Kila mmoja wetu kuna mabadiliko ambayo angependa kufanya kwenye maisha yake.
Lakini wengi huwa tunashindwa kutekeleza mabadiliko haya tunayotaka.
Na moja ya sababu za kushindwa kubadili ni hatua nyingi ambazo zinahusika kwenye mabadiliko haya.
Huwa tunaweka hatua nyingi sana ambazo kuzipitia tu ni changamoto tosha.
Kwa mfano kama umeamua kuanza kufanya mazoezi, unahitaji kuwa na nguo za mazoezi, unahitaji eneo la kufanyia mazoezi na mengine mengi.
Hivyo muda wa kufanya mazoezi unapofika, unaanza kutafuta nguo za mazoezi ziko wapi, unazipata na kuvaa, kisha unaanza kufikiria kwa siku hiyo ufanye mazoezi gani. Kwa kufuata hatua hizi ni rahisi sana kushindwa kutekeleza unachotaka.
Unapopunguza hatua unazofuata kabla ya kufanya kitu, inakuwa rahisi sana kwako kufanya kile ambacho umepanga kufanya. Unaipunguzia akili kazi ya kufanya maamuzi na hivyo moja kwa moja unakwenda kwenye utekelezaji.
SOMA; Chochote Unachotaka Anza Kukitoa Na Utapokea Zaidi Na Zaidi.
Kwenye mfano wa mazoezi hapo juu, kupunguza hatua ni kujua kila siku unafanya zoezi la kukimbia kwenye uwanja wa karibu. Na pia nguo za mazoezi unaziweka eneo moja ambapo huna haja ya kutafuta. Muda unapofika, unachukua nguo na kuvaa na kuelekea uwanjani kukimbia. Kwa njia hii ya kupunguza hatua inakuwa rahisi sana kwako kutekeleza.
Kwenye jambo lolote unalofanya, iwe ni kazi au biashara, punguza sana zile hatua unazopitia katika kufanya kitu. Fanya iwe rahisi sana kwako kuanza kufanya kitu, hapo katikati kusiwe na michakato mingi ambayo inaweza kukukatisha tamaa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kadiri ninavyoweka hatua nyingi kwenye ufanyaji wa jambo, ndivyo inavyokuwa rahisi sana kwangu kukata tamaa ya kufanya jambo hilo. Kuanzia sasa nitapunguza hatua zote ninazopitia kwenye ufanyaji wa jambo. Nitahakikisha inakuwa rahisi kwangu kuingia moja kwa moja kwenye ufanyaji na sio kupitia michakato ambayo haina mchango mkubwa.
NENO LA LEO.
If you have a dream, you can spend a lifetime studying, planning, and getting ready for it. What you should be doing is getting started.
Drew Houston
Kama una ndoto, unaweza kutumia muda wako wote kujifunza, kupanga na kujiandaa kwa ajili ya ndoto hiyo. Lakini kikubwa unachotakiwa kufanya ni KUANZA kuitekeleza ndoto hiyo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
