maisha yako na kile ambacho unafanya.
Kila inapojisikia kulalamika au kulaumu, acha mara moja na jiulize nibadili nini hapa?
SOMA; Wakati Wa Mabadiliko Na Kinachochochea Mabadiliko Ya Kweli.
Kwa mfano hutapata kazi au biashara nzuri kwa kulalamikia uliyonayo sasa, ni lazima ubadili kitu.
Hakuna mtu amewahi kuwa na ndoa bora kwa kulalamikia ndoa yake ilivyo mbaya kwa sasa. Ni lazima ukae chini na uone ni vitu gani vya kubadili.
Kitu chochote ambacho ni muhimu sana kwenye maisha yako unaweza kukipata kupitia mpango wa mabadiliko, ambao umejiwekea wewe mwenyewe.
Mpango wa mabadiliko ni mzuri sana kwako, je unao?
TAMKO LANGU;
Najua kitu chochote bora kwenye maisha yangu hakitakuja kwa kulalamika au kulaumu. Kitakuja pale ambapo nitafanya mabadiliko kwenye maisha yangu na kwenye kile ambacho ninafanya. Nitakapokuwa najisikia kulalamika, nitaacha mara moja na kuangalia ni kitu gani ninachoweza kubadili, kisha nitaelekeza nguvu zangu zote kwenye hiko cha kubadili.
NENO LA LEO.
“What you’re supposed to do when you don’t like a thing is change it. If you can’t change it, change the way you think about it. Don’t complain.”
― Maya Angelou
Unachotakiwa kufanya, kama kuna kitu hukipendi ni kukibadili. Na kama huwezi kukibadili, basi badili fikra zako juu ya kitu hiko. Usilalamike.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.